Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Kesi mgombea binafsi yatua Mahakama ya Afrika

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mchungaji Christopher Mtikila
CHAMA cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wameishtaki Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyopo mkoani Arusha, ikidai kusikilizwa na kutoa uamuzi wa suala la mgombea binafsi.


TLS na LHRC wamedai kuwa suala la kuwapo mgombea binafsi ambalo liliwahi kuzua mjadala na gumzo nchini, ni haki ya msingi ya kikatiba.Hatua hiyo ya TLS na LHRC imekuja takribani mwaka mmoja tangu jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, kutoa hukumu iliyokubali rufaa ya serikali iliyopinga ruhusa ya kuwapo kwa mgombea binafsi nchini.


Juni 17, 2010, majaji saba wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani walitengua hukumu ya kuruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kusema suala hilo litaamuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Lakini jana akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kesi hiyo katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, Rais wa TLS, Francis Stolla alisema kesi hiyo tayari imesajiliwa na kupewa namba 009/ 2011.


Stola alisema kwamba kesi hiyo ni ya kwanza kutoka Tanzania, kwenda katika Mahakama hiyo, lakini pia kesi hiyo ina uwezekano mkubwa wa kushinda kwa kuleta mabadiliko na maendeleo ya demokrasia, haki za kiraia na za kisiasa nchini.


Alisema kesi hiyo ya kikatiba inapinga Ibara ya 39,67 na 77 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa na mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1994.Stolla alisema kwamba mabadiliko hayo yanaondoa kabisa haki ya Watanzania wa kawaida kuchaguliwa katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani kama wagombea binafsi.




Alisema kuwa hawakubaliani na utaratibu huo kwa sababu inawezekana wapo watu hawakubaliani na ilani ya chama, sera na utaratibu wa chama chochote cha siasa kilichopo, lakini sababu ya katiba, wanakosa haki yao ya kuwa viongozi na kuutumikia umma.


Alisema ibara hizo za Katiba ya Tanzania ilivyobadilishwa, inaenda kinyume na Ibara ya 13 inayoeleza haki ya mtu kushiriki katika serikali yake na ibara ya 2 inayoelezea haki ya kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu.


“Pia zinaenda kinyume na ibara ya 3 na 25 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa ya mwaka 1966 (ICCPR-1966),"alisema Stolla
Alisema hilo ni tatizo lililopo katika nchi ya Tanzania pekee, tofauti na nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), kwa sababu nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi ambazo pia ni wanachama wa EAC zinaruhusu mgombea binafsi na tayari Uganda iliwahi kuwa na mgombea binafsi kwa nafasi ya urais, licha ya nchi hiyo kuwa na migogoro ya kisiasa.


Historia ya mgombea binafsi
Oktoba 24 mwaka 1994, Mwenyekiti wa Democratic Party, Mchungaji Christopher Mtikila alishinda kesi dhidi ya Serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambayo iliruhusu kuwapo kwa wagombea binafsi.


Hata hivyo, baada ya kushinda, Serikali ilifanya marekebisho ya Katiba, badala ya kukata rufaa, ili mgombea binafsi asiwepo nchini.
Mei 5, 2006 jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo, lilitoa hukumu nyingine iliyompa ushindi Mtikila kwa kukubali kuwapo kwa wagombea binafsi, uamuzi ambao Serikali iliupinga kwa kukata rufaa.


Rufaa hiyo ndiyo iliyozaa hukumu iliyotolewa na majaji saba wakiongozwa na Jaji Ramadhani, ambayo ilibatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu na kuzuia uwapo wa wagombea binafsi nchini.


Hukumu hiyo ilipondwa na wanataaluma wengi wa sheria akiwamo mtangulizi wa Jaji Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta ambaye alisema kuwa mahakama ilikwepa wajibu na kwamba hukumu hiyo ni ishara kwamba siasa zilikuwa zimeanza kuuyumbisha mhimili wa mahakama.

0 comments

Post a Comment