IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SIKU tano kabla ya Serikali kuwasilisha bungeni bajeti yake ya mwaka 2011/2012, wachumi na wanasiasa nchini wamesema bajeti itakayowasaidia wananchi ni ile itakayopunguza matumizi yasiyokuwa ya msingi serikalini na kutoa kipaumbele katika sekta za elimu na umeme.
Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya Kambi ya Upinzani bungeni kutaja vipaumbele sita vya bajeti yake mbadala ya mwaka wa fedha 2011/2012, ikitaka kufutwa kwa posho za vikao vyote vya serikali na wabunge, huku Serikali nayo ikitangaza mwelekeo wa bajeti yake.Bajeti ya Serikali inatarajiwa kusomwa rasmi bungeni Juni 9 mwaka huu na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, sambamba na bajeti za nchi nyingine za Afrika ya Mashariki.
Tayari Serikali imeshatangaza vipaumbele 12 vya bajeti yake ambavyo ni mara mbili ya vile vya kambi ya upinzani.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi, alisema bajeti itakayowasaidia wananchi ni ile itakayopunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya msingi na kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.
Alieleza kwamba, bajeti itakayokuwa na matumaini kwa wananchi, lazima ipunguze kodi katika bidhaa mbalimbali ili wananchi waweze kumudu maisha.“Bajeti inatakiwa kuangalia jinsi ya kupunguza mfumuko wa bei kwa kina, kwa sasa maisha ni magumu
sana, kwa hiyo lazima Serikali itazame namna ya punguza hali hii,” alisema Dk Ngowi.Prof Deliphine Rwegasira ambaye pia ni mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema mbali na Serikali kupunguza kodi katika bidhaa mbambali ambazo zinatumiwa na wananchi kila siku, pia inatakiwa kuweka ruzuku katika baadhi ya sekta.
“Bajeti lazima imsaidie mwananchi. Sasa hivi mfumuko wa bei upo juu sana kwa hiyo lazima bajeti iwe jibu ya hali hii. Pia lazima mwananchi apate ruzuku kwenye sekta ambazo zitamwezesha kumudu maisha,” alisema Profesa Rwegasira.Alieleza pia kwamba, Serikali inatakiwa kuhakikisha inaondoa pengo la matumizi yake na mapato ili kuwezesha uchumi kuendelea kuwa imara na hatimaye maisha ya mwananchi yawe bora zaidi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema bajeti hiyo inatakiwa kulenga zaidi katika sekta nne ambazo ni elimu, miundombinu, afya na ulinzi na usalama.Hata hivyo, Dk Bana alisema vipaumbele sita vya bajeti ya Kambi ya Upinzani bungeni haviwezi kufananishwa na vipaumbele 12 vya bajeti ya Serikali.
Alisema kambi hiyo haina taarifa za kutosha, hivyo hutoa vipaumbele hivyo kulingana na utaratibu uliopo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Serikali inatakiwa kuimaisha vyanzo vya ndani vya mapato ili kusaidia kukua kwa uchumi utakaosaidia nchi kutokuwa na bajeti tegemezi.
Alisema Sh4 bilioni zinapotea kila siku jijini Dar es Salaam kutokana na msongamano wa magari ambapo kwa mwaka ni zaidi ya Sh500 bilioni.Alisema fedha hizo zinaweza kusaidia kuongeza kiwango cha bajeti za wizara mbalimbali na kuondokana na utegemezi.
Alisema sekta ya elimu inatakiwa kutengewa bajeti kubwa ambayo si chini ya asilimia 25 kwa kuwa kiwango duni cha elimu ndiyo chanzo cha mambo mengi ya maendeleo nchini kusuasua.
“Nadhani elimu ndio kila kitu…., Sekta hii inatakiwa kuwa kipaumbele cha kwanza kabisa na Serikali ijitahidi kuitengea fedha za kutosha,”alisema Mbatia.Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma(SAU), Paul Kyara alisema kuwa bajeti hiyo ilenge katika kuondoa tatizo la mgawo wa umeme ambao kwa kiwango kikubwa huathiri uchumi pamoja na sekta ya elimu na kilimo.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wachumi washauri izingatie elimu na umeme
0 comments