Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Lowassa atinga Kanisa Katoliki

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIKA hatua ambayo imeibua tafsiri nyingi, mmoja wa vigogo wa CCM wanaotakiwa na chama hicho ‘’kujivua gamba’’ kutokana na kuhusishwa na tuhuma za ufisadi, Edward Lowassa, ametetewa na kiongozi wa Kanisa Katoliki kuwa ni mtu mwema na mwadilifu.
Lowassa, ambaye alijiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu Februari mwaka 2008 kutokana na kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, alipata utetezi huo Jumapili iliyopita, mjini Mwanza alikoalikwa na Kanisa Katoliki kupitia Parokia ya Nyakato, Jimbo Kuu la Mwanza, kuongoza harambee ya kuchangisha fedha za kupaua jengo jipya la kanisa katika parokia hiyo.
Lowassa alihudhuria hafla hiyo akiwa na watu wanaotajwa kuwa ni maswahiba wake kadhaa wa kisiasa wakiwamo viongozi kadhaa wa CCM Kanda ya Ziwa.
Kutumika kwa Kanisa Katoliki kumsafisha Lowassa ikiwa ni siku chache tu kabla ya kufanyika kikao cha NEC ya CCM kitakachojadili hatima ya vigogo wa CCM wanaotakiwa kujivua gamba na ambao hawajafanya hivyo, kunaelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini kuwa huenda kukawagawa waumini wa Kanisa hilo.
Hiyo ni kwa sababu huko nyuma Kanisa Katoliki, kupitia Baraza la Maaskofu nchini (TEC), limekuwa moja ya taasisi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ufisadi, na pia lilikuwa likionekana kutowaalika kwenye hafla zake kama wageni rasmi viongozi wanaoandamwa na kashfa za ufisadi.
Lakini si kitendo cha kualikwa tu kwa mbunge huyo wa Monduli kwenye harambee hiyo ya Kanisa Katoliki ya Mwanza kilichozua maneno mjini hapa, bali pia kauli ya Makamu wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza (Vicar General) Padri Richard Makungu, wakati wa kumkaribisha Lowassa, iliyoonekana kumsafisha zaidi baada ya kusema ni mtu “mwema, mweledi, mcha Mungu na mtu makini”.
Alisema Padri Richard Makungu: “Tuliangalia Watanzania wengi lakini tuliona wewe ndiye unafaa kufanikisha harambee hii kwa sababu wewe ni mtu mwema, mweledi na mcha Mungu…wewe ni mzoefu wa harambee; hivyo kupitia kwako tunaweza kupata hata shilingi milioni 200”.
Padri Makungu, ambaye aliendesha ibada ya misa kabla ya harambee hiyo kufanyika, alisema kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, ambaye pia ni Rais wa TEC, alikuwa jijini Dar es Salaam kikazi kabla ya kwenda safarini Benin ambako atakutana na kiongozi wa Kanisa hilo, Baba Mtakatifu Benedicto XVI.
Akizungumza na Raia Mwema mara baada ya harambee hiyo, Padri Makungu alisema kuwa hakuna tatizo lolote kumwalika Lowassa katika harambee hiyo, kwani wao kama Kanisa hawana ushahidi wowote kuthibitisha kuwa yeye ni mtuhumiwa wa ufisadi, hivyo hawawezi kumtenga.
“Kwanza waliomwalika ni kamati ya ujenzi ya kanisa hili, na mimi nimekuja kuendesha misa tu; hivyo kama unataka kujua kwanini wamemwalika yeye hilo kawaulize viongozi wa kamati.
“Lakini sisi kama uongozi wa Jimbo tulipewa taarifa; ndiyo maana nikaja kuendesha hii misa. Kwa hiyo, kama ni kujua tukio hili tulijua, sema tu Mhashamu Baba Askofu yuko Dar es Salaam kikazi na baadaye anakwenda Benin kwenye mkutano ambao utahudhuriwa na Baba Mtakatifu Benedict XVI; hivyo asingeweza kusubiri hii harambee,” alisema Padri Makungu.
Alipoulizwa juu ya kauli yake ya kusema Lowassa ni mtu mwema, mweledi, mcha Mungu na mtu makini wakati chama chake (CCM) kinamtaka kujivua gamba kwa tuhuma za ufisadi, makamu huyo wa Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza alisisitiza kuwa hakuna tatizo lolote na kauli yake hiyo.
“Mimi nimesema vile kwani naamini mtu yeyote ni mwema. Siwezi kumhukumu mtu kwamba ni mwovu. Hata nyumbani kwako ukiwa na mtoto mwovu au ana matatizo huwezi kumkemea na kumgombeza siku zote.
“Lazima utafute namna ya kumsaidia. Kwa hiyo, kwa mtu mzima ataangalia wema wake ndani ya nafsi yake maana hatuna ushahidi wa hayo (ufisadi) wanayosema,” alisema.
Lakini ni kutokana na mapokeo hayo tofauti miongoni mwa waumini wa Kanisa hilo na jamii kwa ujumla ndiyo yaliyofanya Padri Makungu kutoa tahadhari kwa vyombo vya habari, mwishoni mwa harambee hiyo, kwa kuwataka waandishi wasiandike habari chafu tu bali na mengine mema yanayofanywa na kanisa hilo.
“Waandishi wa habari msiandike habari chafu tu. Muandike na mengine mazuri ya kujenga. Harambee hii imefanikishwa na mkono wa Mungu na si kwa mkono wa mtu fulani. Andikeni taarifa za kujenga Taifa na si kubomoa,” alisema.
Akifanunua kauli yake hiyo katika mahojiano na Raia Mwema baada ya harambee hiyo kwisha, Padri Makungu alisema alichokilenga si tu tukio hilo la Lowassa kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo; bali katika mambo mbalimbali ya Kanisa na mengine yenye maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo, Parokia ya Nyakato, Pastory Masota, alisema kuwa mwaliko huo kwa Lowassa ulipata baraka zote za Kanisa; kwani walimwandikia Askofu Mkuu Ruwai’chi na kukubaliwa.
“Mwanzoni tulimwomba Waziri (John) Magufuli ikashindikana. Tukafanya juhudi za kumwalika Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikashindikana. Kwa hiyo, tulipompata Mheshimiwa Lowassa akakubali lakini akasema baada ya miezi sita ndiyo atakuwa na nafasi. Kwa hiyo, tumesubiri miezi sita kufanikisha harambee hii,” alisema.
Alipoulizwa kwa nini walimwalika Lowassa licha ya kuwa anatuhumiwa kwa ufisadi, alirejea kauli ya Makamu wa Askofu Mkuu kuwa hawataki kujiingiza katika masuala hayo kwani hajafikishwa mahakamani hivyo wao hawawezi kuingilia utaratibu wa chama chochote cha kisiasa.
“Hayo (kujivua gamba) yako ndani ya CCM, sisi hatuwezi kuyazungumzia. Sisi tulitaka mtu ambaye angetusaidia kufanikisha kukamilisha ujenzi wa kanisa letu maana mpaka hapo tulipofikia (boma) waamini wamejitolea kiasi kikubwa, ” alisema Masota ambaye mwaka jana aliwania kugombea ubunge wa jimbo la Ilemela kwa tiketi ya CCM lakini akashindwa katika kura za maoni za chama hicho na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Anthony Diallo.
Katika harambee hiyo, Lowassa aliambatana na wale aliowaita marafiki zake akiwamo Mjumbe wa NEC Mkoa wa Mara na mfanyabiashara maarufu kanda ya Ziwa Christopher Mwita Gachuma; aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Lawrence Kego Masha; mfanyabishara na mbunge wa Rorya Lameck Okambo Airo, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja; katibu wa uchumi na fedha wa Mkoa wa Shinyanga na mfanyabiashara, Gasper Ndaki; katibu wa uchumi na fedha na mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Mkoa wa Mara, William Marwa Mathayo; aliyekuwa mbunge wa Busega Dk. Raphael Chegeni; mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza, Maria Hewa ambaye pia ni muumini wa Parokia hiyo ya Nyakato na mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na wafanyabiashara kadhaa wengine kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Arusha, Kagera, Tabora na Shinyanga.
Mbali na Masha, ambaye anatajwa kuwa mtu wa karibu wa Lowassa, hatua ya Gachuma kuwa kama makamu wa Lowassa katika kuendesha harambee hiyo pia imezua hisia tofauti za mwelekeo wa kisiasa nchini kutokana na kuaminika kuwa katika kampeni za kuwania urais ndani ya CCM mwaka 2005 alikuwa upande wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye ambaye kama Lowassa, anatajwa kuwa mmoja wa watu watakaogombea urais mwaka 2015 ingawa mwenyewe hajatangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, hapakuwapo kiongozi yeyote wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa wakati kwa upande wa Serikali alikuwapo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Saidi Amanzi.
Aidha, kitendo cha Lowassa kuendelea kujikita zaidi katika tatizo la ajira za vijana ambalo analielezea kama bomu linalosubiri kulipuka kinaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni mojawapo ya mikakati ya kujijenga kupitia vijana nchini ambao hivi sasa wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa na kuwa tegemeo kubwa la vyama vya upinzani, hususan CHADEMA.
Kama ilivyokuwa wakati alipokutana na waandishi wa habari nyumbani kwake Monduli hivi karibuni, katika hotuba hiyo ya Jumapili alirejea moja kwa moja tatizo hilo huku akisema ameamua kutoa takwimu ili sasa wamwelewe na kwamba si nia yake kumlaumu mtu.
“Si nia yangu kumlaumu mtu yeyote. Nataka kusema kuwa jukumu la kuangalia ajira kwa vijana ni la kila Mtanzania. Nasema tusipoangalia amani na utulivu wa nchi hii itayeyuka kwa sababu ya tatizo hili la ajira.
Binadamu anaishi kwa matumaini kwa hiyo kama hana matumaini usitarajie afanye lolote. Nasema kama sauti ya Yohana Mbatizaji. Hii ni sauti ya mtu aliaye nyikani lakini ni onyo kwa Watanzania wote. Tuliangalie (suala la ajira kwa vijana) wote,” alisema.
Kauli hiyo ya tatizo la ajira kwa vijana imekuwa ikisemwa na baadhi ya wanaodaiwa kuwa wafuasi wake ndani ya UVCCM, na yeye amesema wasipuuzwe kwani tatizo hilo limeongezeka kutoka asilimia 12 mwaka 2006 hadi asilimia 15 na waathirika wengi ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24.
Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 200 zilikusanywa wakati malengo yalikuwa ni kukusanya shilingi milioni 120; kati ya hizo fedha taslimu ilikuwa shilingi milioni 110 na ahadi shilingi milioni 90.
Kauli kuhusu ajira kwa vijana kuwa ni bomu, imeibua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii, ikihusishwa moja kwa moja na ushawishi unaoweza kuibuka kwa ghasia nchi nzima kutokana na tatizo hilo kuwagusa vijana wengi nchini.

0 comments

Post a Comment