IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KUNDI la wafuasi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha, jana lilizingira uzio wa Makao Makuu ya Polisi mkoani hapa ambako mwenyekiti wa umoja huo, James Milya alikwenda kujisalimisha.Wakati Milya akihojiwa, wafuasi hao wa CCM walibaki nje wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu kiongozi wao huyo.
Wafuasi hao walifika hapo wakimsindikiza Milya kwa maandamano maalumu hali iliyowalazimisha polisi kuwazuia kuingia kwenye lango kuu. Walibaki huku kuendelea kuimba.
Milya aliwasili katika Ofisi Polisi Mkoa wa Arusha saa 6:30 mchana akiwa ndani ya gari aina ya Lexus. Mbali ya kusindikizwa na wafuasi wake hao, pia alikuwapo wakili wake, Moses Mahuna.
Baada ya kushuka kwenye gari hilo akiwa na wakili wake na baadhi ya viongozi wa UVCCM, aliekea moja kwa moja katika ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Akili Mpwapwa ambako alikaa huko kwa takriban dakika 15 kabla ya kutoka nje na kupokewa kwa shangwe na wapambe wake.
Baada ya Milya kutoka, maandamano makubwa ya kumsindikiza kiongozi huyo yaliyoongozwa kwa magari, pikipiki na baiskeli yalianza. Yalipita kwenye Barabara ya Makongoro kuelekea Makao Makuu ya UVCCM mkoani hapa.
Hata hivyo, kabla ya kufika katika ofisi hizo, wakiwa katika eneo la mzunguko wa Mnara wa Azimio la Arusha, msafara huo ulikutana na gari la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo lililokuwa likitoka katika ofisi hizo za UVCCM. Lilisimama ghafla na kisha mkuu huyo wa mkoa kufungua dirisha kushuhudia maandamano hayo.
Kitendo hicho cha Mkuu wa Mkoa kilikuwa kama kimewazindua waandamanaji hao ambao walilipuka kwa sauti za juu na mmoja wao akisema: “Haturudi nyuma msimamo wetu uko palepale hata viongozi wa Serikali mkituingilia.”
Baada ya kuwasili katika ofisi za UVCCM Mkoa, waandamanaji hao walipigwa butwaa baada ya kukuta ofisi hizo zimefungwa huku katibu wake, Abdallah Mpokwa akionekana kuondoka kimyakimya. Wapambe wa Milya walipiga kelele kutaka ofisi hizo zifunguliwe ili kiongozi wao aingie ndani bila ya mafanikio.
Mpokwa alipohojiwa kuhusu kufungwa kwa ofisi za jumuiya hiyo, alikataa kuzungumza lolote na kutaka aachwe.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi hizo, Milya alisema alijisalimisha polisi baada ya kupata taarifa za kusakwa tangu wiki iliyopita.
Alisema baada ya kufika kituoni hapo, alitakiwa afike tena leo asubuhi kwa kuwa hakuhojiwa kutokana na viongozi wa jeshi hilo kuwa katika shughuli za mwenge wa Uhuru.“Nilipofika pale, polisi wameniambia kuwa nirudi tena leo kwa kuwa kuna shughuli za mwenge mkoani Arusha,” alisema.
Hata hivyo, alisema hajaelewa chanzo cha kuitwa kwake polisi.Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Monduli, Julius Kalanga alilaani kitendo cha polisi kumsaka Milya na kudai kwamba CCM kinapoteza mwelekeo kutokana na mambo ya chama kufikishwa polisi badala ya kumalizikia ndani ya vikao.
“Chama kinapoteza mwelekeo, hakina msemaji. Mambo ya chama yanafikishwa polisi badala ya kwenye vikao vya chama hii ni ajabu,” alisema Kalanga.
Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Ally Bananga alipinga kitendo cha polisi kumsaka Milya na kusema kuwa huo ni ukandamizaji wa demokrasia ndani ya chama kwa kuwa mambo ya chama yanapaswa kumalizwa ndani ya chama.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - UVCCM waandamana Arusha
0 comments