Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - JK, George Bush wateta Ikulu Dar

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
RAIS Jakaya Kikwete jana alifanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Marekani George W. Bush Ikulu jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine, walijikita kwenye sekta ya afya. Bush na mkewe Laura wako nchini tangu jana katika ziara ya siku sita barani Afrika, zikiwamo Ethiopia na Zambia.


Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ilisema kuwa viongozi hao walizungumzia namna taasisi iitwayo George W. Bush Institute for Global Health inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na changamoto kubwa kwenye sekta ya afya, hasa ugonjwa wa saratani. Taarifa hiyo ilimnukuu, Bush alimweleza Rais Kikwete mipango ya taasisi yake hiyo katika kupambana na ugonjwa huo hasa katika huduma za kupima, kuzuia na chanjo.


Katika mkutano huo, Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kumweleza Bush jitihada za serikali ya Tanzania katika kupambana na magonjwa yanayoua watu wengi yakiwamo malaria, Ukimwi na saratani. Kikwete alimshukuru Bush kwa msaada wake wa fedha kusaidia mapambano ya magonjwa hayo wakati alipokuwa Rais wa Marekani.


Rais Kikwete pia alitumia nafasi hiyo kumweleza Bush kuhusu maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani nchini. Baadaye jioni, Rais Kikwete alikuwa na mazungumzo ya satelaiti na Rais wa Marekani Barack Obama ambapo alitumia fursa hiyo kumshukuru kwa misaada mbalimbali aliyoitoa kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi.


Kikwete ambaye katika mazungumzo hayo alikuwa na Bush, alisema misaada hiyo ya Marekani, imepunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5.7 hivi sasa. “Wakati tukishuhudia kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi, tunawashukuru watu wa Marekani kwa misaada yao” alisema rais Kikwete.


Aliendelea kueleza kuwa mbali na maambukizi, unyanyapaa kwa wagonjwa wa Ukimwi, umepungua jambo ambalo limehamasisha watu kujitokeza kwa ajili ya kupima afya zao kujua maambukizi ya ugonjwa huo na kujitangaza. Alisema takwimu zinaonyesha kwamba watu milioni 13 nchini wamepima na kupata ushauri nasaha. Alisema watu milioni 1.3 wanaishi na virusi vya Ukimwi na yatima wanaotokana na ugonjwa huo ni milioni mbili.


Aliiomba serikali ya Marekani kuendelea kuisaidia Tanzania ili iweze kupiga hatua kubwa zaidi katika mapambano dhidi ya Ukimwi. Katika mazungumzo hayo Bush alisifu juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwamo Ukimwi.

0 comments

Post a Comment