Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mchina ashikiliwa kwa kumpiga ofisa uhamiaji

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MFANYABIASHARA wa Kariakoo raia wa China, Yuxian Weng anadaiwa kumshambulia ngumi za usoni Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Ilala na kusababisha apoteze fahamu kwa saa sita.


Ofisa huyo, Koplo Musa Mkubwa anadaiwa kupigwa ngumi hizo upande wa kushoto wa uso
wake juzi baada ya kumtaka raia huyo wa China aoneshe hati yake ya kusafiria na kibali cha kufanya kazi nchini.


Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Agness Muganda alithibitisha
kupigwa kwa ofisa huyo na kusema kuwa alipoteza fahamu saa kumi jioni na kuzinduka akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili saa nne usiku.


Kwa mujibu wa Kamanda Muganda, baada ya kuzinduka Koplo Mkubwa alikuwa mtu asiyeelewa kitu na daktari aliyekuwepo zamu aliagiza amuone daktari wa kichwa.


Alisema jana asubuhi Koplo Mkubwa alikuwa na nafuu kidogo na baada ya kuonana na daktari
wa kichwa aliruhusiwa kwenda nyumbani lakini awe chini ya uangalizi wa daktari kwa kuhudhuria kliniki ya kichwa.


Gazeti hili lilimtafuta Koplo Mkubwa kwa simu yake ya mkononi na ikapokewa na mwanamke aliyekataa kujitambulisha lakini alidai kuwa amepumzika hivyo hawezi kuzungumza na simu.


Akisimulia masaibu hayo kwa Koplo Mkubwa, Kamanda Muganda alisema siku hiyo maofisa
Uhamiaji kutoka kituo hicho walikuwa katika doria ya kuwatafuta wahamiaji haramu aliodai
kuwa hufikia katika nyumba moja (jina limehifadhiwa) iliyopo Kariakoo.


Alidai baada ya kufika katika nyumba hiyo, walimkuta mama wa Weng na watoto wake ambao
walimtaarifu Weng kuwa kuna watu asiowafahamu wamefika nyumbani hapo.


Kamanda Muganda alisema baada ya muda mfupi, mke wa Weng alifika nyumbani hapo na
maofisa hao walijitambulisha na kutoa vitambulisho vyao na mwanamke huyo aliwapatia hati
zake walizohitaji na baada ya kuridhika waliondoka.


Hata hivyo Kamanda Muganda alisema maofisa hao walipokuwa wakishuka ngazi kutoka
ghorofani, walimsikia Weng akimfokea mlinzi wake akihoji kwa nini ameruhusu majambazi
kuingia nyumbani kwake na mlinzi huyo akajibu kuwa ni maofisa uhamiaji.


Alidai wakati wakishuka ngazi na yeye akipandisha, walikutana katikati na maofisa hao
wakajitambulisha na kumuomba hati yake ya kuishi na kufanya kazi nchini lakini Weng
alikataa na kumpiga Koplo Mkubwa usoni.


Kamanda Muganda alisema baada ya Weng kumpiga Koplo Mkubwa, wenzake walimfunga
pingu raia huyo wa China na kumfikisha ofisini kwao kuchukua maelezo.


“Wakati wakitoka kule kwa mchina Kariakoo ofisa aliyepigwa alikuwa akilalamika maumivu ya
kichwa kuwa anasikia kizunguzungu na wakati yanachukuliwa maelezo pale ofisini alidondoka
na kupoteza fahamu,” alisema Kamanda Muganda.


Alisema baada ya kupoteza fahamu walimpeleka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja lakini alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa na kugundulika kuathirika katika kichwa na hivyo kutakiwa kuhudhuria kliniki ya kichwa.


Habari kutoka ndani ya Uhamiaji zimeonesha kuwa raia huyo wa China alikutwa na hati halali
namba RPA 031266 iliyotolewa jijini Dar es Salaam Julai 28 mwaka 2010.


Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Muganda, raia huyo wa China alipelekwa Kituo cha Polisi cha Ilala na anashikiliwa wakati mgonjwa akiangaliwa hali yake.

0 comments

Post a Comment