Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mshahara wa kima cha chini sasa juu, JK ATANGAZA NYONGEZA BUNGENI

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Rais Jakaya Kikwete, akihutubia Bunge mjini Dodoma jana wakati akihitimisha shughuli za Bunge la Tisa, ili kupisha nchakato wa uchaguzi mkuu wa Mwaka huu.kushoto ni Spika wa Bunge Samwel Sitta
Waandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete ametaja kima cha chini cha mishahara ya watumishi wa umma kuwa ni Sh 135,000 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 107 tangu aingie madarakani mwaka 2005 alipokuta mshahara wa Sh65,000 kwa mwezi.Hili ni sawa na ongezeko la Sh31,000 kwenye mishahara ya kima cha chini ya Sh104,000 iliyokuwa ikilipwa na serikali kwa watuhimishi wa umma mwaka wa fedha ulioishia June 2010.

Rais kikwete aligusia kima hicho cha mishahara katika hotuba yake aliyoitoa jana bungeni wakati akilivunja rasmi bunge la tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuanza kwa Uchaguzi Mkuu.

Alisema ongezeko hilo la mishahara ni mafanikiwa makubwa kwa serikali yake ikilinganishwa na serikali zilizomtangulia.

"Katika kipindi hiki tumepandisha kima cha chini cha mishahara ya watumishi wa umma kutoka Sh 65,000 mwaka 2005 mpaka Sh 135,000 mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 107," alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta) Nicholas Mgaya alisema kuwa nyongeza hiyo aliyotangaza Rais Kikwete sio makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na shirikisho hilo.

"Katika mazungumzo yetu sisi Tucta tulitaka iwe Sh160,000, lakini serikali ikaja na Sh135,000 ambayo hatukuafikiana nayo hivyo serikali imefanya maamuzi ya kukurupuka," alisema Mgaya ambaye hivi karibuni alikuwa katika malumbano makubwa na Rais Kikwete kwamba alikuwa akiwapotosha wafanyakazi.

Hata hivyo, mbali na Rais Kikwete kutangaza kima hicho cha mshahara alisema serikalio yake bado inaendelea na mazungumzo kuhusu nyongeza zaidi.

Rais Kikwete alisema serikali pia imejitahidi kuboresha na kupandisha watumishi madaraja ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imewapandisha watumishi 140,797.

Alisema hatua hiyo ya kuwapandisha madaraja watumishi hao ilienda sambamba na kuwalipa fidia na stahili zao zilizogharimu Sh 108 bilioni.

"Pia tulilipa malimbikizo ya Sh 45.1 bilioni kama malimbikizo na madeni yote halali ya walimu; walimu wa shule za msingi Sh 32.2 bilioni na sekondari Sh 12.9 bilioni," alisema.

Pamoja na jitihada za serikali za kuwapatia wananchi maendeleo yao, Rais Kikwete alisema serikali yake ilikabiliana na changamoto nyingi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Moja ya mambo yaliyokwamisha mikakati ya serikali ya awamu ya nne aliitaja kuwa ni ongezeko la bei za mafuta mwaka 2007 ambapo hadi kufikia Juni, 2008 gharama zilifikia kiwango cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa duniani.

"Na katika nusu ya pili ya mwaka 2008, dunia ikakumbwa na tatizo jingine kubwa la machafuko katika masoko ya fedha na mitaji yaliyosababisha kudorora kwa uchumi wa dunia," alifafanua Rais Kikwete.

Hali hiyo aliilezea kwamba ilkisababisha  uchumi kushuka, mfumuko wa bei kupanda, mapato ya serikali kushuka chini ya malengo.

Kutokana na hali hiyo, Rais akasema serikali ililazimika kutengeneza mpango wa dharura wa kunusuru uchumi kwa kitumia Sh 1.7 trilioni.

"Hatua hiyo ndiyo iliyosaidia kupunguza makali ya athari za kudorora kwa uchumi hapa nchini," alisema Rais Kikwete.

Mbali na changamoto hiyo, Kikwete alisema kuwa Tanzania imeendelea kuwa nchi tulivu, yenye amani na usalama na watu wana umoja licha ya tofauti zao za dini, makabila, rangi na ufuasi wa vyama vya siasa.

"Nchi  imeendelea kuwa kielelezo kizuri cha utulivu wa kisiasa na ukomavu wa demokrasia barani Afrika," alisema.

Vita dhidi ya ufisadi
Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali imepeleka mahakamani kesi za rushwa 780.

Idadi hiyo aliilezea kuwa ni kubwa kuliko kesi zote za rushwa zilizopata kupelekwa mahakamani katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Idadi ya majaji 
Kuhusu mahakama, Rais Kikwete alisema kuwa serikali imeongeza idadi ya majaji, mahakimu na mawakili wa serikali.
"Katika kipindi hicho tumeteua majaji wapya 12 wa mahakama ya rufani kati yao 4 wakiwa wanawake na majaji 51 wa Mahakama Kuu, wanawake wakiwa 24.

"Tumeajiri mahakimu wakazi 256 wanawake wakiwa 117 na mahakimu  wa mahakama za mwanzo 394, kati yao 134 ni wanawake.  Majaji na Mahakimu wanawake wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu," alisema Rais Kikwete katika hotuba hiyo ambayo wabunge walimshangilia mara kwa mara.

Hali ya uchumi
Kuhusu hali ya uchumi, Rais Kikwete alisema Pato la Taifa liliongezeka kutoka Sh 15.9 trilioni mwaka 2005 hadi Sh 28.2 trilioni mwaka 2009.

Kwa ajili hiyo, akasema pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka Sh 441,030 mwaka 2005 hadi Sh 693,185 mwaka 2009.

"Kasi ya wastani ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa asilimia 6.9 katika kipindi hicho," alisema na kuongeza:

"Mapato yetu ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje yaliongezeka kutoka dola milioni 2,994.9 mwaka 2005 hadi dola 4,693.6 milioni mwaka 2009."

Alisema akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kutoka dola 2.21 bilioni mwaka 2005 hadi dola 3.55 bilioni mwaka 2009 ambazo zinawezesha taifa kuagiza bidhaa kutoka nje kwa karibu miezi sita," alisema Rais Kikwete.

Kuhusu mapato na matumizi ya serikali alisema kuwa mapato ya ndani yamepanda zaidi ya mara mbili kutoka wastani wa Sh 177.1 bilioni kwa mwezi 2005/06 hadi Sh 390.7 bilioni kwa mwezi 2009/2010.

"Hii imetupa uwezo wa kuongeza bajeti ya serikali kutoka Sh 4.13 trilioni mwaka 2005/06 hadi kufikia Sh 11.6 trilioni mwaka 2010/11.

"Tumeendelea kupunguza utegemezi wa wafadhili katika bajeti ya serikali kutoka asilimia 44 mwaka 2005/2006 hadi asilimia 28 mwaka huu, 2010/2011," alisema.

Thamani ya madini

Rais Kikwete alisema thamani ya madini yaliyosafirishwa nje ya nchi mwaka 2005 ilikuwa dola 720.49 milioni na mwaka 2009 ilikuwa dola 1,219.06 milioni.

Ajira katika uchimbaji mkubwa, alisema iliongezeka kutoka wafanyakazi 7,000 mwaka 2005 hadi 13,000 mwaka 2008.

Kutangaza utalii wa Tanzania

Rais Kikwete alisema katika sekta ya utalii serikali imeendeleza sekta hiyo muhimu na hasa kutangaza vivutio vya utalii vya nchi katika masoko makubwa duniani.

"Tumetunga sheria ya utalii ya mwaka 2008 na sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 kwa lengo la kuboresha huduma za utalii na kuziba mianya ya uvujaji mapato yatokanayo na utalii. Tumeimarisha pia miundombinu ya utalii kwa kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zaidi za kitalii," alisema Rais Kikwete.

Alisema kutokana na jitihada hizo, watalii wameongezeka na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola 823.5 milioni mwaka 2005 hadi dola 1,198.76 milioni mwaka 2008.

Alisema mwaka 2009 mapato yalishuka kidogo na kuwa dola 1,162.8 milioni  kwa sababu ya kudorora kwa uchumi wa dunia na kusababisha watalii kupungua na kukaa nchini kwa siku chache.

Upimaji wa ardhi
Kwa upande wa ardhi na makazi, Rais Kikwete alisema serikali ilipiga hatua kwani kati ya Januari 2006 na Mei 2010 ilifanikiwa kupima na kutoa hati kwa jumla ya vijiji 6,129.

Kikwete alisema idadi ya vijiji vilivyopimwa na kusajiliwa ni 10,682 ambayo ni sawa na asilimia 97 ya vijiji 11,000 nchini.

"Tumeendelea na mpango wa matumizi ya ardhi, wa kupima mashamba ya wanavijiji na kutoa Hatimiliki za Kimila," alisema.

Vilevile, alisema  kati ya Januari 2006 na Mei 2010, alisema serikali ilipima viwanja 37,458 katika maeneo ya miji mbalimbali ili kuharakisha utoaji wa hati za kumiliki ardhi.

Katika kutekeleza mkakati huo, alisema serikali ilianzisha kanda sita za ardhi nchini zenye mamlaka ya kutoa hati hizo.
Vilevile, chini ya programu ya Mpango wa Kurasimisha Raslimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) Rais alisema jumla ya nyumba 290,000 katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Tanga na Moshi zilitambuliwa na wamiliki kupewa leseni za makazi ambazo wanaweza kuzitumia kama dhamana kuombea mikopo katika taasisi za fedha.

Upande wa sayansi na teknolojia


Kuhusu mawasiliano, sayansi na teknolojia katika miaka mitano, Rais alisema serikali imewezesha ujenzi wa mkongo wa taifa ulioanza Februari, 2009.

Alisema mkakati huo unaendelea vizuri na  ifikapo Juni, mwakani, makao makuu ya mikoa na ya wilaya zote zitafikiwa.


Vilevile, alisema serikali imeanzisha  mpango wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kuendeleza elimu nchini.
Mpango huo unaofahamika kwa jina la “Tanzania Baada ya Kesho” chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alisema una lengo la kuwezesha walimu na wanafunzi katika shule za sekondari kupata na kutumia kompyuta kwa maendeleo ya elimu.

Kwa upande wa elimu


Kuhusu elimu alisema serikali imepanua elimu ya awali na msingiambapo wanafunzi wa awali wameongezeka kutoka 638,591 mwaka 2005 hadi 825,465 mwaka 2010.

 Shule za msingi, zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 15,816 mwaka 2010 na wanafunzi wameongezeka kutoka 7,541,208  hadi 8,419,305 katika kipindi hicho.

Alisema upanuzi huu umewezesha asilimia 97 ya watoto wanaostahili kupata elimu ya msingi kuandikishwa.

"Tumeajiri walimu wapya 6,028 wa shule za awali na 49,694 wa shule za msingi na kwa kushirikiana na wananchi, katika kipindi cha miaka mitano hii, tumeweza kujenga shule za sekondari 2,171 ikilinganishwa na shule 1,202 zilizojengwa toka uhuru mpaka mwaka 2005," alisema Rais Kikwete.

Alisema lengo la sekondari moja kwa karibu kila kata limetekelezwa na baadhi ya kata zina shule zaidi ya moja.

Kwa upande wa shule za sekondari za binafsi, alisema  zimeongezeka kutoka 531 hadi 856 katika kipindi hicho.

Ongezeko hili alilielezea kuwa liliwezesha idadi ya wanafunzi wanaosoma sekondari kuongezeka toka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,638,669 mwaka 2010.

Alisema upanuzi wa mafunzo ya walimu katika vyuo vikuu umeongeza walimu wanaohitimu kutoka 500 mwaka 2005 hadi 5,339 mwaka 2009.

Wabunge wapokea hotuba kwa hisia tofauti

Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wameipokea hotuba ya Rais Kikwete kwa mitazamo tofauti huku baadhi wakiipongeza na wengine kuiponda.

Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa alisema hotuba ya Kikwete jana ilikuwa nzuri kama alivyotegemea kwa kuwa ameeleza na kugusia mambo yote yaliyofanywa na Bunge na serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Lakini Mbunge viti Maalum, Chadema Halima Mdee aliponda hotuba hiyo na kusema haina jipya zaidi.

"Hakueleza mambo mapya, hotuba yake yote ilikuwa copy and paste ya hotuba mbalimbali za mawaziri wake ambazo tulishazisikia na kuzizoea," alisema

Mdee alionyesha wasiwasi juu ya hotuba hiyo akisema aliamini rais angejikita zaidi kuzungumzia uchaguzi ujao na namna utakavyokua wa haki na huru kwa vyama vyote vya siasa, lakini hakufanya hivyo.

Naye mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema hotuba hiyo ni nzuri kwani alieleza utekelezaji wa mambo yote aliyoliahidi Bunge na wananchi wakati anaingia Ikulu mwaka 2005.

"Mimi naona hotuba yake ni nzuri. Imeeleza utekelezaji wa mambo mengi aliyoahidi ingawa naona bado kuna changamoto nyingi kwenye suala la uchumi," alisema Zitto.

"Familia nyingi bado ni maskini na rais hajaeleza mikakati inayoingia akilini ya kutatua tatizo hilo."

Imeandikwa na Boniface Meena, Leon Bahati, Dar na Habel Chidawali, Dodoma
Tags:

1 comments

  1. Hi,iºam Raul from Madrid,Spain,you did a nice job with this website,i like your articles and you photos,i will visit you again soon to see the new post.bye bye,adios
    Nehoiu online Marketing Asesinos seriales Directorio web SEO

Post a Comment