Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sitta: Kuilipa Dowans au la lazima ipitishwe na baraza la Mawaziri

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


Sitta alisema anashangazwa na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutangaza msimamo wa serikali kuilipa Dowans bila suala hilo kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri.
"Nimekuwa wa kwanza kupinga serikali kulipa fedha hizi na anaendelea kusisitiza hatuna sababu ya kuzilipa, bado tuna nafasi kisheria ya kupinga, lakini kibaya zaidi nashangaa kusikia Waziri wa Nishati na Madini, ameutangazia umma kwamba serikali inajiandaa kuilipa Dowans. Uamuzi huo umepitia Baraza gani la Mawaziri," alihoji Sitta.
Alisema fedha hizo ni nyingi kuilipa Dowans ambayo alisema ina mkono wa mafisadi watatu, wanaotaka kuzitumia fedha hizo kwa maslahi yao kisiasa.
Wiki iliyopita, Ngeleja alikaririwa akisema, Serikali imekubali kuilipa Dowans dola za Marekani za Kimarekani milioni 65, sawa na sh bilioni 94.
Alisema sh 185 bilioni zilizokuwa zikitajwa kwenye vyombo vya habari ndizo ambazo kampuni ya Dowans iliiomba ICC ilipwe fidia kwa TANESCO kwa kukatiza mkataba walioingia wa kufua umeme, lakini mahakama iliafiki ilipe dola 65 milioni za Marekani.
Alisema fedha hizo zitalipwa baada ya pande husika kusajili uamuzi huo katika Mahakama Kuu.
"Serikali tumekwishaamua kuwa tutailipa Dowans dola za Marekani 65 milioni, kama ilivyoamuliwa na ICC ambazo ni sawa na sh 94 bilioni, kuchelewa kuwalipa kutatufanya tulipe riba ya asilimia 7.5," alinukuliwa akisema.
Katika mkutano huo, Ngeleja pia aliwataja wamiliki wa Dowans Tanzania Ltd na hisa wanazomiliki katika mabano kuwa ni Dowans Holding S.A ya Costa Rica (81) na Portek.
Huku akirejea barua ya Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brella), aliwataja wakurugenzi na nchi wanazotoka kuwa ni Andrew James Tice (Canada) na Gopalakrishnan Balachandaran (India).
Wengine ni Hon Sung Woo (Singapore), Guy Picard (Canada), Sulaiman Al Adawi (Oman) na Stanley Munai (Kenya).
Wakati Ngeleja akitamka kwamba serikali inajiandaa na kulipa fidia hiyo haraka, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, ameibua utata mwingine baada ya kuutangazia umma kwamba wizara yake haina fedha na haina mpango wa kutenga fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya kuilipa Dowans.
Mkullo alisema TANESCO kupitia wizara yake ya Nishati na Madini, inatakiwa ijipange kusaka fedha za kuilipa Dowans na kamwe fedha hizo hazitatoka Hazina.
Kiini cha sakata hilo kilianza mwaka 2006, wakati TANESCO ilipoingia mkataba wa mauziano ya umeme wa TANESCO na kampuni ya Richmond Development LLC.
Miezi sita baadaye mkataba huo ulihamishiwa kwa kampuni ya Dowans Holdings ya nchini Costa Rica na baadaye kwa Dowans Tanzania Ltd.
Wakati wa utekelezaji wa mkataba huo, ilizuka hoja kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo wabunge kwamba mkataba baina ya TANESCO na Richmond haukuwa halali kisheria hivyo usingeweza kurithiwa na Dowans.
Suala hilo lilizua mjadala mkubwa hali ambayo TANESCO kwa kuwatumia mawakili wa kampuni ya Rex Attorneys ya jijini Dar es Salaam walivunja mkataba huo.
Baada ya kuvunjwa kwa mkataba huo, ndipo kampuni hiyo ikalipeleka suala hilo ICC kama walivyokubaliana na TANESCO kwenye mkataba.
Uamuzi huo wa ICC ulizua mjadala katika siku za hivi karibuni baada ya viongozi wa serikali kutofautiana kuhusu kuilipa kampuni hiyo au kutoilipa.
Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), kinatarajia kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa serikali kukubali kuilipa Dowans.
LHCR, pia inapinga kusajiliwa kwa tuzo hiyo Mahakama Kuu kwa sababu mikataba ya awali ilipatikana kwa rushwa na kukiuka maslahi ya umma.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Fransis Kiwanga, alisema walitarajia kufungua kesi hiyo jana na itasimamiwa na Kampuni ya Uwakili ya The South Law Chembers Advocates.
Sambamba na hilo pia kituo hicho kimeitaka TANESCO kutokubali kuilipa Dowans hata senti moja kwa kuwa haikuridhia kurithishwa na kuhamishwa kwa mkataba wa Richmond kwenda Dowans.
Aidha ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha mara moja kuwabebesha Watanzania mzigo wa kulipia gharama zinazotokana na uzembe, ubadhirifu na ufisadi wake yenyewe huku ikiingilia uhuru na utendaji wa Tenesco kwa kuitaka iilipe Dowans.
"Kwa taifa maskini kama letu lenye matatizo mengi kama ukosefu wa umeme, mfumko wa bei na mengineyo, kutumia hela nyingi hivyo kulipa kampuni ambayo iligundulika kwa uchunguzi sahihi kuwa ni hewa, inatia shaka kwenye umakini wa serikali," alisema.
Mkurugenzi huyo alisema katika suala la Dowans kuna mambo ya kujiuliza ikiwemo kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilithibitisha kama Richmond ni kampuni hewa, inawezekanaje kuwa na mkataba wa kurithisha mali zake kwa Dowans kwani uhalali wa kisheria wa milki ya Dowans kwa mali ya Richmond, haupo na kuhoji kwa nini serikali haikutaifisha mali za Ricmond tangu awali.
Maswali mengini ni ikiwa Dowans haikurithi kwa uhalali mali ya Richmond, inawezaje Dowans kuwa na madai halali dhidi ya serikali
kuhusiana na mali iliyopatikana kwa uhalifu.

Halikadhalika serikali kuharakisha kuilipa Dowans kuhusiana na mali iliyopatikana kwa uhalifu, je nini hasa maslahi ya Wizara ya Nishati na Madini na kuhoji wizara hiyo inamuwakilisha nani katika suala la Dowans.
Hata hivyo wanaharakati hao walionyesha wasiwasi wao kwa serikali inaposema kuwa inalazimika kuilipa Dowans huku wakihoji kama imefuata taratibu za kisheria na kama shauri hili lilipowasilishwa katika mahakama ya ICC, wananchi walijulishwa kuhusu shauri hilo.
Kwa mujibu wa Kiwanga sababu za kuliendesha shauri hilo kwa siri na kutohudhuria mahakamani kwa mawakili wa serikali, zinatia dosari mwenendo mzima wa suala hili ukizingatia kuwa limegubikwa na ufisadi tangu awali.
Alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kupinga hukumu hiyo ya kimataifa na nyingine kama hizo pamoja na maamuzi yoyote ya serikali yasiyokuwa na maslahi kwao zisitekelezwe.
Naye Mkurugenzi wa Tamwa, Annelia Nkya, alivitaka vyombo vya habari kuendelea kupigia kelele sakata hili hadi kuona fedha hizo hazilipwi kwa Dowans.

Sent from my iPhone
Tags:

0 comments

Post a Comment