Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mahakama yaamuru Mbowe akamatwe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imetoa amri ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe popote alipo na kufikishwa mahakamani hapo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutotii amri ya kufika mahakamani hapo.
Mahakama hiyo pia imemtaka mdhamini wa Mbowe aliyetajwa kwa jina la Julius Isaya Magwe, kufika mahakamani hapo mara moja ili kuieleza mahakama hiyo sababu za kutotii amri ya mahakama pale anapohitajika.


Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Charles Magesa alisema jana kuwa kimsingi Mahakama inakubaliana na hoja ya wakili upande wa Serikali kuitaka mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa Mbowe kwa sababu ya kutotii amri ya kufika mahakamani au kumtuma mdhamini wake.


Alisema sababu iliyotolewa mahakamani hapo kwamba mshtakiwa huyo ni mbunge na yupo kwenye vikao vya Kamati za Bunge haina uzito kwa kuwa hiyo ni moja ya shughuli zake kama ilivyo shughuli nyingine kwa watumishi wa serikali.


“Hivyo basi kama ni shughuli zake za kawaida, haimzuii kutii amri ya mahakama pale anapoitwa bila kujali anaitiwa nini,” alisema Magesa.


Hakimu Magesa alisema kuwa anachokumbuka ni kwamba Mahakama hiyo kweli ilipokewa maelezo ya kuwa washtakiwa hawatahudhuria mahakamani hapo Mei 27 mwaka huu kwa sababu ya kuwa katika vikao vya Kamati za Bunge na kuagiza waje wadhamini wao siku kesi inapotajwa. Ndiyo sababu Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alimpeleka mdhamini wake mahakamani hapo.


Lakini, kabla ya kuhitimisha agizo hilo, hakimu huyo, awali alitoa amri ya kutaka kukamatwa kwa Mbunge wa Moshi Mjini, Philimon Ndesamburo, ambaye naye hakutii amri ya mahakama kwa kutofika Mei 27, 30 na 31 na hata jana.


Hata hivyo, baada ya kutoa amri ya kukamatwa kwa Ndesamburo ambaye naye ni mshtakiwa, ghafla alijitokeza mdhamini wake, Rubeni Ngowi na kuiambia mahakama hiyo kuwa alikuwapo Mei 30, ila hakuweza kusogea mbele kwa sababu ya woga wa mahakama na kwa kuwa hakuitwa.


Baada ya maelezo hayo, Hakimu Magesa alimhoji mdhamini huyo akitaka kujua alikuwa wapi Mei 27 mwaka huu kesi hiyo ilipotajwa. Ngowi alijitetea kuwa alikwenda jijini Dar es Salaam kwa familia yake ambayo ilikuwa ina matatizo, lakini Mei 30 alifika mahakamani hapo na kuomba kuondoa amri hiyo ya kukamatwa kwa mshtakiwa wake.


“Basi kwa sababu nakumbuka ulikuwapo Mei 30 na nilikuona hapa mahakamani ukimnong’oneza wakili Kimomogoro, basi naondoa amri hii. Ila naomba utii amri ya mahakama pale mshtakiwa anapokosa uje kutoa sababu za kukosa kwake,” alisema Magesa.


Hakimu Magesa pia alitoa onyo kwa washtakiwa wengine wakiongozwa na Dk Willibrod Slaa wasiache kufika mahakamani, kila siku kesi yao inapotajwa na pale wanapokuwa na sababu ya kutofika, wahakikishe wadhamini wao wanakuwapo kutoa sababu za kukosekana kwao.


Akitoa uamuzi wa hatima ya dhamana za washtakiwa wa kesi inayowakabili viongozi wa Chadema, Godbless Lema, Joseph Selasini na wafuasi wao, Hakimu Mkazi Magesa, alisema Mahakama hiyo imeondoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kama ilivyoamriwa awali na kutupilia mbali ombi la wakili wa serikali la kutaka wafutiwe dhamana.


Alisema kuwa kutokana na kupitia kwa makini maelezo ya utetezi wa pande zote mbili kwa Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki na wakili upande wa utetezi, Medhod Kimomogoro, Mahakama hiyo imeamua kuwapatia dhamana ya kudumu washtakiwa ambao ni Dk Slaa na wenzake, kwa kutii amri ya Mahakama.


“Mahakama hii imeamua kufuta amri ya dhamana ya muda na kuacha dhamana ya awali kwa sababu mara mahakama hii ilipotoa amri ya kuwakamata Mei 27 mwaka huu, washtakiwa hao walifika mahakamani hapa kujisalimisha wenyewe na wengine, akiwamo Mbunge Joseph Selasini, alituma mdhamini wake, hivyo nawaachia dhamana zao,” alisema Magesa.


Kesi hiyo ilifunguliwa na Serikali, Januari 5 mwaka huu ambapo washtakiwa 19 walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka la kufanya kusanyiko pasipo na kibali na kutoa maneno ya uchochezi. Washtakiwa walikana makosa yao na kwa sasa wako nje kwa dhamana hadi Juni 24 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.


Kauli ya Mbowe
Akizungumza na Mwananchi jana jioni, Mbowe alisema anatarajia kutoa tamko kuhusu suala hilo leo saa tano asubuhi jijini Dar es Salaam, lakini alikataa kutaja ni wapi mkutano wake na waandishi wa habari utafanyika.


“Nitatoa tamko kesho, lakini nasikitishwa na tafsiri hii ya Mahakama kwamba mimi nimekaidi amri ya kufika katika vikao vya mahakama. Nasema hivyo kwa sababu mara ya mwisho tulipokuwa mahakamani, tulipewa ruhusa ya kuhudhuria vikao vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Sasa sijui tafsiri yake ni nini, lakini niseme tu kwamba haya yote kuhusu sakata la Arusha na amri za polisi kuwakamata wabunge wa opposition (upinzani) nitalizungumza kesho (leo) kwa vyombo vya habari”.


Kwa mujibu wa Mbowe, waliomba ruhusa ili kuwawezesha kushiriki vikao vya Kamati za Bunge kutokana na umuhimu wa masuala ya bajeti kwa umma ambayo pia yanawagusa mahakimu na Idara ya Mahakama kwa jumla.


“…hebu kama mnakumbuka, katika Bunge lililopita tulijadili ule muswada wa sheria unaogusa idara ya mahakama sisi wabunge wa upinzani tulitumia nguvu kubwa kuwatetea mahakimu katika mambo mengi. Sasa katika suala hili la bajeti si vizuri tukikosekana kwenye vikao na ndiyo maana tuliomba ruhusa siku ile na tukaruhusiwa, ”alisema Mbowe.

0 comments

Post a Comment