IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ATAKA MASLHAI YA DINI YAEPUKWE KATIBA MPYA, WAISLAMU WALILIA AMANI AFRIKA
Waadishi Wetu
Rais Jakaya Kikwete amewatetea wakristo nchini kwamba hawahusuiki na kuchelewa kwa mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi, huku akionya kuwa fikra za aina hiyo si za kweli kwani zinaweza kuchochea mgawanyiko kwa misingi ya dini, hivyo kuhatarisha amani nchini.Badala yake Rais Kikwete amesema mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo umecheleweshwa na taratibu ndani ya Serikali na kwamba taratibu hizo zitakapokamilika itaanzishwa na kuendeshwa na Waislamu wenyewe.
Akihutubia Baraza la Iddi ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Iddi El Fitri mjini Dodoma jana, Rais Kikwete alisema Serikali katika kuruhusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi itazingatia ushauri uliotolewa na Tume ya Kurekesbisha Sheria.
"Napenda kuwatoa hofu pia kwamba hakuna mkono wa mtu wapo mnadhania hivyo. Maana, tunajuana. Si ajabu kuna hisia kuwa huenda Kanisa limeingilia kati kuzuia au kuchelewesha,"alisema KIkwete na kuongeza:
“Nilipokutana na Jukwaa la Maaskofu Julai 22, mwaka huu walisema ngoja ninukuu……Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini na jambo zuri linalowahusu Waislamu. Kwa kuwa ni jambo la kidini waachiwe Waislamu wenyewe walifanye ndani ya Uislamu, pasipo kutumia hazina ya Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi wote nchini……”.
"Na sisi katika kufuatilia utekelezaji wa jambo hili tulikabidhi Tume ya Kurekebisha Sheria kuishauri Serikali. Ushauri wa Tume hiyo ulikuwa kwamba Serikali haiwezi kuunda Mahakama ya kushughulikia masuala ya kidini ya dini fulani. Jambo hilo liachiwe Waislamu wenyewe kufanya,"alisema Rais Kikwete katika hafla iliyofanyika kwenye Msikiti Mkuu wa Gaddafi mjini Dodoma.
Alisema kimsingi Serikali imekubali ushauri huo na kwamba mchakato ulianza kwa kuunda Kamati ya pamoja iliyojumuisha Serikali na BAKWATA na kwamba nia ya Serikali ni kujihakikishia kuwa hicho kitakachoundwa hakiendi nje ya masuala ya kidini yaani ndoa, takala, mirathi na wakfu kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.
"Katu si Mahakama ya kushughulikia masuala ya jinai au madai.Haitajihusisha na masuala ya wizi na kutoa adhabu kama vile za kukatwa mikono. Haitahusika na kesi za fumanizi na hivyo kutoa hukumu ya kuuawa mkosaji kwa kupigwa mawe. La hasha !! Narudia kuwa mamlaka yake yatahusu ndoa, takala, mirathi na wakfu,"alisisitiza Kikwete.
Aonya udini
Pia Rais Kikwete amesema viongozi wa dini nchini watumie nyadhifa zao katika dini kuhubiri amani ili kuepusha waumini wao kujiingiza katika masuala ya sio kubalika katika jamii kama vile chokochoko za kidini.
Rais Kikwete alisema viongozi wadini wanatakiwa kuacha kuhubiri udini na siasa pindi wanapopata kushiriki katika mikutano mbalimbali hapa nchini.
Alisema kufanya hivyo wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani hivyo akasema watumie ipasavya nafasi yao ya kuheshimika katika jamii, kuimarisha amani.“Viongozi wa dini wananafasi kubwa katika taifa na kwamba wao wanaweza kusababisha kuibuka kwa tofauti katika jamii kama hawata tumia nafasi zao vizuri,” alisema Kikwete.
Aliongeza kwamba viongozi wa dini kama watatambua umuhimu wa kuzungumzia umoja na amani iliopo nchini basi watakuwa wameweza kulisaidia taifa kuendelea kuwa na mshikamano na umoja kwa wananchi wake.
“Kama viongozi wa dini watazungumzia umoja na amani pindi wanapokutana basi taifa litaendelea kuwa na watu wenye umoja na mshikamano. Na wananchi wanaweza kupiga hatua za kimaendeleo,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alifafanua kwamba hairuhusiwi kwa kiongozi yoyote wadini kubeza dini ya mtu mwingine na kwamba kwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria.“Hairuhusiwi kiongozi wa dini kubeza dini ya mtu mwingine kwa sababu kila mtu ana haki ya kuamini dini ambayo anaitaka yeye mwenyewe,” alisema.
Mufti Mkuu
Naye, Shehe Mkuu wa Tanzania Mufti Issa Shabani bin Simba alisema, wanaishukuru serikali kwa kutilia makazo juu ya viongozi wa dini wanao jihusisha na uzaji wa madawa ya kulevya.Alisema, Viongozi wa dini wanao jihusisha na uzaji wa madawa ya kulevya wanatakiwa kuchukuliwa hatua pindi wanapobainika kufanya hivyo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuonyesha mwanga wa kuanza kupambana na viongozi wa dini wanaojihusisha na uzaji wa dawa za kulevya na kwamba hii itasaidia kuondoa matatizo ya taifa kuwa na vijana wasiokuwa na uelewa wa maisha,” alisema Shehe Mkuu.
Mapema Rais Kikwete akiwa katika msikiti waKichangani Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam, aliwatakia heri ya sikukuu ya Eid el Fitri Watanzania wote.
Wahimiza amani
Katika swala za sikukuu ya Eid Eid el Fitri zilizofanyika katika misikiti mbalimbali nchini, viongozi wengi wa dini ya Kiislamu walihimiza Watanzania kuishi kwa amani, upendo na kuheshimiana.
Viongozi hao walionya kuwa ili kuwepo na amani ya kweli ni lazima watu kuepuka dhuluma, rushwa na vitendo vyote ambavyo vinamchukiza Mungu.
Isitoshe, viongozi hao waliwataka Waafrika kuwa macho na mbinu za mataifa ya Magaharibi ya kutumia mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanapora raslimali za Bara la Afrika.
Kitaifa Dodoma
Katika swala iliyofanyika kitaifa katika msikiti wa Gaddafi, mkoani Dodoma, Sheikh wa mkoa huo, Mustafa Rajabu Shabani aliwataka Watanzania kutambua kuwa jukumu la kulinda amani na utulivu nchini ni la kila raia hivyo lazima misingi hiyo ijengeke kuanzia ngazi ya kaya na familia.
Sheikh Shabani alisema hakuna mtume yeyote aliyewahi kuja duniani asipate kuhubiri na kuhamasisha amani na utulivu hivyo itashangaza kama Waislamu na Watanzania wote katika dini na madhehebu yao watatokea kupuuza suala la amani na utulivu.
“Jukumu la kulinda amani ni la kila raia. Amani na utulivu katika majumba yete, katika nchi ni amana. Pindi tutakapopoteza amana hii ambayo ilianzishwa na mitume, hakika hakutakuwa na maendeleo tena. Hakuna kufurahi wala kutulia,” alionya Sheikh Shabani.
Alisema mbali na mitume na manabii wa kale pia waasisi wa maiafa ya Afrika wakiwamo Mwalimu Julius Nyerere, Jomo Kenyatta wa Kenya, Kwame Nkuruma wa Ghana nas Muamar Ghadafi ni mifamo bora ya viongozi waliohakikisha hadhi ya Mwafrika.
Alisema Uafrika na rasilimali za nchi zao zinalindwa na kumnufaisha kila raia pamoja na kuhimiza amani na utulivu.
“Hao ndio simba wa Afrika, waliweka misingi ya amani na kulinda hadhi ya Mwafrika. Wamekuwa wakipigania amani na kupinga ubeberu wa nchi za Magharibi ambao hauashirii amani,” alisema Shekhe huyo mbele ya mamia ya waumini waliokuwa wakimsikiliza.
Aliwataka Waafrika kuwa makini na kuziepuka hila za mataifa ya Magharibi na mataifa mengine ya Ulaya ambayo yamekuwa yakipenya katika nchi za Kiafrika kwa malengo ya kuvuruga amani.Alisema nchi za Ulaya kwa kutumia mwamvuli huo zimekuwa zikieneza chuki na kupenyeza vibaraka wao ili ziweze kupora rasilimali za nchi husika barani Afrika hasa almasi, dhahabu na mafuta.
Kufuata mafundisho
Sheikh wa Wilaya ya Pangani, Tanga, Juma Luwuchu alisema waisalmu wamesahau maagizo muhimu ya dini yao ya kutoa sadaka na kuwasaidia kwa hali na mali watu wasiojiweza.
Alisema kwamba waumini wengi wamekuwa wakitekeleza ibada hiyo katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani pekee huku wakisahau kuwa wanahitajika kufanya hivyo wakati wote.
“Waislamu tumeacha ibada muhimu ambayo kama tutaifuata kama alivyoagiza Mtume Mohamad, tutajikuta tukileta amani na mshikamano miongoni mwa jamii na hivyo kuiletea baraka nchi
yetu,” alisema Sheikh Luwuchu.
Kuhusu vijana, Sheikh huyo aliwaasa kuacha kuiga tabia za watu wa Kimagharibi na kwamba Uislamu unautamaduni uliokamilika kuanzia mavazi, kutembea, kuzungumza na hata namna ya kujenga mahusiano
na watu.
Kufuata ibada
Akizungumza katika swala ya Eid iliyofanyika jana katika msikiti wa Ibadhi Jijini Tanga, Imamu Mkuu, Shekh Mohamed Said alisema ikiwa muumini aliyeweza kujifunga kwa kula na kunywa na kuacha vilivyoharamishwa katika mwezi mzima basi ni wajibu wake kuendeleza akiwa na imani hiyo.
Alisema Mungu hakuharamisha vilivyoharamishwa katika mwezi mmoja wa ramadhani tu, bali haramu inabaki kuwa haramu na kuwasisitiza Waislamu waliohudhuria ibada hiyo kuwa mafundisho walioyapata wanayaendeleza pia katika miezi mengine.
Alisema mara nyingi waislamu wanafurika katika misikiti wakati wa Ramadhani kwa kufanya ibada lakini mara mwezi huo inapomalizika mahudhurio yanakuwa ya watu wachache.“Ndugu zangu Waislamu tumeshuhudia kipindi chote cha mwezi mtukufu jinsi waumuni waliyofurika katika nyumba za ibada na baadhi kushindwa kupata sehemu ya kuswalia. Hii inaonesha kuwa Ramadhani ni mwezi wa machumo,” alisema Imamu huyo.
Bakwata Dar walalama
Sheikhe Mkuu wa Bakwata, Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum ameiomba serikali kufanya uchunguzi ili kubaini uhalali wa Radio Imani ya mkoani Morogoro kutangaza siku ya Eid bila kuzingatia taratibu.
Alidai redio hiyo ilienda kinyume na maadili ya dini ambayo mwenye mamlaka ya kutangaza sikukuu ya Eid ni Sheikh Mkuu wa Bakwata.
Alisema hayo wakati ambapo Waislam wa Ansawar Sunna walisheherekea Eid Jumanne wakati ambapo Bakwata ilitangaza kuwa siyo sikukuu kwa sababu hakukuwepo taarifa za kuandama kwa mwezi Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda wala Kenya.
Alisema taarifa zilizotolewa na kituo cha Radio Imani cha Morogoro kuwa mwezi umeandama, kulisababisha mtafaruku miongoni mwa Waislam.“Mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za kuandama kwa mwezi ni Bakwata kupitia Sheikhe Mkuu na sio mtu yeyote,” alisema Salum na kuongeza:
Kwa taarifa zilizotolewa na kituo hicho cha radio, kinaweza kusababisha mpasuko na machafuko kwa Waislamu kwa kutoa taarifa alizodai hazikuwa na ukweli.
Habari hii imeandikwa na Israel Mgussi, Dodoma, Burhani Yakub,Pangani, Salim Mohamed, Tanga, Said Powa na Ibrahim Yamola, Dar
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - JK: Kanisa halina mkono Mahakama ya Kadhi
0 comments