Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KIMATAIFA , HABARI ZA LEO - Ubalozi wa Libya nchini wakaidi amri ya Membe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Bendera iliyokuwa inatumiwa na Gaddafi

Bendera inayotumiwa na waasi ambayo inaaminika kuwa ilikuwa ni bendera ya Libya baada ya uhuru mwaka 1951
UBALOZI wa Libya nchini umeendelea na msimamo wake wa kupeperusha bendera ya waasi, licha ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuonya kuwa umekiuka taratibu za kidiplomasia.

Msimamo wa ubalozi huo ni kinyume na msimamo wa Tanzania ambayo hautambui Baraza la Mpito (NTC) huko Libya, linaongozwa na waasi wanaotaka kuiangusha Serikali ya Kanali  Muammar Gaddafi.

Hadi jana, Ubalozi wa Libya hapa nchini ambao upo Upanga, Dar es Salaam ulikuwa ukipeperusha bendera hiyo ya waasi ambayo ina rangi nne; nyeupe, nyekundu, nyeusi na kijani.

Bendera ya Taifa la Libya chini ya uongozi wa Gaddafi ilikuwa na rangi ya kijani.Wachunguzi wa mambo wanasema huenda msimamo wa balozi huyo wa Libya ukasababisha apewe amri ya kuondoka nchini kama ilivyokuwa kwa aliyeko Zimbabwe, ambaye tayari ameambiwa afunge virago vyake.

Sehemu mbalimbali nchini Libya ambazo zipo chini ya waasi zinapeperushwa bendera hiyo mpya, ambayo inaelezewa kuwa ilikuwa ikitumika baada ya Libya kupata uhuru mwaka 1951.

Mwanzoni mwa wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alikuja juu akisema ubalozi wa Libya ulipeperusha bendera hiyo ya waasi kinyume cha taratibu.

Membe alisema taratibu za kubadili nembo ya taifa lolote kwenye ubalozi katika nchi yoyote ni lazima lifuate taratibu zikiwapo za uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia kwa nchi husika.

Katika kuchukua hatua, Membe alimwita Balozi wa Libya hapa nchini, Ahmed Ash’hab ofisini kwake na kufanya naye mazungumzo.Hata hivyo, hadi jana wizara haikuweka wazi walichoafikiana kwenye mazungumzo hayo yaliyochukua saa kadhaa wizarani.

Lakini kitendo cha bendera hiyo ya waasi kuendelea kupepea kwenye ubalozi huo siku moja baada ya mazungumzo hayo, kinaashiria kwamba  Ash’hab hakubaliani na msimamo wa Membe.

Juhudi za kumpata Membe ili aelezee juu ya mustakabali wa mazungumzo hayo ziligonga ukuta baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokelewa.

Ofisa Mawasiliano ya Umma wa wizara hiyo, Assah Mwambene alisema kuwa hajui lolote kuhusu maafikiano ya viongozi hao kwenye kikao chao cha juzi.Hatua ya ubalozi wa Libya nchini kupandisha bendera ya upinzani ni mfululizo wa balozi mbalimbali za nchi hiyo duniani.

Baadhi ya balozi ambazo zimeripotiwa kupandisha bendera ya waasi wa Libya ni Pakistan, Ufilipino, Uturuki, Zimbabwe na Namibia.

Hata hivyo, Balozi wa Libya nchini Zimbabwe, Taher El Magrahi tayari amekumbana na vipingamizi kutoka kwa Serikali ya Rais Robert Mugabe.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard la Zimbabwe, toleo la Jumapili iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi hiyo ilimwamuru El Magrahi kushusha bendera hiyo haraka na kupandisha iliyokuwa ya Serikali ya Gaddafi.


Ubalozi huo wa Libya nchini Zimbabwe ulipandisha bendera hiyo ya NTC baada ya waasi kufanikiwa kuuteka Mji Mkuu wa Tripol, yakiwapo makazi ya Gaddafi.

Amri ya Serikali ya Zimbabwe ya kutaka ubalozi huo kushusha bendera ya waasi wa Libya ulipingwa vikali na El Magrahi.Yeye alijitetea kuwa bendera hiyo siyo mpya bali ni ya taifa hilo la Libya ambayo ilikuwa inatumiwa tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1951.

Msimamo wa El Magrahi ulisababisha Serikali ya Zimbabwe kutoa amri ya balozi huyo kufunga virago vyake na kurejea nchini mwao.Hadi jana, hakukuwepo na taarifa iwapo balozi huyo ametii amri hiyo.


Nchi nyingi za Afrika hazijatoa msimamo wao juu ya kuwatambua au kutowatambua waasi chini ya baraza lao la NTC.NTC limekuwa likiungwa mkono na Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa ya Magharibi.

Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato) ukiongozwa na Marekani umekuwa ukiwasaidia waasi wa  Libya kwa kuhujumu nguvu za kijeshi za Serikali ya Gaddafi kwa mashambulizi ya anga.

Katika kikao cha Umoja wa Afrika (AU) kilichofanyika hivi karibuni, kilitoa msimamo wa kutotambua moja kwa moja NTC.Badala yake, AU ilishauri iundwe Serikali ya Mpito ambayo itawahusisha pia wajumbe kutoka Serikali iliyoangushwa ya Gaddafi.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites


0 comments

Post a Comment