IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MMILIKI wa Chuo cha Ualimu Green Bird, kilicho wilayani hapa, mkoani Kilimanjaro, Habibu Mndemu amefariki dunia baada ya kushambuliwa na ng’ombe.
Tukio hilo limetokea jana wakati Mndemu alipokuwa akikagua mazingira chuoni hapo katika moja ya majukumu yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na kukagua mradi wa mifugo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mtumishi wa shamba la mifugo chuoni hapo, Zakaria Simoni alisema mmiliki huyo alikuwa na kawaida ya kukagua ng’ombe kila siku hadi anafikwa na mauti hayo.
Alisema wakati yeye anaendelea na usafi baada ya kuwatoa ng’ombe nje, alisikia kishindo kikubwa na kelele, alipotoka alikuta dume la ng’ombe limemwangusha Mndemu huku likimpiga kwa kichwa na kumkanyaga kila sehemu ya mwili.
Simoni alisema kuwa alianza kufanya jitihada za kumuokoa kwa kumchapa ng’ombe huyo kwa fimbo huku akipiga yowe, lakini haikusaidia hadi alipotokea mwalimu mmoja na kumpiga kichwani kwa kutumia jembe ng’ombe huyo.
Alisema baada ya tukio hilo, walimchukua Mndemu hadi kituo cha afya Mwanga na wakati kunafanyika jitihada za kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya KCMC alifariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko alikiri jeshi lake kupokea taarifa ya tukio na kusema uchunguzi unaendelea kutambua chanzo kwa kumtumia mtaalamu wa mifugo.
You Are Here: Home - - Ng'ombe aua mkuu wa chuo Mwanga
0 comments