Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Hali si shwari Wilayani Tarime

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAKATI serikali ikisema watu watano waliouawa na polisi wilayani, Tarime Mkoa wa Mara walikuwa ni wahalifu waliotaka kuvamia Mgodi wa North Mara Barrick, msafara wa Mbunge wa Jimbo hilo (CCM), Nyambari Nyangwine umeshambuliwa katika mkutano wa kuzungumzia sakata hilo.Tukio hilo lilitokea jana muda wa saa saba mchana mara baada ya mbunge huyo kuingia ghafla kwenye mkutano wa jamii maarufu kama Ritongo kwenye eneo la Mnada wa Matongo.Vurugu kubwa ziliibuka na kusababisha msafara wa mbunge huyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Amos Sagara kupondwa mawe.Katika tukio hilo, walinzi wa viongozi hao walijeruhiwa vibaya na baadhi ya magari kuharibiwa.

Mbunge asimulia alivyotimuliwa
Akisimulia tukio hilo, mbunge huyo alisema: "Mimi na mwenyekiti wa halmashauri, tulikwenda kutaka kuwafariji wenzetu wa eneo la Nyamongo ambao ndugu zao waliuawa na polisi wakati wakidaiwa kuvamia Mgodi wa North Mara mwanzoni mwa wiki hii na watu watano kuuawa."

Alisema walitaka kufanya mkutano na wananchi katika eneo la Stendi la Kewanja Nyamongo: "Tulifika na kuanza kukaa kabla hatujaanza kuhutubia lilijitokeza kundi kubwa la vijana zaidi ya 100 na kuanza kudai wanachama tulioongozana nao, wakiwa na sare za CCM wazivue na kuondoka maeneo hayo nikiwamo mimi."

Alisema baada ya tamko hilo, vijana hao walianza kuwashambulia viongozi hao kwa mawe.
Alisema katika tukio hilo, walinzi wake sita wakiongozwa na Godfrey Francis na Sutwa, walijaribu kupambana na kundi hilo ndipo yeye (Nyangwine) alipofanikiwa kupenya na  kuingia katika gari na kuondoka. hata hivyo, walirushiwa mawe yaliyowajeruhi baadhi ya walinzi hao na kuharibu magari yao.

Alisema katika msafara huo, magari yaliyoharibiwa kwa kuvunjwa vioo vyote na kupondwa mawe ni pamoja na lile la Idara ya Elimu aina ya Land Cruser, alilokuwa nalo mwenyekiti huyo wa halmashauri. Mengine ni Toyota RAV4 na Toyota Prado.Mbunge huyo alisema tukio hilo la kushambuliwa kwao lilitokea saa 5.00 asubuhi.

Baada ya kushambuliwa Mbunge huyo aliwaambia vijana hao: "Wananchi wa Nyamongo msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kuvamia Mgodi wa North Mara na kuwashambulia viongozi wa umma kwa kuwapiga mawe, suluhu inapatikana kwa pande zinazopingana kukaa pamoja wala si kurushiana mawe."

"Tumekuja kwa nia njema kuwafariji, lakini baadhi ya wanasiasa wamegeuza maafa haya kama mtaji wa kupandia, jambo ambalo ni hatari kwa jamii ya Kitanzania nakemea na kulaani kitendo hiki."

Alisema katika mkutano huo uliovurugwa, alitaka kuzungumzia masuala ya mauaji ya mara kwa mara kati ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo na sababu za kuvamiwa kwa mgodi ambao wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakidai kutolipwa fidia ya mali zao.

Alisema serikali itaunda tume huru itakayowashirikisha wananchi, viongozi wa vijiji, wa serikali, wazee wa mila na wamiliki wa Mgodi huo wa North Mara Barrick.

Diwani naye aeleza  kilichotokea
Diwani wa Kata ya Matongo (Chadema), Bathlomeo Machage alidai kuwa wananchi walihamaki kumwona mbunge huyo na timu yake iliyovalia sare za CCM ikiingia kwenye mkutano wa jamii ambao haukumhusu.

“Nilimkaribisha kiti kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa kiongozi pekee zaidi ya wazee wa mila, tukasalimiana, lakini yeye akachukua kipaza sauti cha gari lake la matangazo maana walikuwa wanatoka kumpokea katibu mkuu wao wa taifa,” alisema.

Alisema kitendo hicho kiliibua mzozo huku wananchi wakisema mkutano huo haukuwa wa CCM na kuhoji iweje aende na sare za chama na kutaka kuwahutubia wakati hawakuwa wamemwalika.

“Alisema anakuja kuwapa pole, hapo ndipo wananchi wakachachamaa na kudai alikuwa wapi na hizo sare zake hazitakiwi. Alitulia kidogo, nikamwomba awasikilize wananchi maana ndiyo wenye mkutano, hakunielewa akataka kuzungumza,” alisema diwani huyo.
Alisema baada ya mabishano hayo kuliibuka hasira na wananchi wakaanza kupiga yowe iliyowavuta wengine na kuanza kukusanyika.

Baada ya kukusanyika diwani huyo anasema walianza kumrushia mawe mbunge huyo na wafuasi wake. Alisema baadhi ya vijana walifanikiwa kumnusuru na kumwingiza ndani ya gari ambalo pia lilishambuliwa pamoja na mengine katika msafara wake.

“Alishambuliwa gari lake na kupigwa vioo kwa nyuma, lakini lile la halmashauri limeharibiwa sana kwa kweli hali ilichafuka na mimi nikalazimika kukimbia eneo hilo,” alisema.

Machage alisema mara baada ya vurugu hizo kundi la vijana waliokuwa wamepandwa na jazba walijikusanya wakitaka kwenda kuvamia mgodi huo kwa lengo la kuuchoma moto.“Kwa kushirikiana na wazee wa mila tulifanikiwa kuzima jaribio hilo na kuwarudisha vijana na hali irejea kuwa ya utulivu,” alisema.

Sijawahi kuona ghasia kama hizi
Akizungumzia ghasia hizo, Mwandishi wa Habari wa ITV na Redio One, Mkoa wa Mara , George Marato alisema: “Sijawahi kuona tukio kama hilo tangu nizaliwe maana walinivamia hata mimi wakidai wapo waandishi wanaondika habari za upotoshaji na kupiga gari tulilokuwa nalo, wapo wanaonifahamu wakanitetea nikaachwa. Hapa nilipo nimepoteza baadhi ya vitu nimechafuka sana,” alisema.

Baadhi ya wananchi walisema wamekerwa na kitendo cha mbunge huyo kutokwenda kukutana na wananchi waliopiga kambi katika Hospitali ya Wilaya kwa siku mbili, wakiwa wamesusa kuchukua miili ya ndugu zao waliouawa kwa kupigwa risasi na askari polisi badala yake alikwenda kwenye mkutano wa CCM.Zaidi ya watu 200 walikusanyika nje ya chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya Tarime wakitokea maeneo ya Nyamongo.

Kauli ya serikali kuhusu mauaji ya Tarime
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Hamis Kagasheki alisema, polisi waliamua kutumia nguvu baada ya kuzidiwa na kundi kubwa la watu hasa baada ya kupiga mabomu ya machozi bila mafanikio.

“Tukio hili limetokea katika mazingira haya kwa sababu walikuwa ni watu wengi na tunasikitika kwa sababu hakuna serikali inayopenda kuua raia wake. Ingekuwa askari waliwafuata watu hao katika maeneo yao ya kazi, hapo unaweza kusema jeshi la polisi lina uonevu.”

Alisema kabla ya tukio hilo la juzi, kulitokea mengine, Mei 7 na Mei 14, mwaka huu katika mgodi huo na watu walipora mali lakini hakukuwa na mauaji.Balozi Kagasheki alisema katika tukio la juzi, takriban watu 1,500 walivamia mgodi huo kwa nia ya kwenda kwenye kinu cha dhahabu na kusema katika tukio hilo, pia walivunja magari na kujeruhi polisi saba.

Alisema tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), ametuma timu maalumu kwenda eneo hilo kufanya uchunguzi wa tukio hilo.Katika hatua nyingine, Kagasheki amesema ameshangazwa na baadhi ya watu kuligeuza tukio hilo mtaji wa kisiasa na kuwahamasisha wafiwa wakatae msaada wa serikali kwa ajili ya mazishi.Balozi Kagasheki alisema chama kimoja cha siasa kiliomba kibali cha kufanya maandamano na mkutano wa hadhara leo katika eneo hilo lakini kimenyimwa.

Alisema walikataa kutoa kibali hicho kwa sababu maandamano yaliyopangwa kufanywa, yanahatarisha amani.
“Tunakiri kwamba hawa ni wahalifu lakini bado ni Watanzania wenzetu ndiyo maana kama serikali tumeamua kutoa msaada wa mazishi,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema hadi sasa ni familia moja tu iliyokubali msaada wa mazishi kutoka serikalini lakini familia nyingine nne zimekataa.Naibu Waziri huyo aliwaonya wale wote watakaokwenda kinyume na kufanya shari katika eneo hilo, kwamba sheria itachukua mkondo wake.

Watu waliouawa katika tukio hilo ni Chacha Ngoko (25), mkazi wa Kewanja Nyamongo, Emmanuel Magige Ghati (19), mkazi wa Kijiji cha Nyakunguru, Chacha Mwasi (23), mkazi wa Kijiji cha Bisarwi Komaswa na wengine wawili ambao majina yao hayakutambuliwa.

Wabunge Chadema watinga Tarime
Wabunge wawili wa Chadema, Godless Lema (Arusha Mjini) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani na Esther Matiko (Viti Maalumu na Waziri Kivuli - Uwekezaji), wamewasili Tarime na kukutana na ndugu wa waliofiwa wakitaka maiti zisichukuliwe hadi uchunguzi wa kina utakapokamilika.

Lema alisema matatizo hayo yanatokea kwa sababu ya mfumo mbovu wa utawala wa nchi kutotii Katiba na sheria zilizopo wakisema mauaji yaliyofanywa hayakustahili kwa kuwa watu walikuwa wanapigwa hadi vichwani.
Alisema chama kitatoa tamko lakini hakishabikii uvunjaji wa amani na kwamba hakipendi kuona watu wanauawa na polisi wenye dhamana ya kuwalinda.

“Hapa tukio si msiba, bali iwe alama ya kudai ukombozi mauaji yakome, maana kijana kama huyu Emanuel Magige kamaliza kidato cha sita anataka kwenda chuo kikuu, leo ameuawa ni hatari! Tunakwena wapi sisi?” Alisema na kuongeza:"Tunataka nchi za Afrika na dunia ziilaani serikali kwa mauji yanayofanywa na vyombo vya dola. Hili nalipeleka bungeni na tunataka iwe mwisho.”

Kwa upande wake, Matiko aliwataka wananchi kuendelea kushikamana kudai haki maana mauaji hayo hayapaswi kunyamaziwa. Alisema watahakikisha haki inapatikana ili iwe fundisho.Maiti zilizobaki ni nne na moja inadaiwa kuchukuliwa usiku kwa gari la serikali hata hivyo, madai hayo hayakuthibitishwa.Kutokana na hali ilivyokuwa Mjini Tarime na viunga vyake, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mkama ameahirisha mkutano wake mjini hapo.

0 comments

Post a Comment