Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Jaji Samatta ataka mafisadi wabanwe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KASI ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma, imemtisha Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta, ambaye amevitaka vyombo vya habari kukemea bila uwoga.Jaji Samatta alisema kutokana na ufisadi huo kufanywa kwa sura tofauti, Watanzania hawawezi kushinda vita dhidi yake bila vyombo vya habari na waandishi.Alitoa kauli hiyo juzi usiku kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa waandishi bora wa habari kwa mwaka 2010.

Tuzo hizo ziliandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).“Mheshimiwa Rais (Rais wa MCT ) kama sote tujuavyo, nchi yetu imekuwa inapata mapigo makubwa ya ufisadi katika sura zake mbalimbali," alisema na kuongeza: "Ningependa kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vya habari, ambavyo vimejitokeza kwa ujasiri mkubwa kushiriki mapambano dhidi ya maovu hayo.”

Kwa mujibu wa Jaji Samatta, mafisadi wanaamini kuwa nchi inawahitaji zaidi kuliko wao wanavyoihitaji fikra ambazo ni finyu na hazina tija.“Naogopa sana kufikiri kitu gani kitatokea iwapo watu jasiri wakiweka chini silaha zao na kutangaza kuwa mafisadi wameshinda vita.
Au wanahabari mkiamua kuwa kalamu, kompyuta, 'microfone' na kamera zenu, sasa havitatumika katika vita dhidi ya mafisadi,” alisema Jaji Samatta na kuongeza:”Wanahabari msimwonee mwananchi yeyote, lakini, vilevile msimwogope mtu. Lishughulikieni kila suala linalojitokeza kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za maadili ya taaluma yenu,Pambaneni na wale wote nchini wanaokubaliana na matamshi ya kutisha aliyotoa Napolean Bonaparte, mtawala wa Ufaransa kwenye karne ya 19 aliposema:Kuna kitu kimoja tu hapa duniani, nacho ni kuendelea kupata fedha na fedha zaidi, mamlaka na mamlaka zaidi.

Vitu vingine vinavyobaki havina maana.”Alisema mafisadi wasipate picha kuwa, falsafa hiyo inakubalika hata Tanzania, ili vizazi vinavyokuja visipate shida kuona au kutambua kuwa kwenye vita dhidi ya ufisadi, waandishi wa habari hawakusita kuwa upande wa wanyonge.Jaji Samatta alisema bila kuwashinda mafisadi, siku zote uhuru wa mwananchi, demokrasia na utawala wa sheria vitakuwa hatarini.Alisema taarifa zinaonyesha mafisadi wapo hadi ngazi ya serikali ya vijiji na kwamba, kwa kupitia vyombo vya habari anapata nguvu ya kuamini taifa halijaishiwa watu jasiri.

”Mafisadi inasemekana sasa wako hadi ngazi ya serikali za vijiji. Nisomapo baadhi ya makala katika magazeti na kusikiliza baadhi ya maoni kwenye runinga, au redio, napata nguvu kuamini kuwa nchi yetu haijaishiwa watu ambao ni jasiri kupambana na ufisadi,” alisema.Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, alimnukuu mmoja wa viongozi wa Marekani, Thomas Jefferson, aliyesema: Kama ningepewa na uwezo wa kuamua kama tuwe na serikali bila magazeti, au magazeti bila serikali, ningependelea bila kusita hilo la pili.

”Jaji Samata alisema hakuna mashaka kuwa, kuna watu wengi duniani ambao hawatakubaliana na maoni hayo, lakini anaamini hakuna mpenda demokrasia na utawala wa sheria anayeweza kusita kukubali kuwa vyombo vya habari vina umuhimu wa kipekee kwenye maisha ya binadamu. Alisema kwenye vyombo vya habari vinavyowajibika ipasavyo, madikteta, mafisadi, wala rushwa, wakandamizaji na wabaguzi hupata shida kufanikisha matakwa yao.

“Kuvifunga minyororo vyombo vya habari, ni kuwafunga minyororo wananchi,” alisema Jaji Samata.Pia, Jaji Samatta alivitaka vyombo vya habari vya umma, kutoa nafasi sawa kwa vyama vya siasa vinavyotambulika kisheria, badala ya kupendelea chama tawala.

Katika hatua nyingine, Jaji Samatta alisema sekta ya mahakama ni moyo wa demokrasia, lakini mahakama zilizo huru na zisizo na uwoga.Jaji Samata alivitaka vyombo vya habari kutoa mchango wake kuwezesha wananchi na viongozi kuheshimu uamuzi wa mahakama.Kuhusu katiba mpya, Jaji Samata alisema kama taifa likipata katiba isiyoridhisha, haitakuwa rahisi kwa vyombo vya habari kukwepa kuwa kwenye makundi yatakayolaumiwa.

0 comments

Post a Comment