Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Spika ashtakiwa rasmi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KAMBI ya Upinzani bungeni imetekeleza azimio lake la kumshtaki Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa kile wanachodai anapendelea serikali bungeni, kwa kuwasilisha rasmi barua ya malalamiko ofisi ya Katibu wa Bunge.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, zimeeleza kuwa barua hiyo iliyopelekwa Kamati ya Kanuni za Bunge, iliwasilishwa ramsi juzi jioni.


"Ni kweli barua hiyo nimeipata, wameileta jana (juzi) mchana na sasa ninaendelea na mchakato wa kuitisha kikao cha kamati hiyo kujadili suala hilo," alisema Joel.Hata hivyo, Joel alisema kujadiliwa kwa suala hilo kutategemea mapendekezo yatakayotolewa na mwanasheria wa Bunge ambaye kwa mujibu wa utalaamu alionao katika masuala ya kanuni za bunge, anaweza kulitupa shtaka hilo au kulikubali.


"Nasema nimeipokea na iko kwenye mchakato, lakini kumbuka taasisi hii inaendeshwa kisheria na ina mwanasheria wake. Tutampa aipitie na akiona kuna kasoro, atawasiliana na mlalamikaji kumshauri cha kufanya, akiona iko sahihi itaendelea kwenye mchakato mwingine," alisema.


Akifafanua jinsi ya suala hilo litakavyoshughulikiwa, Joel alisema: "Malalamiko hayo yanaletwa kwa kutumia kanuni ya 5(4) ya Bunge ambayo inasema: Mbunge ambaye anaona haridhishwi na mwenendo wa spika bungeni, anaweza kulalamika kwenye Kamati ya Kanuni ya Bunge."


"Kanuni ya 5 inasema, Spika ataitisha kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge na Kanuni ya 6 inasema: Spika au Naibu Spika anayelalamikiwa hatakuwapo kwenye kikao hicho na wajumbe wa kamati watamchagua mmoja wao kwa kura zenye ushindi wa asilimia 50 kuongoza kikao hicho."


Shtaka hilo limefunguliwa wakati tayari Makinda akieleza kuwa, yuko tayari kuhojiwa kwa sababu anaamini hana tatizo lolote katika uendeshaji wake wa vikao.


Wiki iliyopita, Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, alisema atawasilisha kwenye Kamati ya Bunge malalamiko dhidi ya Makinda kuwa anapendelea serikali katika uongozaji wa mijadala ya bunge.


Jana Tundu Lissu alisisitiza kuwa tayari amewasilisha barua hiyo kwenye kamati hiyo na anasubiri utaratibu mwingine unaofuata.

0 comments

Post a Comment