IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
LAMTAKA AACHE KILA KITU ALICHOPEWA, MTIKILA AMUUNGA MKONO
OFISI ya Bunge imemtaka Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kususia pia huduma zingine anazopewa na Serikali kulingana na wadhifa wake, badala ya kukataa gari, dereva na mafuta pekee.Akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema huduma zote anazopewa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni zipo kisheria, hivyo hawezi kuchagua masharti anayotaka kuyafuata na mengine kuyakataa.
"Haya ni mambo ya kisiasa na sisi kama watendaji hatutaki kujiingiza kwenye siasa. Lakini niseme tu kwamba, lile gari hakupewa kufanyia shughuli za kisiasa ni la Serikali kwa ajili ya kazi zake kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni," alisema Joel na kuongeza:
"Wabunge wote wanaongozwa kwa masharti, Spika ana masharti yake, Kiongozi wa Upinzani Bungeni ana masharti yake na wabunge wengine nao wana masharti yao. Sasa mtu huwezi kukubali masharti fulani na kukataa mengine, huku ni kuvunja sheria."
Joel alisema moja ya masharti aliyopewa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ni kupokea gari la Serikali, dereva na kuwekewa mafuta kwenye gari hilo wakati wa shughuli za Bunge.
"Sasa pamoja na kupewa gari, Ofisi ya Bunge pia inawajibika kisheria kumpa kiongozi huyo nyumba mbili; Dar es Salaam na Dodoma na mlinzi wa kulinda usalama wake wa kila siku," alisema Joel.Aliendelea,"Sasa akisema gari sitaki, huu ni utashi wake, lakini kwa nini akatae gari tu wakati kuna huduma zingine anazopewa?"
Juzi baada ya kupitishwa Bajeti ya Serikali, Kambi ya Upinzani ilitangaza mgogoro na Bunge wa kutochukua posho za vikao vya Bunge kuanzia jana. Lakini hili lingefanyika baada ya kuwasilisha taarifa rasmi bungeni jana.
Sakata la kugomea posho za vikao, lilitangazwa kwa mara ya kwanza na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe na tayari ameandika barua ya kuikataa posho hiyo.
Hata hivyo, wakati kambi hiyo ikitoa msimamo huo wa pamoja, Mbowe alitangaza kuacha kutumia gari alililopewa na Serikali, dereva na mafuta kama sehemu ya kuonyesha kutoridhishwa na hatua ya Serikali kudharau mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na kambi hiyo kuiboresha bajeti.
"Tumewaita hapa kueleza msimamo wetu kama Kambi ya Upinzani baada ya Serikali kuyakataa baadhi ya mapendekezo yetu. Serikali haikukubaliani nasi kuondoa sitting allowances (posho ya vikao),"alisema Mbowe na kuongeza:
"Haikukubaliana nasi pia kuuza mashangingi ya anasa, kuondoa misamaha ya kodi kwenye makampuni ya madini, katika susala la pension kwa wastaafu na kupunguza gharama za kuwasafirisha viongozi wa umma kwenye first class (daraja la kwanza)."
"Sisi tunaamini kuwa viongozi wanaopaswa kusafirishwa kwa ndege katika daraja la kwanza ni Rais na mke wake, Makamu wa Rais na mkewe, Waziri Mkuu na mke wake, Spika wa Bunge na mwenza wake. Halafu mawaziri wanapaswa kusafiri kwa daraja la kawaida na wabunge wote,"
Aliendelea" Na kwa kuwa hawataaki kukubaliana nasi kuuza magari ya fahari, mimi kuanzia sasa (juzi), silitaki gari lao, dereva wao na hata mafuta yao, habari ndio hii."
Barua ya Chadema haijafika Ofisi za Bunge
Lakini Joel alisema kuwa hadi jana mchana, hakuwa amepokea barua yoyote kutoka Chadema ya wabunge wake kukataa posho wala Mbowe, kugoma kuendelea kulitumia gari, dereva wala mafuta.
"Siwezi kufanya kazi kwa taarifa za vyombo vya habari. Mbowe hajanipa gari wala sijapata barua ya wabunge kukataa posho. Mambo hayo yapo kisheria muulizeni (Mbowe) kanipa lini gari hilo?"alihoji
Bunge kuendelea kuwalipa posho
Kuhusu wabunge hao kutochukua posho, Joel alisema posho hizo hazitasitishwa kutolewa kwao hadi utaratibu utakapobadilishwa. "Haya mambo yapo kisheria jamani, nisipowalipa posho mimi nashtakiwa," alisema.
Aliendelea"Mbunge anapewa posho kama sharti namba 3. Sasa kusitisha posho hizo ni mlolongo mrefu ambao hauwezi kufanyika kwa haraka kiasi hicho. Kinachoweza kufanyika, ni kila mbunge anayetaka kutochukua posho kuniandikia barua na sio kama kambi kwa sababu posho hizo ni za mbunge."
Akishaniandikia barua, alisema " Kuna njia mbili; moja ni mimi kumpa posho yake halafu yeye airudishe serikalini au mimi niikatie risiti halafu niirudishe serikalini, lakini haiwezi kupelekwa kwingine kokote zaidi ya kuwapa wabunge wenyewe."
Joel alipuuza madai ya kambi hiyo kutaka kuwe na fomu mbili bungeni; kulipana posho bungeni na fomu ya mahudhurio ili wao wasaini fomu ya mahudhurio tu, wasipewe posho hizo, akisema "Fomu iliyopo ni ya mahudhurio, wanataka fomu gani sasa?
Lissu adai Mbowe alirejesha shangingi
Mbowe jana hakupatiakana ofisini kwake kuzungumzia suala hilo, lakini, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisisitiza kuwa tayari alirejesha gari hilo tangu Jumatatu.
"Ni kweli barua hatujapeleka ila itapelekwa kesho, lakini tayari Mbowe amerudisha gari hilo tangu juzi (Jumatatu) na ameanza kutumia usafiri binafsi," alisema Lissu.
…apongezwa kwa kurudisha shangingi
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanasiasa, wasomi na wananchi wamepongeza uamuzi wa Mbowe wa kurudisha gari la Serikali ili kuipunguzia gharama za uendeshaji.
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila aliunga mkono uamuzi huo na kusema hata katika nchi tajiri viongozi wenye nyadhifa za uwaziri wanatembelea magari ya kawaida.
“Uingereza nchi tajiri, lakini mawaziri wake wanatembelea vigari vidogo vinaitwa Austin, lakini sisi na umaskini wetu mawaziri wanatembelea magari ya kifahari,” alisema Mtikila na kuongeza.
“ Inashangaza sisi walalahoi, lakini viongozi wanatembelea magari ya kifahari kuwashinda wanaotupa misaada, hivi viongozi hawa hawajifunzi,” alisema Mtikila.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), Dk Benson Bana alisema, Mbowe ana hoja ambayo inapaswa kuungwa mkono na watu wengi wenye kuitakia mema nchi hii.
Dk Bana alisema ingawa hoja hiyo inamjenga Mbowe kisiasa, lakini ukweli unabaki kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuyahudumia magari hayo.
Naye Shaaban Mtawa, fundi wa magari wa Kinondoni jijini alisema kitendo cha Mbowe kurudisha gari hilo kimemfurahisha na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo.
“Viongozi wengi wanaishi Dar es Salaam, wanatembelea magari ya kifahari bila ya sababu ya msingi wakati yanatumia fedha nyingi,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kinachofanywa na Mbowe ni propaganda za kisiasa zenye lengo la kumpatia umaarufu.
“Mbowe ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, amepewa gari kwa ajili ya kazi hiyo, anarudisha gari kwa sababu yeye ni tajiri, angekuwa hana uwezo kama wabunge wengine angefanya hivyo?,” alihoji Mtatiro.
Mtatiro alisema Mbowe asijifanye kuwa anawahurumia Watanzania maskini wakati maisha anayoishi ni ya kifahari yasiyofanana na wananchi wa kawaida.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - BUNGE LATOA MASHARTI KUPOKEA SHANGINGI LA MBOWE
0 comments