IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) Zachary Kakobe ametuma salamu za Pasaka kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kumfananisha na Pilato.
Kakobe amefikia uamuzi huo wa kumfananisha Kikwete na Pilato akidai serikali yake ilitumia Polisi wakiwa na silaha za moto kuvunja na kung’oa mabago ya kanisa hilo kimabavu ili kupitisha nguzo za umeme wa msongo wa KV 132.
Salamu hizo amezitoa jana katika ibada maalum na takatifu ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo miaka kadhaa iliyopita kanisani kwake Mwenge barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam.
Ibada hiyo iliyotumia takribani saa tatu iliyokuwa na kichwa cha somo kisemacho ‘Kuupiga mateke Mchokoo’ alitumia dakika 15 kuitupia madongo Serikali ya Awamu ya Nne kwa kusema walichokifanya ni sawa na kupiga mwiba mkali mateke wakiwa peku.
Maneno hayo yalikuwa yakimtoka Askofu huyo huku akishangiliwa na waumini wake waliokuwa wamefurika katika ibada hiyo ya Pasaka ambayo huadhimishwa mara moja kwa mwaka na kuwataka waumini kununua kanda za somo hilo ili wampelekee Rais Kikwete ambaye yeye anamuita Pilato akasikilize.
"Hata kama Pilato ameamuru kuvunjwa na kung’olewa kwa mabango ya Kanisa la Mungu bado bendera yake itapepea milele na milele, kuna kanda za mafundisho haya ya somo la leo mnunue mumpelekee Pilato asikilize," alisema Kakobe kwa jazba.
Alisema baada ya ukomunisti ulioigawa Ujerumani na kuwa na Ujerumani Mashariki na Magharibi kukoma na kuwa na Ujerumani moja sasa Tanzania umeibuka ubepari ambao nao inashindana na nguvu za Mungu.
Kakobe alisema rais ni mtu kama walivyo watu wengine hivyo kuingilia mamlaka ya Mungu ni laana kubwa ambayo atakuja kuijutia maisha yake yote.
“Kikwete na mawaziri wake wote wamediriki kuleta askari mahali hapa wakiwa na mitutu iliyokuwa na risasi ili kugombana na Kakobe wakidhani wanagombana na mwanadamu kumbe wanagombana na Mungu sasa yatawarudia,†alisema Kakobe na kuongeza.
"Mimi nashangaa baada ya Kikwete kuwa rais wa nchi hii wapo watu waliojitokeza na kusema kuwa amechaguliwa na Mungu, lakini mbona hatendi yale mema ambayo yanaifurahisha mbingu badala yake anakwenda kinyume".
Kakobe alisema kuwa nchi hii imekumbwa na ubepari usiozingatia uhalali wa watu, wapo kwa ajili ya kuonea watu ambao hawapo katika madaraka kwa kutumia mabavu ya mitutu yao.
"Pamoja na hayo yote, lakini nasema hakuna dola mbele za Mungu kwani yeye ndiye aitiaye nguvu na maarifa hivyo ni lazima kiheshimiwe kilicho chake, lakini kwa kuwa serikali hii inaongozwa na Pilato ambaye alihusika katika kifo cha Yesu basi ipo siku atajua kuwa vya Mungu apewe Mungu na vya Kaizari apewe vilivyo vyake," alisema Kakobe.
Aidha, alisema yeyote ambaye atapigana na kazi ya Yesu madhara yatamrudia mwenyewe, na hakika yameanza kuonekana kwani hivi sasa hali ni tete katika serikali yake kila kiongozi wake ni mbabe hakuna aliyemsafi huo ndiyo mshahara wake.
Kakobe alimtahadharisha Kikwete kuwa asipotubu basi yatamkuta yale yaliyomkuta Belishaza. “Hii ni salamu yangu ya Pasaka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, nasema hivyo kwa msisitizo na herufi kubwa,†alisema Kakobe.
You Are Here: Home - - Kakobe amtumia salamu za Pasaka Rais Kikwete. Katika Ujumbe wake amfananisha sawa na Pilato
0 comments