Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Bunge: Wabunge wa Chadema wamepokea posho

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter LICHA ya msimamo wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuchukua au kutochukua posho za vikao, taarifa za Ofisi ya Bunge zinaonyesha kuwa wabunge wa chama hicho isipokuwa Zitto Kabwe, wamekuwa wakisaini fedha hizo hadi kuahirishwa kwa Mkutano wa Nne wa Bunge wiki iliyopita.

Juni 7, mwaka huu Zitto aliwasilisha barua Ofisi ya Bunge kukataa posho ya Sh70,000 (Sitting allowance), kwa siku akisema watumishi wa Serikali na wabunge, hawastahili kulipwa posho wanapohudhuria vikao rasmi vya uwajibikaji wao wa kawaida ndani ya Bunge.

Msimamo huo uliungwa mkono na Kambi Rasmi ya ya Upinzani Bungeni baada ya kiongozi wake, Freeman Mbowe kusema hilo limo kwenye Ilani ya Chadema ya mwaka 2010. Pia Mbowe alikataa kutumia gari la Serikali maarufu kama shangingi.
Hata hivyo, msimamo huo ulipingwa na baadhi ya wabunge huku Mbunge kutoka chama hicho, John Shibuda akienda mbali kwa kutaka badala yake, ziongezwe ikiwezekana hadi kufikia Sh500,000.

Kaimu Katibu wa Bunge John Joel, alisema jana kuwa ni Zitto pekee ambaye ameacha kusaini fedha hizo tangu alipotoa msimamo wake.

Akizungumzia kwa simu, Joel alisema wabunge wote wa Chadema wanachukua posho lakini, Zitto amegoma kusaini.
Joel alisema katika kumbukumbu, kila Mbunge wa Chadema aliyesaini wakati akiingia kikaoni ndani ya Bunge alilipwa posho na kuongeza kwamba hakuna aliyezikataa au kuzirudisha.
“Wabunge wote wa Chadema waliosaini wamekuwa wakipewa posho, ni Zitto pekee ambaye amekuwa akigoma kusaini posho hizo,” alisisitiza Joel.

Alipoulizwa kama pia Zitto alikuwa akiingiziwa, alijibu: “Zitto hakuwa akisaini na aliacha tangu alivyotangaza msimamo wake mwezi Juni”.

Alisema kwa utaratibu, kila mbunge anayesaini wakati akiingia bungeni kuhudhuria kikao hupewa posho yake ya kikao.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliwahi kumuonya Zitto kwamba, kama asingesaini mahudhurio ambayo ndiyo yanayotumika kuandaa posho hizo, angeweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kusimamishwa ubunge.

Lakini,  duru za kisiasa zinaonyesha ingekuwa ni vigumu kwa Spika kumfukuza Zitto baada ya kugoma kusaini kwani amekuwa akionekana bungeni huku akiibua hoja nzito ikiwamo ya kulishawishi Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza suala la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kurejeshwa kazini na mamlaka ya nidhamu ambayo ni Katibu Mkuu Kiongozi.

Pia Zitto aliwasilisha kusudio la kuomba Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza tuhuma za ufisadi wa Kampuni ya Meremeta.

Msimamo wa Zitto
Juni 7, mwaka huu Zitto aliandika barua akisema posho hiyo haistahili kulipwa kwake, wabunge wengine wala watumishi wa umma kwa kuwa kuhudhuria vikao ni sehemu ya kazi zao.


Badaye, mara baada ya Chadema kutangaza msimamo huo, Spika Makinda alipinga uamuzi wa kususia posho akisema suala hilo lipo kisheria na kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kuamua kuliondoa.

Hata hivyo, akihitimisha hoja za wabunge katika hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya ofisi yake na zilizo chini yake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema suala la posho lipo kwenye mchakato wa kuangaliwa upya na kwamba zile za vikao huenda zingefutwa.

Waziri Mkuu ambaye awali alionekana kupingana na Chadema, alisema Katiba inakataza suala la posho zisizo za msingi na kwamba utaratibu huo umeandaliwa kwa kufuata utaratibu mzuri bila ya kuathiri mazingira na mfumo uliopo ndani ya Serikali kwa watumishi wake.

Hata hivyo, Shiduda ambaye ni Mbunge wa Maswa Magharibi amepinga msimamo huo wa chama chake na kujikuta akiwa katikati ya mgogoro na baadhi ya viongozi wake kiasi hata cha kutishia nafasi yake ya uanachama.

0 comments

Post a Comment