Kyrgyzstan yaamua kufunga kituo cha kijeshi cha Marekani
Mswada wa sheria umepitishwa bungeni bila ya shida.Kutoka jumla ya wabunge 81 waliokuwepo,78 wameunga mkono kukifunga kituo cha Manas. Mbunge mmoja alipinga na wawili walizuia kura zao.Baadae mbunge Zaynidin Kurmanov wa chama tawala Ak Zhol alisema, sheria hiyo sasa inapaswa kutiwa saini na Rais Kurmanbek Bakiyev alieishtusha Washington mwezi uliopita,alipotangaza mpango wa kukifunga kituo hicho cha kijeshi.
Baada ya kutiwa saini, Marekani itaarifiwa kukiondosha kituo hicho kutoka ardhi ya Kyrgyzstan katika kipindi cha siku 180 zijazo. Kwa mujibu wa Avtandil Arabaev mbunge mwingine wa chama tawala,serikali ya Kyrgyzstan kisheria ina haki kamili kujitoa katika makubaliano yaliyotiwa saini pamoja na Marekani.Mbunge pekee aliepinga ni Bakyt Beshimov wa chama cha Social Demokratik. Yeye amesema, hatua ya kukifunga kituo hicho kutadhoofisha usalama katika kanda hiyo na ugaidi utaweza kuenea kwa urahisi.
Uamuzi wa kukifunga kituo cha kijeshi cha Marekani umepokewa kwa hisia mbali mbali katika mji mkuu Bishkek. Kwa mfano mwananchi Vladmir Morozov alisema,amefurahi kuwa hatimae mji wao hautokuwa na Wamarekani waliojifanya kama ni wamiliki wa mji huo.Lakini mwananchi mwengine alisema,wanaotaka kukifunga kituo hicho hawajui wanachozungumza. Kwa maoni yake,Wakyrgyz hawawezi kuishi peke yao. Uchumi haukui. Wanahitaji kaka mkubwa ikiwa ni Marekani,Urusi au nchi nyingine.
Rais Bakiyev alitangaza kukifunga kituo cha Manas baada ya Urusi kuahidi kutoa msaada wa zaidi ya dola bilioni mbili kufufua uchumi uliodorora nchini Kyrgyzstan.Lakini serikali imesisitiza kuwa Moscow haikutoa sharti la kukifunga kituo hicho.Moja lakini ni hakika kufungwa kwa kituo hicho cha kijeshi nchini Kyrgyzstan kutasababisha matatizo zaidi kusafirisha vifaa na mahitaji mengine ya vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan,wakati ambapo Rais wa Marekani Barack Obama amepanga kuongeza kwa takriban maradufu idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan ambako hali ya usalama inazidi kuwa mbaya.
Kituo cha Manas kinachoongozwa na kama wanajeshi 1,000 vikiwemo pia vikosi vya Ufaransa na Uhispania,kilifunguliwa nchini Kyrgyzstan kusaidia majeshi ya muungano yanayopigana dhidi ya Wataliban nchini Afghanistan. Kituo hicho kilifunguliwa kufuatia mashambilio ya Septemba 11 mwaka 2001.Baada ya Kyrgyzstan kutangaza kukifunga kituo cha Manas,Urusi na Tajikistan zimesema zipo tayari kuruhusu ardhi yao kutumiwa kusafirisha vifaa ambavyo si silaha, kwa ajili ya majeshi ya NATO na Marekani nchini Afghanistan.Lakini siku ya Jumanne,Jemadari David Petraeus alikwenda Uzbekistan kukutana na Rais Islam Karimov na kujadili usalama wa kanda hiyo.Ziara hiyo inatazamwa kama ni ishara kuwa Marekani inataka kuitumia nchi hiyo kupitisha vifaa vinavyohitajiwa na majeshi ya muungano nchini Afghanistan.
0 comments