Waziri Profesa Juma Kapuya ambaye anashauriwa kujipima na kujiuzulu uwaziri kutokana na vifo vya watoto 19 waliofariki Tabora katika ukumbi unaomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). |
PADRI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mkokola, Father Winnefrid Dinno amesema Rais Jakaya Kikwete alitumia busara kumtuma Profesa Juma Kapuya kuja Tabora kujionea vifo vya watoto 19 vilivyotokea kwenye jengo la taasisi iliyo chini ya wizara yake, ili waziri huyo ajipime na baadaye kujiwajibisha.
Watoto hao walifariki kutokana na kukosa hewa na kukanyagana wakati wakiwa kwenye ukumbi wa disko wa Bubbles ulio kwenye jengo la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambao awali ulijengwa kwa ajili ya mikutano ya watu wasiozidi 150, lakini ukabadilishwa matumizi na kuzibwa madirisha, huku ukichukua idadi kubwa zaidi ya watu.
Hitilafu ya umeme ilisababisha viyoyozi viwili vilivyo kwenye ukumbi huo kuzima na hivyo watoto kuanza kusukumana kwenda nje huku hewa ikiisha ukumbini na hivyo wengi wao kuzirai na kufa kwa kukosa hewa na kukanyagana.
Padri huyo anaona sababu hizo za kiufundi zinatosha kabisa kumfanya Profesa Kapuya, ambaye ni Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, na wengine wote waliokuja Tabora kwenye msiba huo, watubu na kujiuzulu.
Akihubiri kwenye ibada maalum ya kuwaombea waliofariki, Fr Dinno alisema Prof Kapuya anatakiwa ajiuzulu kwa kuwa anajua kuwa jengo lililoua watoto hao liko chini ya wizara yake na kwamba, alikuwa anajua kuwa kulikuwa na matukio mawili kama hayo kwenye jengo hilo, ingawa hayakuua.
"Alinyamaza kimya mpaka tukio hili limekuwa kubwa kiasi ambacho kimekuwa ni kitendawili kisicho na mteguaji," alisema Fr Dinno alirejea matukio ya mwaka 2006 na 2007 ambayo yalisababisha watoto kadhaa kuzirai baada ya kutokea hitilafu kama hiyo kwenye ukumbi wa Bubbles.
Akitoa mfano wa uwajibikaji, alisema waziri mmoja wa Russia ambaye wizara yake inajihusisha na starehe alijiuzulu mwaka huu baada ya ukumbi uliokuwa ukipiga disko kuungua moto na kusababisha vifo vya watu saba na wengine 600 kujeruhiwa wakati walipokuwa wakicheza muziki usiku kabla ya moto kulipuka na kuunguza klabu yote.
"Waziri wa Russia alijiuzulu kwa vifo tena vya watu wazima, iweje Kapuya asiachie ngazi kutokana na vifo vya watoto 19 ambao ni nguvu kazi ya kesho," alihoji huku akionyesha kutoridhika na juhudi ambazo serikali inadai inazifanya kujua chanzo.
"Kushikilia wahusika hakusaidii kwani bado watu muhimu hawajaachia ngazi. Waachie ngazi kwanza ndio haki itatendeka, vinginevyo tutaletewa ripoti ambayo hata mtu ambaye hajasoma hawezi kukubaliana nayo."
Fr Dinno alisema rais ana busara sana kwa kuwa alijua kwamba mhusika mkuu katika vifo hivyo ni waziri mwenye mamlaka na jengo hilo ndiyo maana alimtuma kumwakilisha kuhudhuria mazishi hayo ili aweze kujipima yeye mwenyewe na kuachia ngazi.
Kuhusu watu waliomwakilisha Rais Kikwete kwenye msiba huo wa kitaifa, Fr Dinno alisema viongozi hao walikuwa wakitoa maneno ya kejeli ambayo hayafai kwa wafiwa.
NSSF ilikuwa ya kwanza kutoa ubani wa Sh 500,000 kwa kila familia ambayo ilipoteza mtoto kwenye tukio hilo na Sh100,000 kwa kila familia iliyoathirika, viwango ambavyo pia vilitolewa na Rais Kikwete na kutangazwa kwa niaba yake na Waziri Kapuya.
Lakini Padri Dinno anaona uwakilishaji wa fedha hizo kwa waliofikwa na janga hilo haukuwa wa kiungwana na pengine uliwaumiza zaidi wafiwa.
Alisema viongozi hao waliotumwa walisema fedha hizo si fidia kwani watoto wangeweza kufa kwa kifo chochote na ndugu wa marehemu wasingepewa fedha, lakini wakasema serikali iliona si jambo jema kuwaacha bila kuwapa chochote.
Fr. Dinno alisema mbali na hayo, viongozi hao waliwaambia wafiwa kwamba vifo hivyo ni vya kawaida kwani kuna mtu mmoja mkoani Arusha aliwahi kununua kila kitu, lakini alipokuwa akila mfupa ulimkwama na kupoteza maisha na kwamba ndugu zake hakupewa chochote.
"Kauli za namna hiyo ni za kejeli na hazifai kwa watu ambao wana majonzi mazito kama hayo," alisema Padri huyo.
"Hawa ni viongozi wanaowakilisha watu na watu wenyewe ndio hao wanaowatolea maneno ya kejeli na katika majonzi mazito kama haya.
"Nyie viongozi ni bora mje mtubu kabla ili mtakapojiuzulu jamii iwaone kwamba kejeli mlizozitoa hamkudhamiria mkiwa kama viongozi mliotumwa na rais."
0 comments