TANZANIA imeitaka Idara ya Habari na Mawasilliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha kuwa inaongeza idadi ya waandishi katika Idhaa ya Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ili iweze kutekeleza kwa ukamilifu majukumu yake ya ukusanyaji, utoaji na usambazaji wa taarifa zinazohusu shughuli za umoja huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa Tanzania imetoa wito huo wakati wa mkutano wa 33 wa Kamati ya Habari ya Umoja wa Mataifa.
Pamoja na mambo mengine kamati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1978 ikiwa na wajumbe 113 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, juzi hiyo walipokea na kujadili taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuhusu utendaji wa idara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ofisa Ubalozi Mwandamizi, Maura Mwingira alisema katika mkutano huo, Tanzania inafarijika na kuridhishwa na namna ambavyo lugha ya Kiswahili kupitia Radio ya Kiswahili ya UN imeendelea kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano, kupata umaarufu na kuongeza idadi ya watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo licha ya kwamba ina wafanyakazi wachache.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa UN iliyowasilishwa kwa wajumbe na Katibu Mkuu Msaidizi anayeongoza Idara ya Habari, Akito Akasaka, imeonyesha kuwa, katika eneo la Radio ya Umoja wa Mataifa, Radio hiyo ambayo hutoa taarifa zake katika lugha sita rasmi za UN, na lugha mbili za Kiswahili na Kireno, imekuwa na mafanikio makubwa ambayo pia yamehusisha ongezeko la watumiaji wa taarifa zake.
Lugha rasmi za Umoja wa Mataifa ni Kiingereza, Kifaransa, Kiaarabu, Kirusi, Kichina na Kihispania, Kwa upande wa Idhaa ya Kiswahili, Akasaka alisema, Radio hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2006, idadi ya watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo imepanda kutoka asilimia moja wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia asilimia 21, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Radio Maarifa FM iliyoko Tanzania.
“Haya si mafaniko madogo, ni mafanikio makubwa ambayo kila mmoja wetu anapashwa kujivunia na tunawapongeza wafanyakazi hao wawili kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya”, alisisitiza ofisa ubalozi.
Idhaa hiyo ina wafanyakazi wawili tu, inaongozwa na Mtanzania, Flora Nducha.Ni kutokana na uchache huo wa wafanyakazi, ndio maana Tanzania imeitaka sekretarieti ya Idara hiyo ya Habari ya Umoja wa Mataifa kuangalia uwezekano wa kuongeza wafanyakazi. Idhaa nyingine zina wafanyakazi zaidi ya wanne.
Tanzania imewaeleza wajumbe wa Mkutano huo kuwa Lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 katika eneo la Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kati na nje ya maeneo hayo kwamba ni kiungo muhimu cha upashanaji wa habari hususani katika udhibiti wa migogoro na ujenzi wa amani.
Ni kutokana na umuhimu wa lugha hiyo, Tanzania imesema, ndio maana Umoja wa Afrika uliamua kwa makusudi kabisa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa kati ya lugha rasmi za umoja huo. “Kiswahili ni lugha muhimu sana kama chombo cha mawasiliano katika Umoja wa Mataifa na katika suala zima la ulinzi, usalama na ujenzi wa amani na maendeleo.
Tunatambua changamoto ya ufinyu wa bajeti inayoikabili Idara ya Habari na Umoja wa Mataifa kwa ujumla wake, Lakini bado tunaamini kwamba mtafikiria suala la kuongeza idadi ya wafanyakazi katika idhaa hiyo hivi karibuni,” akasisitiza Ofisa Ubalozi Mwandamizi.
0 comments