IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limetangaza kususia bidhaa na huduma zote zizalishwazo au kutolewa na nchi ya Uswisi kwa kile ilichokiita njama za nchi hiyo kuukandamiza Uislamu.
BAKWATA imewataka Waislamu wote nchini na duniani kutoshirikiana na nchi ya Uswisi katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na masuala yote ya jamii.
Uamuzi huo ulitangazwa jana kwenye ofisi za Makao Makuu ya BAKWATA, zilizopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam na Mufti Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua walizochukua dhidi ya Uswisi.
“Kuanzia leo tusitumie vyombo vyao vya usafiri vya abiria na mizigo, zikiwemo meli na ndege, tusiwekeze kwenye benki zao na kama yupo mwenye fedha katika chombo chochote au biashara, basi aziondoshe mara moja.
“Tusinunue bidhaa zozote zile za Uswisi, au kutumia huduma zozote za Uswisi au kuwaunga mkono katika jambo lolote lile,” alisema Mufti Simba.
Alisema uamuzi huo unatokana na amri iliyotolewa na Uswisi Novemba mwaka jana, ambapo ilipiga marufuku ujenzi wa minara katika misikiti nchini humo, kufuatia kura ya maoni ambayo zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wake waliunga mkono, na asilimia 42 wakipinga uamuzi huo.
Alisema amri hiyo ya kupiga marufuku minara ya misikiti, inaingilia haki na uhuru wao wa kufanya ibada kwa Waislamu na halitakuwa jambo jema, kitendo hicho kuachwa bila kulaaniwa.
“Hatuwezi kuona njama za kuangamiza Uislamu na sisi tukanyamaza kimya, hatukubaliani na uamuzi huu,” alisema.
Mufti Simba alisema katazo hilo halijengi umoja, mshikamano na kuvumiliana baina ya wana dini, bali inakuza uhasama na kuchochea chuki baina ya Waislamu na waumini wa dini nyingine.
“Hii ni kibri na dharau kubwa kwa Uislamu na Waislamu, si kwa wale wanaoishi Uswisi pekee, bali kwa Waislamu wote na wapenda amani duniani kote.
“Waislamu duniani kote hatuna budi kulinda na kuienzi dini yetu, na kwa hili, hatuna budi kuchukua hatua madhubuti ambazo ni za kiungwana na ambazo ziko ndani ya uwezo wetu ili kuulinda na kuuendeleza Uislamu,” alisema Sheikh Simba.
Aliongeza kuwa kama wapenda amani duniani wataungana na kukemee hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Uswisi, kuna dalili serikali hiyo kulegeza msimamo wake huo unaokiuka haki za binadamu.
“Tunawapongeza Waislamu wa Libya kupitia kiongozi wao, Muammar Gaddafi, kwa kuwa mstari wa mbele katika kulaani njama hizi. Nchi chache zimelaani, lakini bado haitoshi,” alisema Sheikh Mkuu.
Alisema pamoja na ukweli kuwa wakazi wengi wa nchi hiyo si Waislamu, bado katika ulimwengu uliostaraabika suala la kutambua, kuheshimu na kuvumiliana tofauti za kiimani ni la msingi na la lazima.
Aliongeza kuwa nchi hiyo inafahamika kwa utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimiana baina ya dini tofauti, lakini inasikitisha kuwa hivi sasa imekubali kufanyika kura za maoni katika mazingira ya propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu, jambo linaloliondolea heshima taifa hilo.
You Are Here: Home - - BAKWATA yaitenga Uswisi • YAPIGA MARUFUKU UJENZI WA MINARA MISIKITINI
0 comments