Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Fifa kujenga uwanja wa kisasa Tanzania

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MEDANI ya soka yaTanzania inaweza kunufaika kwa uwanja mpya wa kisasa wa michezo hasa soka baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kukubali kufadhili mradi huo, imebainika.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo aliiambia Mwananchi juzi kuwa ujenzi huo ulikuwa hatarini kukwama, lakini ofisi imeingilia kati na kutengua uamuzi wa halmashauri ya Jiji la Tanga kukataa kutenga eneo la ujenzi wa uwanja huo wa kimataifa wa michezo.

Jenerali Kalembo alisema kuwa ameingilia kati na kutengua maamuzi ya halmashauri ya Jiji la Tanga ya kukataa maombi yaliyokuwa yametolewa na TFF kutaka kutengwa kwa eneo kwa ajili ya kujenga uwanja ambao Fifa imetoa ofa kwa nchi mbili barani Afrika ikiwamo Tanzania.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na mkuu huyo wa mkoa ni kuwa Fifa imeshaandika barua kwa TFF ikitaka iandae eneo ili mchakato huo wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu uweze kuanza.

Baada ya kupata barua hiyo ya Fifa imeelezwa kuwa TFF iliendesha vikao vya kupendekeza mkoa gani ujengwe ndipo kura nyingi zikaangukia Tanga ambayo ilikuwa ikichuana na Mwanza.

Kutokana na kura hiyo, TFF iliuandikia barua kwa uongozi wa Jiji la Tanga kuomba litenge eneo la ujenzi huo, lakini ilishangaa kujibiwa kuwa mkoa huo hauna eneo.

Habari zilizoifikia Mwananchi ni kuwa barua hiyo ya jiji ya kukataa kutoa eneo iliandikwa kwa siri, lakini, Jenerali Kalembo alipenyezewa taarifa hizo ndipo alipowasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga na kumweleza kuwa barua ya jiji ni batili na kwamba iliandikwa na wahuni bila yeye kuhusishwa.

Akiwa katika ziara wilayani Tanga wiki iliyopita, Jenerali Kalembo aliwajia juu viongozi wa jiji hilo kwa kukataa maombi ya TFF ya kutengewa eneo kwa ajili ya kujenga uwanja huo.

“Nyie mnasema nawaonea jiji, hivi huu mchezo wenu wa kukataa uwanja mmeona ni mzuri, hamuoni kama mnataka kuzorotesha maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla?”alihoji Jenerali Kalembo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya jiji hilo.

Jenerali Kalembo alisema jitihada zake zimezaa matunda kwani tayari jiji limeshatenga eneo kubwa katika kitongoji cha Mnyanjani na limetekeleza agizo lake la kuiandikia barua TFF na kuijulisha kuhusu hilo.

“Tumeshatenga eneo kubwa kuliko hata lile la uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam na tumeshairuhusu TFF kuleta maafisa wa Fifa waje waanze mchakato wa ujenzi huu,”alisema Kalembo.

Alipoulizwa jana kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu waTFF, Fredrick Mwakalebela alikiri kuwa wamepata barua hiyo juzi kutoka kwa uongozi wa halmashauri ya jiji la Tanga.

"Mimi siwezi kusema lolote kuhusu hilo jibu kamili litalolewa na kamati ya utendaji ya TFF pindi itakapokutana na kujadili suala hilo," alijibu Mwakalebela kwa ufupi.
Tags:

0 comments

Post a Comment