Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Kamati Kuu Chadema kuwajadili madiwani wa Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KAMATI Kuu (CC) ya Chadema inakutana keshokutwa Dodoma kujadili pamoja na mambo mengine, ripoti ya mgogoro ulioibuka kati ya madiwani wa chama hicho na CCM kuhusu Meya wa Jiji la Arusha.


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, ambaye aliipokea ripoti hiyo hivi karibuni kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo na Mwanasheria wa Chadema, Mabere Marando, aliliambia gazeti hili jana, kuwa taarifa hiyo itajadiliwa na CC siku hiyo.


Dk. Slaa alisema, ameipitia na kuiwasilisha CC ambayo imefanywa kuwa miongoni mwa ajenda za mkutano huo, ili ijadiliwe na kutolewa uamuzi kabla umma haujataarifiwa kupitia njia mbalimbali zikiwamo za vyombo vya habari.


“Tuna ajenda mbalimbali katika kikao hicho cha Ijumaa wiki hii, kwanza ni kikao cha kawaida si maalumu, watu wasifikiri tunakaa kwa suala hilo, lakini moja ya ajenda ni kujadili suala hilo kwa mapana yake na kisha tutawapa taarifa,” alisema Dk. Slaa.


Alizitaja baadhi ya ajenda zitakazojadiliwa katika kikao hicho kuwa ni pamoja na kupokea taarifa ya utendaji wa chama na hali ya kisiasa ndani ya chama na nchini kwa jumla.


Kuhusu hali ya kisiasa, Dk. Slaa alipoulizwa kama watajadili suala la Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, alisema suala hilo halijamfikia na kufafanua kuwa Katiba ya chama hicho iko wazi, kuwa ni chombo gani kinafaa kumjadili Mbunge kama Shibuda.


“Hilo suala sinalo mezani kwangu, hivyo hatuwezi kujadili kitu tusichonacho, ila Katiba iko wazi, kuna mamlaka husika ya nidhamu, kamati ya wabunge wa Chadema ndiyo hasa inashughulika na suala hilo, kwanza si sisi, likiletwa kwangu sawa, ila kabla sina cha kusema,” alisisitiza Dk Slaa.


Shibuda aliwatibua nyongo wabunge wenzake wa Upinzani hasa Chadema, baada ya kutofautiana nao kuhusu posho za wabunge na watumishi wa umma akidai ataendelea kuzipokea huku akitoa kauli za kuwaponda Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (Mbunge wa Hai) na Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto (Mbunge wa Kigoma Kaskazini).


Kitendo hicho cha Shibuda aliyehamia Chadema katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana akitokea CCM, alichokifanya wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alikabidhiwa barua akitakiwa aandike barua ya kujieleza na kuomba radhi. Wabunge wengine walitaka afukuzwe uanachama.


Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari akisema kambi hiyo imemwandikia barua Shibuda ikimtaka aombe radhi kwa maandishi na kama hatafanya hivyo, suala lake litapelekwa CC ili ione na kuamua kama hakufanya kosa.


Mgogoro wa Arusha uliibuka baada ya mwafaka baina ya madiwani hao kupatikana kwa Chadema kupewa unaibu meya wa Jiji, baada ya mgogoro uliokuwapo wa viongozi hao wa Chadema kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha ambaye ni wa CCM, Gaudence Lyimo.


Tume hiyo iliundwa kuchunguza namna mwafaka huo ulivyofikiwa, baada ya kuibuka malalamiko kwa baadhi ya viongozi wa Chadema akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa madiwani wenzake wamekisaliti chama kukubaliana na CCM kumtambua Lyimo.


Chadema ilimkataa kwa madai kuwa uchaguzi haukufuata utaratibu na misingi ya haki.


Pamoja na madai ya Lema ya usaliti kutokana na mwafaka kutokuwa na baraka za viongozi wa juu wa chama, madiwani hao waliendelea kudai kuwa uamuzi wa kumkubali Lyimo ulizingatia maslahi ya wananchi wa kata zao na Jiji la Arusha na si vyama.

0 comments

Post a Comment