Wajumbe wa mkutano wa CHADEMA, washabiki na wanachama wakiwa wamemzonga Nape kwa shauku |
Pia morali wa viongozi, watumishi, wanachama na wakereketwa wa CCM imekuwa juu sambamba na mwitikio wa wanachama na wananchi katika mikutano ya hadhara iliyofanywa na viongozi wa CCM katika mikoa mbalimbali.
Akizungumza jana na gazeti hili, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, utendaji wa sekretarieti hiyo katika miezi hii mitatu, umepata mafanikio na changamoto ambazo hata hivyo zinalenga kufanikisha kazi ya kukijenga chama. Sekretarieti hiyo iliundwa Aprili 12 mjini Dodoma.
“Wenyewe mlishuhudia idadi kubwa ya wanachama na wananchi waliojitokeza katika mkesha wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa TANU tarehe 7-7-1954 na katika maadhimisho yake pale Lumumba,” alisema Nape.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni katika mifumo ya kiutendaji ndani ya idara zote za CCM kuzungumza na kuonana vizuri bila mwingiliano.
Kuhusu changamoto, Nape alisema ni pamoja na juhudi zinazofanywa na watu wasioitakia mema CCM wakiwamo baadhi ya wanasiasa kutumiwa kwa lengo la kukatisha tamaa juhudi za kufanya mabadiliko ndani ya chama.
“Pia baadhi ya vyombo vya habari kutoa taarifa za kupika, ambazo zimeshaanza kutekelezwa na nyingine za kuwalisha baadhi ya viongozi, kwa lengo la kukidhi matakwa na maslahi yao, yakiwamo ya kugombanisha viongozi, wanachama na umma kwa jumla,” alisema.
“Hata hivyo, juhudi hizo hazitukatishi tamaa na kutuvunja moyo kuendelea kwetu kupambana ili kufanikisha lengo la kuboresha chama chetu na kusimamia utekelezaji wa uamuzi ambao ulifanywa na vikao vya juu vya CCM Aprili,” alisema bila kufafanua.
Aprili, CCM ilitoa siku 90 kwa viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi ili wajivue gamba kwa kuachia nyadhifa zao ndani ya CCM, vinginevyo wavuliwe nafasi hizo.
Nape alitoa mwito kwa wanachama, wakereketwa na wananchi kwa jumla, kupuuza njama na uzushi unaokusudiwa kufanywa na baadhi ya watu kwa lengo la kuchafua dhamira safi ya chama na Serikali zake kuendeleza mapambano dhidi ya umasikini na kuleta maendeleo nchini.
0 comments