IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk. Valentino Mokiwa na Askofu mpya wa Kanisa hilo aliyewekwa wakfu hivi karibuni, Stanley Hotay wamesema wanasubiri kukamatwa kwani taarifa za kutakiwa kukamatwa wamezipata kupitia vyombo vya habari.
Askofu Mokiwa alisema hajamkosea mtu hadi kutakiwa kukamatwa na hivyo anasuburi polisi wamkamate: "Mimi nipo kwenye kikao muda huu, bado hawajanikamata nawasubiri waje, mimi naamini sijamkosea mtu."
Mapema jana asubuhi, kiongozi mmoja wa juu wa kanisa hilo, alisema kuwa maaskofu hao walikuwa njiani wakielekea Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kujisalimisha.Hata hivyo, baadaye ilieleza kuwa walibadili uamuzi huo na kurejea katika chumba cha mkutano wa viongozi unaoendelea hapa Arusha.
Polisi mkoani Arusha jana walishindwa kumkamata Askofu Mokiwa na Askofu Hotay kwa maelezo kuwa bado hawajapata hati ya Mahakama ya kuwakamata.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alisema licha ya maaskofu hao kuwapo Arusha, walikuwa hawana mpango wowote wa kuwakamata kwani hawana hati ya Mahakama ya kuwaamuru kufanya hivyo (arrest warrant)
"Hatuwezi kuwakamata tu bila 'arrest warrant' nikipata tutawakamata," alisema Mpwapwa.
Juzi, Jaji Kakusulo Sambo alitoa amri ya kukamatwa, Askofu Mokiwa na Hotay kwa tuhuma za kudharau amri ya Mahakama ambayo ilitolewa Ijumaa wiki iliyopita, ambayo ilizuia kanisa hilo kumsimika Askofu Hotay Jumapili.
Akisoma maamuzi hayo mbele ya mamia ya waumini wa kanisa hilo, Jaji Sambo alisema haikuhitaji mtu kuwa na elimu ya shahada kutambua kuwa walichokifanya maaskofu hao ni kuvunja na kudharau amri halali ya Mahakama Kuu.
"Madai ya awali yaliyofikishwa mahakamani kuna watu, wanapinga Hotay kusimikwa kuwa Askofu kutokana na taratibu za kanisa lao kukiukwa, sasa kumsimika kwa kueleza kuwa kasimikwa kama Askofu wa Anglikana Tanzania na siyo Askofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ni kuingilia mwenendo wa kesi kwani kinachopingwa ni Uaskofu wake," alisema Jaji Sambo.
Alifafanua kuwa vielelezo vilivyofikishwa Mahakamani vinatoka, Shule ya Sekondari ya Ilboru iliyopo Arusha, ambayo Hotay alijiunga kidato cha kwanza mwaka 1984 vikionyesha kuwa aliandikishwa kuwa alizaliwa mwaka 1972 tofauti na cheti cha kuzaliwa kilichotolewa Februari mwaka jana.
Jaji Sambo alisema inasikitisha viongozi wa dini kuanza kuvunja sheria za nchi jambo ambalo likiachiwa nchi itakuwa mahala pabaya.
Tamko la Katibu wa Anglikana
Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji Dk Dickson Chilongani amepinga vikali madai kuwa kanisa hilo liliidharau Mahakama na kufanya ibada ya kumsimika Askofu Hotay.
Dk. Chilongani alisema kuwa kilichotokea ni mgongano wa mawazo katika kuelewa namna kumsimika Askofu na kumweka wakfu.Chilongani alisema kuwa kilichofanyika Arusha ni kumweka wakfu na kumwingiza katika daraja la Uaskofu Hotay lakini si kumtawaza kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
“Siwezi kupingana na Mahakama maana wao ndiyo waliotoa amri hiyo, lakini ninachoweza kusema ni kwamba tumeshindwa kuelewana kati yao na sisi maana tuliheshimu amri yao na sisi tukamweka wakfu wa kumwingiza katika daraja la Uaskofu siyo kumpa Dayosisi,” alisema Chilongani.
Hata hivyo, Chilongani alisema hapingi uamuzi wa Mahakama wa kumkamata kiongozi wake huyo lakini akasisitiza kuwa hakuwa amevunja sheria yoyote, bali pingamizi liliwachanganya kwani lilielekeza kutomtambua Hotay katika Dayosisi ya Mount Kilimanjaro na si katika nafasi ya Uaskofu.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa kanisa hata kama waumini wa Arusha watatokea kumkataa Hotay kuwa Askofu wao, bado kiongozi huyo anaweza kupangiwa nafasi nyingine katika Jimbo na akabaki na daraja lake la uaskofu.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mokiwa: Nasubiri wanikamate
0 comments