Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Safari ya wanafunzi UDSM yaishia mikononi mwa polisi Dom

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WANAFUNZI 50 wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) juzi wakiwa mjini Dodoma waliwekwa chini ya ulinzi mkali na Jeshi la Polisi  kwa muda wa saa nane ili wasihudhulie kongamano la Katiba lililokuwa lifanyike jana, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Kwa mujibu wa wanafunzi hao, Polisi waliwazuia kuhudhuria kongamano hilo kutokana na sababu za  kiintelijensia, huku likiwatuhumu kuwa lengo lao lilikuwa si kufanya kongamano, bali kupandikiza chuki kwa wanafunzi wa Udom dhidi ya serikali.

Akizungumza na katika ofisi za gazeti hili Tabata relini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Umoja wa wanafunzi hao wanaosoma Sayansi ya Siasa na Utawala (Dupsa), Godbless Nyongole  alisema kwa kitendo hicho kilisababisha wanyimwe haki yao ya kikatiba.

“Tulikuwa na barua ya ruhusa kutoka chuoni kwetu, pia uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ulikuwa ukijua kuwa tunakwenda ila inashangaza tulivyozuiwa na polisi huku tukielezwa kuwa lengo letu halikuwa kongamano,” alisema
Nyongole,Aliongeza, “Tumenyimwa haki yetu ya msingi kwa mujibu wa kifungu cha  17, 18 na 20 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”.

Alisema kuwa kongamano hilo lilikuwa lifanyike juzi na kwamba mada zilizokuwa zijadiliwe ni mbili ambazo ni,  Katiba mpya,  mtazamo na nafasi ya vijana pamoja na wajibu na nafasi ya kijana katika maendeleo ya nchi na Bara la Afrika.

Akisimulia sakata hilo, Nyongole alisema kuwa waliondoka jijini Dar es Salaam Ijumaa saa 5 asubuhi, lakini walipofika maeneo ya Chamwino mjini Dodoma basi lao walilokuwa wamepanda lilisimamishwa na askari wa usalama barabarani.

“Ilikuwa saa 12:45 jioni, walitusimamisha na kutupeleka katika Kituo cha Polisi cha Chamwino, wakati wanatupeleka nyuma ya basi letu kulikuwa na gari lingine la polisi likitufuatilia,” alisema Nyongole.

Alisema kuwa baada ya kufika kituoni  hapo walikuta kundi kubwa la askari ambao waliwaweka chini ya ulinzi ambapo baadaye  waliwaleleza kuwa wanataka kuzungumza na viongozi wa msafara huo ili wachukue maelezo yao.

Alisema kuwa baada ya hatua hiyo kilifanyika kikao kilichodumu kwa saa saba baina yao na baadhi ya viongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Dodoma pamoja na  Kamanda wa Polisi mkoani humo.

“Walituhoji wote na kutuuliza makabila yetu, dini, umri, namba zetu za usajili za chuo na sehemu tunapoishi, kisha wakatueleza kuwa hawawezi kuturuhusu kufika Chuo Kikuu cha Dodoma kwa sababu za Kiintelejensia,” alisema Nyongole.

Alidai kuwa katika kikao hicho kilichoanza saa 2 usiku na kumalizika saa 8 usiku bila muafaka wowote, RPC aliwataka waondoke mara moja mkoani humo na kurejea Dar es Salaam.“Ilibidi tuhoji hizo sababu za Kiintelijensia ni zipi, maana tulizuiwa kufanya kongamano wakati ni haki yetu, eti wakasema lazima tuwe na kibali, sisi tukahoji kibali cha nini wakati vyuo vyenyewe ndio vimekubaliana,” alihoji Nyongole.

Alisema kuwa polisi waliwaeleza kuwa wanafunzi wa UDSM wamekuwa tishio kwa serikali na kwamba lengo lao la kwenda UDom ni kupandikiza mbegu za chuki kwa wanafunzi wa chuo hicho dhidi ya serikali.

Alisema kuwa baada ya mabishano ya muda mrefu waliondoka kituoni hapo kwa shingo upande huku usiku wa kuamkia jana (saa 10 alfajiri) kurejea jijini Dar es Salaam ambapo walifika saa 7 mchana.Kamada wa Polisi mkoani humo alipotafutwa na gazeti hili kwa njia ya simu kuzungumzia sakata hilo hakupatikana ila dereva wake alisema kuwa Kamanda alikuwa katika kikao.

0 comments

Post a Comment