Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Rais Kikwete akubali nyongeza za mishahara

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MVUTANO uliodumu kwa takriban mwaka mmoja baina ya serikali na Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi (Tucta) unaelekea kumalizika, baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza hadharani kuwa  serikali imekubali ombi la wafanyakazi la kutaka kupandishwa mishahara na kupunguziwa kodi.

Mapema mwaka jana Shirikisho la Tucta liliingia katika mvutano na Serikali likitaka  kuongezwa mishahara na kupunguza kodi kutoka  asilimia 15 hadi asilimia tisa.

Katika kipindi hicho Serikali ilikataa kupunguza kwa kiwango hicho na kutaka ipunguwe hadi asilimia 13 hali iliyosababisha wafanyakazi kutishia kugoma.Akizungumza katika maadhimisho ya sherehe za siku ya wafanyakazi duniani, Mei Mosi jana, Rais Kikwete alisema kuwa dhamira ya Serikali siku zote ni kuona wafanyakazi wanalipwa mishahara inayokidhi mahitaji ya kimaisha.
Alisema Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imejitahidi kupandisha mishahara kutoka kima cha chini cha Sh 65, 000 hadi kufikia Sh 135,000 na jitihada hizo zimekuwa zikifanyika pia katika kuongeza mishahara ya wafanyakazi kisekta.
"Tatizo la ajira nchini na mishahara duni kwa wafanyakazi linaweza kumalizika kwa kuongeza jitihada za kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje, kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma tofauti na ilivyo sasa,"alisema.
Alisema ufinyu wa mapato ya Serikali na kasi ndogo ya uwekezaji iliyopo nchini katika sekta mbalimbali, umekuwa ukikwamisha jitihada za Serikali kufikia malengo hayo na hivyo kutokidhi matarajio ya wafanyakazi na vijana kwa kuwapatia ajira.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kuwa  kumekuwa na jitihada za kuboresha mazingira ya kuvutia uwekezaji nchini na kutolea mfano wa miradi 3,881 yenye thamani ya dola 27 bilioni za Marekani  ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na kuwezesha kuzalisha zaidi ya ajira 444,343.
"Zoezi la uwekezaji lilidorora zaidi mwaka jana pale dunia ilipokumbwa na mdororo wa uchumi na hivyo kuwafanya baadhi ya wawekezaji waliokwisha onyesha nia ya kuwekeza nchini kushindwa kufanya hivyo."
Alitolea mfano wa kiwanda cha mabati kilichokuwa kijengwe mkoani Mtwara kwa thamani ya zaidi ya Sh 3.5 bilioni kukwama kutokana na mtikisiko wa kiuchumi duniani  na hivyo kukwamisha fursa nyingi kwa Watanzania lakini pia Serikali kushindwa kupata mapato yake.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete alisema wafanyakazi watapata fursa ya kuchangia mjadala wa mabadiliko ya katiba kama yalivyo makundi mengine katika jamii.
“Maombi yenu nimeyasikia mtashiriki katika mjadala huo muda utakapowadia, maoni ya kila Mtanzania yatasikilizwa siyo kama kundi fulani hivi linalotaka mawazo yao tu ndiyo yasikilizwe na wengine wakizungumza wao wanachukia, hatuwezi kwenda hivyo,”alisema.
Wingi wa wageni umekuwa ukiwapa kazi Mara baada ya kufika Samunge, raia hao wa kigeni walikaguliwa hati zao za kusafiria na maafisa uhamiaji,Waajiri wakandamizaji Kuhusu waajiri Rais kikwete alimtaka Waziri wa Kazi na Ajira, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Kamishina wa Kazi, kusimamia vema sheria za kazi kuwabana waajiri wanaowakandamiza wafanyakazi na wasioheshimu sheria za kazi na kutaka wanaokiuka wawachukulie hatua za kisheria.
Pia Kikwete amewakata wahusika hao kuwabana maafisa wa kazi wanaotoa upendeleo kwa waajiri, ili kupindisha sheria  ikiwa ni pamoja na kuwahamisha vituo vya kazi maafisa wa kazi waliokaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu.
Kuhusu ajira kwa wageni, Rais Kikwete aliiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi na Wizara ya Kazi na Ajira  kuhakikisha wanashughulikia tatizo hilo na kudai kuwa kitendo cha kuwanyima ajira wazalendo na kuwapa wageni ni makosa.
Kauli ya Tucta
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu katibu mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya aliendelea kusisitiza kuwa Serikali bado inao uwezo wa kuwalipa mishahara wafanyakazi wake inayokidhi mahitaji ya kimaisha.

Alisema ikiwa Serikali itaacha matumizi yasiyokuwa ya lazima, kama vile kupunguza misururu ya misafara ya viongozi, ununuzi wa magari ya kifahari yasiyo ya lazima, kulipa posho kubwa katika semina na kupunguza misamaha ya kodi iliyopo kutawezesha mishahara ya wafanyakazi kupanda hadi kufikia kima cha chini cha Sh 350,000 kwa mwezi badala ya Sh 135,000.
Mgaya alisema Tucta isingependa kuona kila mwaka ikiendelea kuzungumzia matatizo yale yale, badala yake inapenda kuisikia Serikali ikichukua hatua katika kutatua changamoto zinazowakabili ili miaka inayofuata kujadili mambo mengine.
Sherehe hizo zilipandwa na maandamano ya wafanyakazi na magari yakionyesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wafanyakazi.
Mvutano wa Serikali na Tucta
Dalili njema na kurejea kwa uhusiano baina ya Tucta na Serikali zilianza April 21, mwaka huu pale Rais Kikwete alipokutana na viongozi wa wafanyakazi Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mvutano huo uliodumu kwa takriban mwaka mmoja kiasi cha Tucta kutoa tamko kwamba lingewashawishi wafanyakazi kote nchini kutompigia kura mgombea yeyote asiyejali maslahi yao katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.
Wakati mvutano huo ukiendelea Mei 4, 2010 Kikwete alilihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuyakataa hadharani mapendelezo ya Tucta ya kutaka kima cha chini cha mshahara cha Sh 350,000/- .
Kikwete alisema hawezi kuwadanganya wafanyakazi kuwa atawaongeza mishahara wanayotaka na kwamba alikuwa tayari kuzikosa kura zao.

Hata hivyo Agosti 21, 2010 Kikwete akiwa mgombea wa urais kupitia CCM alitamka wakati wa uzinduzi wa kampeni za kitaifa za chama hicho kuwa “mishahara ya wafanyakazi ilikuwa imepanda, ingawa si kwa kiwango kilichokuwa kikitakiwa na Tucta”.
Licha ya hatua hiyo, Tucta kupitia kwa Mgaya walibeza kauli hiyo ya Rais wakisema kuwa tangazo hilo lilikuwa limechelewa, huku wakisisitiza msimamo wao wa kutompa kura mgombea yeyote wa kiti cha urais asiyejali masilahi yao au yule aliyezikataa kura zao.
Singida
Mkoani Singida, katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Serikali iliwaambia wafanyakazi kuwa imeshalipa watumishi wake kiasi cha Sh 971 milioni kwa madai mbalimbali kati ya mwaka juzi na mwaka jana.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone wakati maadhimisho yaliyofanyika kimkoa Singida Mjini. Katika hotuba yake iliyosomwa na DC wa Singida, Pascal Mabiti alisema madai hayo ni ya likizo, uhamisho, kujikimu, matibabu, posho za kujikimu kwa walimu wapya, nauli, gharama za mizigo na wategemezi wao.
Habari imeandikwa na Venance George na Lilian Lucas, Morogoro, Elizabeth Ernest, Dar na Gasper Andrew, Singida.

0 comments

Post a Comment