Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Vurugu Ubungo, abiria wakaa saa nane kituoni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MAELFU ya abiria jana walikwama kuondoka  katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo (UBT) kwa saa zaidi ya nane baada ya madereva wa magari hayo kugoma wakishinikiza kushughulikiwa kwa madai yao.Wakati mgomo huo ulioanza saa 12.00 hadi saa 7.00  mchana ukiendelea, vurugu ziliibuka kituoni hapo ambapo magari kadhaa yaliharibiwa kwa kupigwa na mawe na kuvunjwa vioo kutokana na kile kilichodaiwa madereva wake walikiuka makubalino.
Madereva hao walijitokeza wakiwa na madai kadhaa na baadhi yake ni kutaka  wamiliki magari hayo kuwapatia mikataba ya ajira, kupinga kile walichodai uonevu unaofanywa na polisi wa usalama barabarani katikia mikoa ya Iringa na Mbeya na kutaka muda utoaji  leseni mpya uongezwe.
Magari yashambuliwaMagari yaliyoshambuliwa ni pamoja na Champion linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Dar es Salaam, Lupelo linalofanya safari zake Dar es Salam na Mbeya na Newforce Enterprises Ltd linalofanya safari zake Dar es Salaam na Mbeya.Gari hizo zilishambuliwa saa nne asubuhi ambapo jeshi la Polisi lilipotaka kutumia nguvu kulazimisha madereva kuondoa gari kituoni hapo.
Baada ya madereva wa magari hayo kulazimisha kutoka ndani, madereva wenzao waliyashambulia magari hayo kwa mawe, hivyo yalilazimika kusimama na kuegeshwa nje ya kituo.
Kufuatia hali hiyo Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Taifa, Mohamed Mpinga, Kamanda wa Kanda maalamu ya Dar es Salaam Sulemani Kova, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana na Mkurugenzi wa Uchumi wa Sumatra, Ahmad Kilima waliwasili kituoni hapo kutatufa utatuzi wa mgomo huo.
Viongozi hao walilazimika kufanya kikao cha ndani ambacho kilichukua takribani saa moja na kukubalina kwa kauli moja kuwa gari hizo zingeondoka na madai yao kufanyiwa kazi.
Hata hivyo wakiwa bado kwenye kikao hicho mamia ya abiria walifika kwenye mlango wa ukumbi na kuanza kuimba nyimbo za kudai haki zao huku wakitishia kuingia ndani iwapo maafisa hao wengechelewa kutoa suluhu.

“Tunataka haki zetu, tunataka haki zetu na kama mtachelewa tutaingia humo ndani ili kuja kudai haki zetu,”alisikika abiria mmoja akizungumza kwa sauti.Kauli hiyo iliwashitua maafisa waliokuwa ndani hivyo muda mfupi baadaye kikawasili kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) ambacho kilisambaratisha abiria hao kwa mkong’oto.
Uamuzi wa serikali
Ilipofika saa sita mchana kikao hicho kilikuwa ikimemalizia na maafisa kumuagiza katibu wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA), Salum Abdallah kuwashawishi madereva wenzake kuingia kwenye magari kuanza safari.

Kauli ya katibu huyo iliamsha hasira toka kwa madereva hao ambao walimshambulia kwa maneno na kuelezea dhamira yao ya kuendelea na mgomo.Kufuatia hatua hiyo Kamanda Kova aliwashauri maafisa waliokuwa ameongozana nao kwenda waliko madereva hao na kuwaeleza kila kitu walichofikia.
Kamanda Mpinga aliyesema kuwa Jeshi hilo limepokea malalamiko yanayowahusu na watayafanyia kazi. “Kwa upande wetu tumepokea malalamiko kuwa polisi wamekuwa wa Mikoa ya Iringa na Mbeya wamekuwa wakiwaonea na kupokea rushwa, madai haya yote tutayafanyia kazi,”alisema Mpinga.
Mpinga alifafanua kuwa pamoja na kushughulikia madai ya rushwa kwa askari hao pia Jeshi hilo litaongeza muda wa utoaji leseni kwa madereva kama wao walivyodai.Naye Mkurugenzi wa Uchumi wa Sumatra, Ahmad Kilima aliwataka waajiri kuhakikisha wanarekebisha kero ya mikataba  baina yao na madereva.
Mkurugenzi huyo alisisitiza madereva kuwa makini pindi wanapoingia mikataba na waajiri wao ili kukwepa udanganyifu.
Kwa upande wake Kamanda Kova alitoa pole kwa abiria na kudai kuanzai sasa watafanya kazi kwa ushirikiano na taasisi zote kuhakisha kero za madereva hao zinatekelezwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema serikali imepokea kilio cha madereva hao na kwamba mkuu wa Mkoa amekubali kukaa nao kesho kujadili kero zao na kuchukua hatua.
Rugimbana alifika katika kituo hicho kumwakilisha Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick aliwataka madereva hao kuendelea na safari huku akisema kuanzia sasa ofisi yake itashirikiana nao katika kuyashughulikia matatizo yao.
Mwenyekiti wa Uwamata,Yusuf Magamba alisema wamefikia makubaliano hayo kutokana na maafisa toka Serikalini kuwahakikishia kuwa kutakuwa na mkutano mwingine kesho.

Alisema kama yale watakayoyajadili katika kikao hicho hayatakuwa na mwelekeo wa kiutekelezaji wao watarudisha suala hilo kwa wananchama nao ndiyo watakaoamua cha kufanya.
Mmoja wa abiria  Juma Athumani ambaye alikuwa ana safari kwenda Kilimanjaro alisema kuwa madereva wana haki ya  kugoma lakini walitakiwa kutoa tarifa mapema kwa abiria kwa sababu wamesababisha usumbufu mkubwa.
“Mgomo wa madereva umetusababishia madhara makubwa kwanza wametuchelewesha tunapo kwenda pia siyo vizuri kufanya mgomo bila kutoa taarifa kwa abiria siyo jambo zuri kwa sababu abiria ndiyo chanzo chao cha mapato,” alisema Athumani.

0 comments

Post a Comment