Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Nape ashusha pumzi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo kinaanza vikao vyake vya kawaida mjini Dodoma, lakini ambavyo vimekuwa vikisubiriwa kwa hamu na wanachama wake pamoja na Watanzania, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema mageuzi ndani ya chama hicho ni mchakato endelevu.


Leo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, itaanza kikao cha siku mbili kwenye Makao Makuu ya Chama hicho (White House) Barabara ya Nyerere, Dodoma.


Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na Kamati Kuu ni hali ya siasa nchini na kufanya
maandalizi ya ajenda za kikao cha NEC itakayokutana Novemba 23 na 24 mwaka huu.


Pia Kamati Kuu itajadili masuala mengine mbalimbali ya ndani ya chama na jumuiya zake yakiwemo masuala ya utumishi.


Lakini akizungumza kwa simu na gazeti hili jana jioni kufafanua ajenda za kikao hicho na minong’ono kwamba kutakuwa na kufukuzana katika vikao hivyo, Nape alikataa kuthibitisha hoja hiyo.


“Mchakato wa mageuzi ndani ya CCM haufanyiki kwa siku moja, una mambo mengi, ni suala endelevu. Litachukua muda mrefu,” alifafanua Nape na kuongeza kuwa katika vikao hivyo, pamoja na mambo mengine, vitapitia na kutathimini utekelezaji wa mageuzi
yanayoendelea ndani ya chama hicho tawala baada ya kuwepo kwa maazimio 26 yaliyotolewa katika kikao cha NEC kilichokaa miezi minne iliyopita.


“Likitokea la kufukuzana wanachama, litakuwa ni sehemu tu, lakini hili la mageuzi, ni suala endelevu; kwa mfano tunataka kujenga chuo cha Ihemi, hadi sasa hata ujenzi haujaanza na ndio kwanza tumeanza michoro.


“Kuna suala la kuwapatia ujuzi watumishi wetu, huu wote ni mchakato unaoendelea. Nia yetu ni kujenga chama ambacho kitaweza kwenda na mageuzi ya sasa na kuendelea kuaminika kwa
wananchi, hivyo si suala la siku moja,” alisema Nape na kuongeza kuwa vyombo vya habari ndio vinazungumzia suala la kufukuzana.


Lakini wakati Nape akitoa ufafanuzi huo, kumekuwapo na minong’ono kuhusu majaliwa ya baadhi ya makada kutokana na joto kali miongoni mwa makada wa chama hicho na hasa baada ya kuibuka kwa hoja zinazokinzana kuhusu falsafa iliyoanzishwa na Mwenyekiti Rais Kikwete ya kujivua gamba.


Inadaiwa kuwa baadhi ya wajumbe katika Sekretarieti ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu Wilson Mukama, walipotosha dhana hiyo ya kujivua gamba ambayo iliasisiwa na Rais Kikwete wakati wa maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 34, Februari mwaka huu.


Nape na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, John Chiligati ndio wanaotuhumiwa kupotosha dhana hiyo kwa madai ya kuwahusisha moja kwa moja baadhi ya makada wa chama hicho.


Katika moja ya maazimio ya NEC iliyopita, ilikuwa suala la wanachama wenye kashfa mbalimbali zikiwemo za ufisadi kupima wenyewe na kujitathimini kabla ya chama hicho kuchukua hatua dhidi yao.


Ingawa hakuna rekodi rasmi za watuhumiwa hao kutajwa, Nape aliwahi kukaririwa kuwataja
wanachama watatu, Rostam Aziz, Edward Lowassa na Andrew Chenge kama watu wanaopaswa
kujivua magamba.


Hata hivyo, ndani ya miezi minne tangu kikao cha mwisho kilichotoa azimio la watu hao kujitathimini na kuchukua hatua wenyewe, mmoja wa makada wake maarufu, Rostam alijiuzulu nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama hicho akisema anafanya hivyo baada ya kuchoshwa na siasa uchwara.


Rostam aliyekuwa Mbunge wa Igunga, na aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Mweka Hazina wa CCM Taifa, alikuwa Mjumbe wa NEC kupitia Mkoa wa Tabora.


Alijiuzulu Julai 14, mwaka huu, na tangu wakati huo, macho na masikio yamekuwa yakielekezwa kwa kina Lowassa na Chenge.


Lakini kwa nyakati tofauti, wawili hao wamekaririwa wakitoa kauli tofauti. Chenge aliwahi kukaririwa akisema kwamba hajui kama anatakiwa kujivua gamba, wakati Lowassa aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wake nao, kwamba suala la kujivua gamba na kashfa ya Richmond, atayazungumzia muda ukifika.


Kwa hiyo, vikao vinavyoanza leo vinasubiriwa kwa hamu matokeo yake kwa nia ya kujua kama dhana ya kujivua gamba itakwenda na wawili hao ambao wamekuwa wakitajwa kwa muda mrefu, au chama hicho tawala kitaamua kusonga mbele na mageuzi yake bila kuvuana
magamba.


Aidha, tangu juzi na jana, Kamati ya Maadili ya chama hicho ilikuwa inakutana chini ya uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, na juzi iliwahoji
baadhi ya viongozi wa UVCCM kutokana na mwenendo wa kisiasa katika jumuiya hiyo.


Viongozi hao waliohojiwa wanadaiwa kutoa kauli mbalimbali za kudhoofisha utendaji wa chama hicho na zinazoashiria mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala.


Aidha, baadhi ya viongozi wa juu wa UVCCM katika siku za karibuni, wamejikuta katika mgogoro kati yao wenyewe au na viongozi wa mikoani.


Katika hatua nyingine, Nape amesema baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa, Novemba 25 hadi 27 kutafanyika semina ya Watendaji wa chama ngazi ya Kitaifa hadi Wilaya.


“Katika semina hiyo watakaoshiriki ni Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya
Taifa, Sekretarieti za Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (UWT, UVCCM na WAZAZI), Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya zote nchini,” alisema Nape jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.


Wakati huo huo, Rais Kikwete juzi alikutana na kuzungumza na wabunge wa CCM na kupata nao
chakula cha usiku katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper mjini Dodoma.


Kwa mujibu wa Ikulu, Rais Kikwete aliwapa changamoto wabunge hao wa CCM waende kwa wapiga kura wao na kuwaelimisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya uliopitishwa Jumamosi bungeni.


Aliwasisitizia wabunge hao umuhimu wa kupeleka elimu hiyo ya mchakato wa kupata Katiba
mpya kwani hivi karibuni kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa nini kinachoendelea, na kusema kuwa wakiwa wabunge wa chama tawala ni wajibu wao kuelimisha umma kwamba kanuni na sheria zote zimefuatwa katika kupitisha muswada huo ambao umesomwa
kwa mara ya pili, baada ya kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa sheria.


Rais Kikwete aliwakumbusha wabunge hao kwamba mchakato huo si jambo geni na kwamba ndio uliofuatwa na marais wote kutoka wa awamu ya kwanza hadi ya tatu, akisisitiza kwamba ni muhimu wananchi wote wakaelewa hilo, ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya watu wachache wanaotaka kupotosha umma kwamba hatua hiyo ni batili wakati sio kweli, ikizingatiwa kwamba kila lililo katika Katiba ya sasa limezingatiwa.


Pia aliwasihi Watanzania kujitokeza kutoa maoni yao ya ni Katiba gani wanayoitaka pindi muda wa kufanya hivyo utapowadia, na wasikubali kughilibiwa na wachache waliopania kupindisha ukweli.

0 comments

Post a Comment