Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Wabunge CCM walalama mkutano wao na Kikwete

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
BAADHI ya wabunge wa CCM wamelalamikia mkutano ulioitishwa baina yao na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kwamba haukuwa na tija tofauti na matarajio makubwa waliyokuwa nayo.


Rais Kikwete, juzi usiku alikutana na wabunge wa chama chake katika Ukumbi wa St. Gasper nje kidogo ya Mji wa Dodoma lakini habari zilizopatikana jana zilisema mkutano huo uligeuka kuwa wa “chakula cha jioni.”


“Mkutano wenyewe haukuwa na tija, kwanza tulisubiri sana hadi watu wakaanza kukata tamaa, lakini hata Rais alipofika hakukuwa na mkutano kama tulivyoambiwa na badala yake tuliambiwa ni dinner tu (chakula cha usiku) halafu mazungumzo ni siku nyingine,” alisema mmoja wa wabunge aliyehudhuria hafla hiyo.


Mbunge mwingine alisema: “Wengine tulikuwa tumejipanga kumuomba Rais achukue hatua kuhusu mambo yanavyokwenda ndivyo sivyo, serikalini na kwenye chama, lakini ndiyo hivyo, haikuwezekana, maana tuliishia kula na baadaye kutawanyika.”


Usiku huo, Rais Kikwete alitoa hotuba fupi yenye sura ya salaam kwa wabunge hao huku akiwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya bungeni na kwa ujasiri wao wa kutokuwa wanyonge kwenye mijadala bungeni.


Kikwete alinukuliwa na vyanzo vyetu akiwapongeza wabunge wa CCM kwa jinsi walivyoutetea Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 pamoja taarifa za Kamati mbili za Bunge zilizowasilishwa kuhusu sekta ya gesi na ile ya Kamati Teule.


Mbunge mwingine aliyezungumza na gazeti hili alisema: “Sisi ndiyo tulimwomba Rais aje kuzungumza nasi, lakini hatujui ni nini kilichotokea, tumeahidiwa kwamba huenda akaja kusema na sisi tutakapokutana mwezi Februari mwakani.”


Kwa mujibu wa mbunge huyo, walikuwa wamejiandaa kuzungumzia matatizo ya nchi hasa kuyumba kwa uchumi, hali ngumu ya maisha na udhaifu katika utendaji wa Serikali ambao umekuwa ukiwaweka katika wakati mgumu kuwakabili wapinzani bungeni.


“Mambo hayaendi kabisa, watendaji serikalini ni kama hawaoni, sasa tulidhani kwamba fursa hii ilikuwa ni ya kumshauri Rais aweze kuchukua hatua zaidi, vinginevyo tutakwama, hatuna matumaini kadri siku zinavyokwenda,” alisema mbunge huyo.


Jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya wabunge wa CCM, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na katibu wa kamati hiyo, Jenister Mhagama (Mbunge wa Peramiho), kuzungumzia mkutano huo hazikufanikiwa.


Taarifa rasmi kutoka Ikulu ilisema Rais alizungumza na wabunge wa CCM kisha kupata nao chakula cha usiku katika ukumbi wa St. Gasper.


Taarifa hiyo ilisema Kikwete aliwapa changamoto wabunge hao kwenda kwa wapiga kura wao kuwaelimisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.
Taarifa hiyo imemnukuu Mwenyekiti huyo wa CCM akiwasisitizia wabunge hao umuhimu wa kutoa elimu kuhusu suala hilo, kutokana na kuwapo kwa upotoshaji unaofanywa kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge.


Mawazo ya wabunge


Baadhi ya wabunge walisema kutoruhusiwa kwao juzi kuzungumza na Rais kunaweza kuwa kumechochewa na kikao cha wabunge wa CCM kilichokutana Alhamisi usiku, Novemba 17, mwaka huu chini ya Pinda.


Katika kikao hicho, wabunge hao waliripotiwa kugeuka mbogo hasa baada ya kupewa taarifa kuhusu kile kilichokuwemo kwenye taarifa za kamati mbili za Bunge kwamba kulikuwa na madudu ambayo yanaichafua Serikali.


Kutokana na hali hiyo, wabunge wanadaiwa kukataa kupokea maelezo ya kina kuhusu taarifa hizo na kumwambia Pinda kwamba taarifa hizo zisomwe kama zilivyo bungeni ili na wao wapate fursa ya kuchangia ndani ya ukumbi wa Bunge kama ilivyo kwa wapinzani.


“Tulikataa maana tungekesha, halafu ni kama walitaka kutupunguza nguvu na sisi tukawa na msimamo kwa kutaka zisomwe kama zilivyo, tumechoka kubebana maana hawa wenzetu serikalini ni kama hawasikii, tunabebana mpaka lini!,” alisema mbunge mwingine ambaye kama wenzake, hakutaka kutajwa gazetini.


Katika siku za karibuni, wabunge wa CCM wameripotiwa kuwa wakali hasa wakieleza kutoridhishwa na utendaji wa baadhi ya mawaziri na watendaji wengine serikalini.


Wakati wa Bunge la Bajeti, walikuwa ni wabunge wa CCM ambao walikuwa mwiba kwa mawaziri wengi kiasi cha kufikia hatua ya kukwamisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, hivyo Serikali kuamua kuiondoa kwenda kujipanga upya.


Pia wabunge hao wakiwa kwenye kikao cha kamati ya chama, walikataa kusikiliza maelezo ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wakisema lazima iwasilishwe bungeni ili wachangie kama wabunge wengine.


Katika Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa Ijumaa iliyopita, wabunge hao wa CCM waliwasilisha majedwali ya marekebisho ya muswada huo kwa wingi kiasi cha kusababisha kuitishwa kwa kikao cha kamati yao kuwasihi kuondoa baadhi ya hoja zao.


Imedaiwa kwamba hatua ya kupitiwa kwa majedwali hayo katika kikao hicho cha chama, ilitokana na wabunge hao wa CCM kuyawasilisha zaidi ya 40 huku mengine yakiwa na mapendekezo ya marekebisho ambayo yanadaiwa kuwa yalibeba ajenda zenye sura ya upinzani.


Ni kutokana na hali hiyo, baadhi yao wanadhani kwamba huenda hilo likawa moja ya mambo yaliyowakwaza kuzungumza na Rais.


Kuwasili kwa Rais
Rais Kikwete aliwasili Dodoma juzi, jioni kwa lengo la kuongoza vikao vya CCM ambavyo ni Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.


Taarifa iliyotolewa jana mjini Dodoma na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye inaonyesha kuwa vikao hivyo vinaanza leo hado Novemba 27, mwaka huu.


Nape katika taarifa hiyo alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana leo na kesho na kufuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitakachofanyika Novemba 23 na 24, wakati Novemba 25 hadi 27, kutakuwa na semina ya watendaji wa CCM ngazi ya taifa hadi wilaya.


Washiriki wa semina hiyo watakuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Sekretarieti za Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi ambazo ni UWT, UVCCM na WAZAZI, makatibu wa CCM wa mikoa na Wilaya zote nchini.

0 comments

Post a Comment