Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bunge lafichua mpango hujuma sekta ya gesi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini,January Makamba
KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini imefichua njama nyingine zinazoandaliwa ili kuikosesha Serikali gawio linalotokana na faida ya biashara ya gesi inayofanywa na Kampuni ya Songas.


Kamati hiyo kupitia Kamati yake ndogo imebaini kwamba kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT), ilifanya udanganyifu unaofikia Dola za Marekani 64milioni sawa na Sh110 bilioni na kuilaumu Serikali kwa kukaa kimya kuhusu hali hiyo.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, January Makamba alifichua mpango huo wa hujuma bungeni juzi, wakati akihitimisha hoja ya taarifa ya Kamati yake kuhusu hali ilivyo katika sekta ndogo ya gesi nchini ambapo maazimio 26 yaliridhiwa na Bunge na kuwasilishwa serikalini kwa utekelezaji.


January aliliambia Bunge kuwa kuna njama za kuikosesha Serikali gawio kutokana na faida inayotarajiwa kuanza kupatikana kuanzia mwaka ujao, baada ya kampuni ya Songas kuanza utekelezaji wa mpango wa kupanua bomba la gesi kwa kutumia mkopo kutoka sekta binafsi.


“Serikali inamiliki hisa katika biashara hii ya gesi kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), asilimia 29 na nyingine kupitia Tanesco tisa na asilimia zinazobaki (62) ni za Songas, sasa hawa Songas wanataka kukopa fedha ili kupanua bomba la gesi bila kuwashirikisha wabia ambao kimsingi ni Serikali!” alisema.


Alisema ili kutekeleza mpango huo utakaowezesha bomba hilo kusafirisha futi za gesi 35 milioni za ujazo, Songas wamekopa katika taasisi binafsi kiasi cha Dola za Marekani 120 milioni ambazo kimsingi zitaathiri hisa za Serikali.


“Kitaalamu hisa za Serikali zitaathirika, zitapungua na kwa mkataba uliopo ni kwamba wakati gawio la faida litakapoanza kutolewa, wa kwanza kupata ni yule mwenye hisa nyingi. Ina maana kwamba Serikali yetu haitaambulia kitu katika biashara hii,” alisema.


Tangu kuanza kwa biashara ya gesi mwaka 2004, mradi huo umekuwa ukiendeshwa kwa hasara na kwa mujibu wa hesabu zake, huenda ukaanza kuzalisha faida mwakani au mwaka 2013.


Katika mpango wa awali, Serikali ilipaswa kunufaika na hisa zake kutokana na biashara hiyo ya gesi lakini January anasema haitaweza kupata gawio ikiwa Songas wataruhusiwa kuendelea na mpango wao wa upanuzi ambao kimsingi haujawashirikisha wabia wake ambao ni Serikali.


“Tulipowauliza Tanesco na TPDC walisema hawajui jambo hilo kwa sababu hawakushirikishwa, lakini la ajabu kabisa ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini nayo haijui. Nadhani hapa kuna tatizo la msingi, hebu wenzetu wafuatilie mambo haya ili tusije tukapoteza uhalali wa hata kuwa wabia katika mradi muhimu namna hii na kuna kila dalili kwamba katika mwaka wa kwanza wa gawio tunaweza tusipate kitu kabisa,” alisema January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM).


Alisema katika mradi wa sasa, Serikali imewekeza kiasi cha Dola za Marekani 216 milioni (sawa na Sh388.8 bilioni kwa viwango vya sasa vya kubadilisha fedha) na kwamba fedha hizo zilizotokana na mkopo kutokana na Benki ya Dunia na taasisi nyingine za fedha duniani hivyo, zilipaswa kuliletea faida Taifa na si vinginevyo.


Uchunguzi wa Kamati


Akisoma taarifa hiyo, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Jumanne Zedi alisema ukaguzi uliofanywa na TPDC ulibaini kuwa, PAT walijirudishia fedha za gharama walizotumia kuzalisha gesi kati ya mwaka 2004 na 2009.


Kadhalika, kamati hiyo ilibaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa na TPDC kwa ajili ya kusomesha wataalamu wa shirika hilo na wale wa wizara katika sekta ya nishati hiyo.


Kamati ya Nishati na Madini ilipewa kibali cha kufanya uchunguzi huo na Spika wa Bunge, Anne Makinda baada ya kueleza nia yake katika taarifa kuhusu maoni yake kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Julai 15, mwaka huu.

0 comments

Post a Comment