Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO , HABARI ZA MICHEZO - Yanga: Hakuna kulala sasa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamesema hawana muda wa kupoteza kwa sasa na ndiyo maana imewapa mapumziko ya siku tatu, wachezaji wake na baada ya
hapo mazoezi yataanza kama kawaida.


Mbali na wachezaji hao, pia Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe ameondoka nchini jana kwenda kwao Uganda kwa mapumziko.


Lakini kwa taarifa ambazo zilipatikana juzi mchana, zilieleza kwamba Timbe hakuwa na mpango wa kuondoka lakini kuna mmoja wa wanafamilia yake amepata ajali kwa kugonga na gari.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo Louis Sendeu, alisema baada ya mechi zao za ligi kusimama kupisha maandalizi ya timu ya taifa 'Taifa Stars', wametoa likizo ya siku tatu kwa timu hiyo.


"Tumewapa mapumziko wa siku tatu na baada ya hapo mazoezi kama kawaida, hatuna muda wa kupoteza tutahakikisha tunakuwa na mazoezi ya kutosha, ili kurudi katika nafasi yetu kwenye msimamo wa ligi," alisema Sendeu.


Akizungumzia ushindi walioupata juzi wa mabao 5-0, dhidi ya Coastal Union ya Tanga alisema ni ushindi wa kawaida na wameupokea vizuri, kwani kwa timu kama yao huo si ushindi wa kuushangaa.


Alipoulizwa kuhusu kuondoka kwa Timbe, alisema ni kweli alitarajiwa kuondoka jana baada ya kupewa mapumziko ya siku tatu.


Alisema ameaga anaondoka kwenda kuiona familia yake, lakini kama ina matatizo au vinginevyo yeye (Sendeu) hafahamu hilo.


Naye Timbe, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa juzi, alisema timu yake haijawahi kucheza katika kiwango kama kile na endapo itafanya hivyo, hakuna shaka itatetea ubingwa wao.


"Nimefurahishwa kwa jinsi timu ilivyocheza, hasa kwa upande wa washambuliaji lakini mabeki bado kuna matatizo ambayo nitayafanyia kazi," alisema Timbe.


Kwa ushindi huo wa juzi, Yanga sasa imefikisha pointi 12 sawa na timu za JKT Ruvu na Mtibwa Sugar ya Morogoro, ila zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.


Ligi hiyo inaongozwa na Simba yenye pointi 18, ikifuatiwa na Azam FC ambayo ina pointi 14 na JKT Oljoro, ipo nafasi ya tatu kwa pointi 13.

0 comments

Post a Comment