Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - TUNDU LISSU ASEMA WAZIRI NGELEJA MUONGO

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WABUNGE  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana waliwasha moto bungeni, huku wakiilazimisha serikali na Bunge kuchukua hatua za haraka kujinusuru.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alimbana vilivyo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akidai waziri huyo amelidanganya Bunge, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akiibana serikali juu ya ufisadi wa Kagoda.
Wakati Lissu alikuwa tayari kuthibitisha kauli yake pale pale, kama kanuni zinavyotaka, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliingilia kati kumnusuru Ngeleja, akataka mbunge huyo awasilishe hoja yake kwa maandishi kuthibitisha uongo wa waziri Ijumaa wiki hii badala ya jana.
Hata hivyo, Lissu alipinga uamuzi huo, akitaka kutetea kauli yake na kuthibitisha uongo wa waziri jana hiyo hiyo, bila mafanikio.
Lissu hakuridhika na majibu ya Ngeleja yaliyotokana na swali lake la nyongeza.
Katika swali hilo, Lissu alitaka kujua hadi sasa ni wananchi wangapi wameondolewa katika kata za Mang,onyi, Ikungi na Mhitiri ili kupisha kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Mining Co. Ltd iliyopewa leseni ya kutafiti dhahabu katika jimbo lake.
Vile vile, alitaka kujua kiasi cha pesa walicholipa; kwanini wamejenga uwanja wa ndege, na kwanini kampuni hiyo ilitwaa maeneo mengine kwa nguvu.
Waziri Ngeleja alijibu kwa kifupi, akisema kampuni hiyo haijachukua maeneo hayo kwa nguvu, na akaongeza kuwa hata mwaka 2008 alifanya ziara na kushuhudia hali hiyo.
Ndipo Tundu alisimama na kutaka kuuliza swali la nyongeza, lakini Makinda alikataa, Lissu akaomba mwongozo wa Spika.
Tundu aliposimama, alisema katika majibu yake Ngeleja ni mwongo; na akataka atoe ushahidi kuthibitisha uwongo wa waziri.
Hata hivyo, Spika Makinda alimtaka Tundu Lissu kuandika maelezo yake, ili Ngeleja ajibu, na kwamba atafikisha maelezo hayo kwenye vyombo vyake ili wayapitie na kutoa majibu bungeni.
Hali hiyo ilimlazimu Tundu kusimama tena na kupambana na Spika kwa kutumia kanuni za Bunge, akihoji iweje Mbunge anapotoa madai kama hayo atakiwe kuthibitisha papo hapo lakini yeye anaambiwa aandike.
Akijibu hoja hiyo, Makinda alisema kutokana na muda mchache uliopo, hawezi kuruhusu malumbano hayo Bungeni kwani yatamaliza muda wa maswali na majibu.
Alisema mazingira yaliyotokea kwa Tundu, yanafanana na tukio la Mbunge mwingine wa CHADEMA wa Arusha Mjini, Godbless Lema wa Arusha Mjini, ambaye katika mkutano wa Bunge uliopita, alitaka kujua hatua ambayo mbunge anaweza kumchukulia kiongozi mkuu kama Waziri Mkuu iwapo amelidanganya Bunge.
Ilikuwa mara baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa kauli ya serikali kuhusu maandamano na mkutano wa CHADEMA, ambayo polisi waliyasambaratisha na kuua watu watatu.
’’Jamani tusome vizuri kanuni. Hili ni kama tukio la Lema ambalo nitalitolea majibu kwenye mkutano huu. Sio lazima utoe maoni sasa hivi ndani ya Bunge.
"Ninamuagiza Tundu aniandike na Ngeleja atajibu, nitapeleka kwenye vyombo vyangu ambako wanaweza kuwakutanisha Lema na Ngeleja na Bunge kusomewa uamuzi Ijumaa. Huo ndio utaratibu," alisema Makinda.
Hata hivyo hatua hiyo haikumridhisha Tundu Lissu ambaye akiwa nje ya Bunge alisema Spika ana nia ya kuwalinda mawaziri wanapobanwa bungeni.
Kwa upande wake, Mnyika aliibua upya suala la ufisadi wa Kampuni ya Kagoda, inayodaiwa kuchota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambalo serikali imekuwa anaogopa kulijadili.
Mara kadhaa huko nyuma, viongozi waandamizi serikali wamesema kwamba ”kagoda hakamatiki” na kwamba ”hafahamiki,” huku taarifa zikionyesha kuwa ufisadi huo ulifanyika katika mazingira ya kisiasa yanayodaiwa kukinufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuchota pesa hizo ni watu wazito ndani ya CCM na mfumo wa utawala nchini.
Ufisadi huo uliibuliwa Bungeni na aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrord Slaa, katika Bunge liliopita. Dk Slaa ni Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Jana Mnyika aligusia suala hilo wakati akiuliza swali la nyongeza, akitaka kujua kauli ya serikali lini itakamilisha uchunguzi kuhusu kampuni hiyo ya Kagoda na kuwachukulia hatua wahusika.
Akijibu swali hilo kwa kifupi sana, Waziri wa Nchi Ofisi Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alisema serikali bado inaendelea na uchunguzi wa tuhuma dhidi ya kampuni hiyo.
Hata hivyo, jibu hilo lilionekana kutowaridhisha wabunge wengi kwani zaidi ya wabunge kumi walisimama kutaka kuuliza maswali ya nyongeza.
Akiuliza swali lingine la nyongeza, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF), alihoji kuwa kwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU) Dk. Edward Hosea, alisema tatizo la kesi ya ufisadi mkubwa kama wa Kagoda ni DPP, hivyo alihoji kama Serikali iko tayari kutoa taarifa Bungeni kuonyesha kesi zilizokwama kwa DPP.
Akijibu swali hilo, Waziri Chikawe alisema Serikali ipo tayari kutoa taarifa hiyo bungeni na itafanya hivyo katika mkutano huu wa tatu wa Bunge unaoendelea mjini hapa.
Kashfa ya Kagoda ambayo ilipata kulitikisa Bunge miaka mitano iliyopita, limekuwa likipigwa danadana na Serikali kwa sababu za kisiasa.
Kampuni ya Kagoda ilikwapua jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT. Fedha hizi na nyingine zipatazo Sh. 73 zilichotwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Taarifa zinaonyesha kuwa ni Yusuf Manji aliyedhamini Kagoda kufungua akaunti katika tawi la CRDB Benki la Holland jijini Dar es Salaam ambako mabilioni ya shilingi yalipitia.
Serikali imekuwa ikikana kufahamu wamiliki wa Kagoda na kwa zaidi ya miaka mitano sasa imekaa kimya juu ya wizi wa kampuni hiyo.
Aidha, serikali imekuwa ikijikanyaga kuhusu wizi huu. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, aliwaandikia maodita wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini akisema, fedha za Kagoda zilitumika kwa “kazi za usalama wa taifa.”
Katika barua yake ya Septemba 15, 2006, Meghji anasema, “Kama unavyofahamu vema, mamlaka ya serikali huwa na siri, vilevile haja ya kugharamia matumizi ya busara. “Kwa hiyo... malipo ya dola 30,732,658.82 za Marekani yaliyofanywa na BoT kwa Kagoda Agriculture Limited, yaliidhinishwa na serikali kugharamia matumizi yake nyeti na ilikuwa lazima kuchukua hatua hii ya kudumisha usiri huu.”
Hatua hii inaleta maswali mengi kuliko majibu; yakiwa ni pamoja na iwapo Manji na wakwapuaji wa Kagoda ndio hasa wanaitwa “Usalama wa Taaifa.”
Baadaye jana Mnyika alitoa tamko kwa vyombo vya habari likisema:
“Itakumbukwa kwamba Kagoda inatuhumiwa kuchota jumla ya dola za Marekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) mwaka 2005.
“Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu ufisadi wa Kagoda; mathalani tarehe 15 Septemba 2006 Waziri wa Fedha wa wakati huo Zakhia Meghji aliandika barua kwa wakaguzi wa mahesabu wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini kuwa fedha za Kagoda zilitumika kwa kazi ya usalama wa taifa na kutaka usiri na busara katika ukaguzi wa mahesabu ya kampuni hiyo. Baadaye Waziri Meghji alifuta barua hiyo.
“Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba cheti cha usajili wa Kagoda kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA) kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005.
“Mpaka sasa siri za ufisadi wa Kampuni hiyo na wa kampuni zingine zilizohusika kwa wizi wa Kagoda zimebaki kwa Rais Jakaya Kikwete na wajumbe watatu wa timu uliyoiunda wakati huo ikiwemo idadi na majina ya watuhumiwa wanaodaiwa kurejesha sehemu ya fedha.
“Wakati serikali imekuwa ikieleza kwamba haiwajui wamiliki wa Kagoda; taarifa mbalimbali zimekuwa zikimtaja Rostam Aziz (Mb) na wengine.
“Baadhi ya vyombo vya habari vimewahi kuandika kwamba Wakili Bhyidinka Sanze wa Kampuni ya mawakili ya Malegesi (Malegesi Law Chambers) ya Dar es Salaam katika maelezo yake kwa Kamati ya Rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) alikiri kwamba alishuhudia mkataba wa Kagoda na mikataba mingine iliyohusu ufisadi huo.
“Wakili huyo alieleza kwamba mkataba huo ulishuhudiwa na Caspian Construction Limited (inayomilikiwa na Rostam Aziz) iliyopo Dar es salaam na kwamba alielezwa kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiwezesha CCM kugharamia uchaguzi na kwamba maelekezo hayo yalitolewa kwa aliyekuwa gavana wakati huo (marehemu Daudi Balali) na Rais wakati huo Benjamin Mkapa.
“Hata hivyo, pamoja na serikali kwa wakati wote kuendelea kusisitiza kutowajua wamiliki wa Kagoda; Taarifa za hivi karibuni zimemtaja mfanyabiashara Yusuph Manji kupitia kampuni ya familia yake ya Quality Finance Corporation Limited (QFCL) anadaiwa na serikali kurejesha fedha za Kagoda.
“Katika mazingira haya ya utata ndio maana natoa kauli ya kuitaka serikali kutoa tamko la kina kuhusu kashfa hii ya Kagoda.”
Swali la msingi liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Pudenciana Kikwembe (CCM), kuhusu rushwa, akitaka kujua Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba lengo la taifa katika kupambana na rushwa linafanikiwa.
Waziri Chikawe akijibu swali hili alisema kwa kuwa watoaji na wapokeaji wa Rushwa ni wananchi wenyewe, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa askari.
"Vita hii ni yetu sote, ninawaomba viongozi wote wa serikali, siasa na dini na jamii kwa ujumla, kukemea rushwa kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Spika.
Wakati huo huo, moto juu ya mjadala wa Katiba mpya uliwaka jana Bungeni, huku baadhi ya wabunge wakitaka muswada wa serikali unaopelekwa Bungeni uahirishwe.
Aliyeibua hoja hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), akisema wananchi wanahitaji kupewa muda wa kujadili suala hili kabla halijatungiwa sheria.
Zitto alisema ni wabunge wapewe fursa ya kuwaelimisha wananchi wao.
Lakini Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisisitiza kuwa muswada huo utawasilishwa kama ilivyopangwa.
Akijibu swali bungeni jana, Kombani alisema kinachofanyika sasa si kupitisha Katiba Mpya bali kuangalia jinsi ya kuunda tume itakayosimamia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.
Alisema sheria hiyo, pamoja na mambo mengine, ndiyo itakayoanzisha tume itakayoratibu zoezi la utungwaji wa Katiba Mpya.
Alisema muswada huo umekamilika na utawasilishwa katika mkutano huu wa Bunge kwa hatua zaidi.
Waziri Kombani ambaye alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Fakharia Shomar Khamis, alisema muswada huo sanjari na kuainisha majukumu ya tume, utaanisha jukumu la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu katiba inayotumika sasa.
"Watu wanapotosha kwamba Bunge limekuja kupitisha muswada wa Katiba Mpya. Nimeona kwenye kongamano na watu wengine wakijadili. Mkawaambie wananchi hatupitishi katiba mpya sasa," alisema Kombani.
Kwa mujibu wa Kombani, katika utoaji elimu, Serikali itashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Alisisitiza kuwa serikali imeona kuna umuhimu wa kutoa elimu juu ya katiba ya sasa ili wawe katika nafasi nzuri ya kuchangia mawazo ya kuanzishwa kwa Katiba Mpya.
Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alihoji kama Serikali haioni umuhimu wa kutoa elimu juu ya Katiba ya sasa ili wananchi waweze kuchangia mawazo ya kuanzishwa kwa Katiba Mpya.
Hata hivyo, wadau wa katiba, wakiwamo wanasheria, wanasiasa na wasomi kadhaa nchini, wanadai kuwa sheria inayotarajiwa kutungwa kwa muswada huu haikidhi matakwa, na haiendani na mahitaji ya Katiba mpya inayotakiwa.
Hoja kuu ambayo imekuwa ikijengwa kwa muda mrefu na wanazuoni, ni kwamba uhalali wa Katiba unatokana na uhalali wa mchakato wa kuitengeneza, na kwamba kwa staili hii ya harakaharaka ya serikali kutunga sheria inayolalamikiwa, wananchi watashindwa kushiriki kutunga katiba yao.
Wadau wengi wanadai muswada huu hauna maslahi kwa taifa, bali unalenga kulinda maslahi ya kikundi kinachotawala, na kunyamazisha wakosoaji wake.

0 comments

Post a Comment