Waziri wa Nchi Ofisi Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe |
Kesi ya Kampuni ya Kagoda, inayodaiwa kuchota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeibuka tena bungeni jana.
Hoja hiyo ambayo iliasisiwa na aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, miaka mitano iliyopita, jana iliibuliwa tena na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA).
Mnyika ambaye alikuwa akiuliza swali la nyongeza, alitaka kujua kauli ya serikali lini itakamilisha uchunguzi kuhusu kampuni hiyo ya Kagoda utakamilika na wahusika kuchukuliwa hatua.
Akijibu swali hilo kwa kifupi, Waziri wa Nchi Ofisi Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alisema serikali bado inaendelea na uchunguzi wa tuhuma dhidi ya kampuni hiyo.
Hata hivyo, jibu hilo lilionekana kutowaridhisha wabunge wengi kwani zaidi ya wabunge 10, akiwamo Mnyika, walisimama kutaka kuuliza maswali ya nyongeza.
Akiuliza swali jingine la nyongeza, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF), alihoji kwamba kwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, alisema tatizo la kesi ya ufisadi mkubwa kama wa Kagoda ni DPP, hivyo alihoji kama Serikali iko tayari kutoa taarifa bungeni kuonyesha kesi zilizokwama kwa DPP.
Akijibu swali hilo, Waziri Chikawe alisema serikali ipo tayari kutoa taarifa hiyo bungeni na itafanya hivyo katika mkutano huu wa tatu wa Bunge unaoendelea mjini hapa.
Kashfa ya Kagoda ambayo ilipata kulitikisa Bunge miaka mitano iliyopita, imekuwa ikipigwa danadana na serikali kwa sababu za kisiasa.
0 comments