Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Chadema wamtiwisha JK deni la Dowans

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa, amesema wanaopaswa kulipa deni la Dowans ni Rais Jakaya Kikwete na Kamati kuu ya CCM.Dk Slaa imetoa kauli hiyo siku moja baada ya Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kubariki Dowans ilipwe Sh 94 bilioni kufuatia kampuni hiyo kushinda kesi katika Mahakama ya Biashara ya Kimataifa (ICC), dhidi ya serikali ya Tanzania.

Akihutubia katika Kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema na kuwashirikisha vijana wa chama hicho walioko vyuo vikuu jijini Dar es Salaam jana, Dk Slaa alisema amepata taarifa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu wakiongozwa na Rais Kikwete walikubali  Dowans ilipwe na Serikali.

 "Ni uzembe umefanyika katika suala hilo, mimi nasema alipe Rais Kikwete na Kamati Kuu ya CCM,” alisema Dk Slaa huku akishangiliwa na mamia ya wanafunzi na wafuasi wa chama hicho waliofurika Viwanja vya Mabibo External.

Kuhusu hukumu hiyo, Dk Slaa alisema kuna mambo mengi ambayo yako kinyume na sheria lakini hakuna mtu anayejali kuyashughulikia.

Alitoa mfano wa taarifa zilizopo kuwa kesi hiyo haijawasilishwa mahakama kuu ya biashara kama inavyohitajika kisheria ili malipo yafanyike na kwamba kilichopelekwa ni viambatanisho vya kesi.

“Kuna utata mkubwa sana katika kesi hii, kwanza kesi yenyewe haijasajiliwa katika Mahakama Kuu kama inavyotakiwa, kilichowasilishwa huko ni Indices (Viambatanisho) za kesi, tunataka Mwanasheria Mkuu atupe maelezo,” alisema Dk Slaa.

Alifafanua kuwa Kampuni ya uwakili ya Rex Attorney iliyokuwa mshauri wa Serikali wakati wa kuvunja mkataba huo, inapaswa itoe maelezo wakati huu Dowans inatakiwa kulipwa.
“Rex Attorney ni nani, aliishauri nini Serikali kuhusu kuvunja mkataba na anaishauri nini kuhusu kuilipa Dowans?” alihoji.

Hali ya Siasa
Akizungumzia hali ya siasa nchini, Dk Slaa alisema hadi sasa, nchi imechanganyikiwa na kusisitiza kauli yake kuwa nchi hii haitawaliki.

Huku akikatizwa na kelele za mara kwa mara kutoka kwa wanafunzi waliofurika katika viwanja hivyo, Dk Slaa alisema anashangazwa na jinsi serikali inavyozuia watu kuzungumzia masuala ya siasa.

“Ukitaka watu wasiongee siasa unataka nini, hii ni kasumba ya viongozi wasiopenda kufikiri, wanaolichanganya taifa na kusababisha migogoro mikubwa,” alisema na kuongeza:
“Viongozi wa dini wanapokemea watu wanaotenda maovu katika siasa wanasemwa kuwa wanaingilia siasa, lakini Rais Kikwete alipowaita viongozi hao Kunduchi kuwaomba kura walikuwa hawaongei siasa?,” alihoji.

Udini
Dk Slaa pia alitumi nafasi hiyo kuwaonya viongozi wanaoeneza maneno kuwa kuna udini nchini.

Alisema dhana hiyo inachochewa na viongozi dhaifu wanaotafuta hoja itakayomeza hoja za msingi za maendeleo ya taifa.

Dk Slaa ambaye alishika nafasi ya pili katika matokeo kura z urais kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita alisema anashangazwa na kauli za Rais Kikwete kuwa kuna harufi ya udini wakati hachukui hatua yoyote na wakati udini ni kosa la jinai kwa vile ni sawa na ubaguzi.

“Kama rais analalamika kuwa kuna udini na hachukui hatua, nani achukue hatua, hatujaona mtu yeyote aliyekamatwa kwa kuhubiri udini, Watanzania bado tunaishi kama ndugu tena kwa amani,” alisema Dk Slaa.

Alitoa mifano ya mwaka 1987 kulipoibuka vuguvugu kubwa la udini, lakini aliyekuwa rais kipindi hicho, Mzee Ali Hassani Mwinyi, alichukua hatua za kuunda kamati kutoka madhehebu yote iliyoshughulikia kiina cha tatizo hilo na kulimaliza.

Alisema hakuwahi kusikia Rais mstaafu Mwinyi akikemea udini majukwaani na kushangaa kauli za Rais Kikwete juu ya kuwepo kwa udini ambao hakuna hata mmoja aliyechukuliwa hatua za kisheria.

Vyuo vikuu na Siasa
Akizungumzia vyuo vikuu kujihusisha na siasa, Dk Slaa alisema ni jambo la ajabu kwa wanafunzi kuzuiwa kushiriki siasa wakati vyuo vinawafundisha siasa.

“Mwalimu Julius Nyerere alianza harakati za ukombozi akiwa chuoni, kwenye vyuo ndiko kunakopikwa watu wanaofikiria, ndio kituo cha mawazo na hoja za maendeleo, tunataka viongozi makini na si viongozi wa propaganda,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Nchi isiyotaka kuchukua changamoto kutoka kwa vijana itakuwa imepotea. Wakati umefika vyuo viwe ni msaada kwa nchi na wanafunzi wanatakiwa wawe huru”.

Kiongozi huyo wa Chadema aliituhumu Bodi ya Mikopo kuwa imejaa upendelea na kuongeza na kwamba alishawahi kutoa mapendekezo  ivunjwe na kuundwa mpya.

Akizungumzia viongozi wa nchi kupewa shahada za heshima, Dk Slaa alisema inasikitisha kuona kuwa chuo ambacho hata hakina program ya Shahada Uzamili, kinakuwa na sifa ya kutoa shahada ya heshima.

“Degree (shahada ya kwanza) hazigawanywi kama karanga, haya ni matokeo ya kupendeleana, chuo chenyewe kina matatizo chungu nzima, wakuu wake wanatoa ‘degree’ hizo ili waendelee kunufaika,” alisema huku akishangiliwa na wanafunzi hao waliokuwa wakitamka “UDOM...UDOM....UDOM....” wakimaanisha chuo Kikuu cha Dodoma.

Mabere Marando
Kwa upande wake, Wakili wa Kujitegemea na mwanachama wa Chadema, Mabere Marando, alisema suala la katiba mpya kwa sasa halina mjadala tena.

“Katiba mpya, tupende tusipene, Kikwete apende asipende, CCM ipende isipende, lazima iandikwe upya hilo si suala la mjadala tena,” alisisitiza Marando a kuongeza:
“Hoja iliyopo ni je viongozi walio madarakani wanasoma alama za nyakati au wapo tu kama kisiki wanasubiri wafagiwe na upepo”.

Marando pia aliponda hali ya kupingana iliyojitokeza kwa mawaziri, baraza la vijana wa CCM kupingana na wazee kuwa ni ishara kuwa chama hicho kinaelekea kufa.

“Chama chochote cha siasa kinazaliwa, kinakua, kinazeeka na kinakufa, CCM sasa inakufa. Hebu kisaidieni kife bila ya sisi kupata madhara,” alisema Marando ambaye ni mmoja wa waasisi wa mageuzi nchini.

Kuhusu mabadiliko ya katiba, Marando alitoa mfano wa katiba mpya ya Kenya kuwa ina vipengele ambavyo ni lazima katiba yetu iwe navyo.

Alitoa mifano ya Ibara ya 71 ya Katiba ya Kenya kuwa masuala ya madini lazima yaidhinishwe na Bunge kabla ya serikali kutia saini mkataba wowote ule.

Alisema pia Ibara ya 152 ya katiba hiyo kuwa inamtaka Rais kuchagua baraza la mawaziri nje ya bunge na wabunge watakuwa na kazi ya kukubali au kukataa uteuzi wake.


John Mnyika
Naye Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, alionya kuwa iwapo viongozi walioingia madarakani kwa hila hawatabadilika, nchi inaweza kugeuka na kuwa kama Tunisia.

Joseph Mbilinyi (Sugu)
Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu aliyekuwa kivutia kikubwa katika kongamano hilo, aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kusoma kwa bidii na kuja kuikombia nchi.

Sugu ambaye alilazimishwa na wanachuo hao kuongoza kuimba wimbo wa taifa wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, alisema amekuwa mstari wa mbele katika kupigia kelele matatizo yanayowakabili wanafunzi vyuoni na kuwasisitiza kusoma ili watumie elimu yao katika siasa za kweli na si propaganda.


Kutoka Dodoma, Israel Mgussi na Masoud Masasi wanaripoti kuwa,
Chadema mkoani Dodoma kimefanya maandamano ya amani kuunga mkono maandamano yaliyofanywa na chama hicho mkoani Arusha Januari 5, mwaka huu kupinga mchakato wa uchaguzi na matokeo ya Meya wa Jiji la Arusha.


Katika maandamano ya jana ambayo mamia ya wafuasi wa chama hicho walijitokeza Chadema ilitoa tamko la kulaani Jeshi la Polisi kwa madia kuwa linaendelea kuwakumbatia waovu wanaoitafuna nchi kwa kuwatisha na kuwaua raia wasiokuwa na hatia.


Mkurugenzi wa Oganizesheni na Mafunzo wa chama hicho taifa, Benson Singo Kigaila ambaye ndiye alipokea maandamano hayo katika Viwanja vya Barafu mjini hapa alisema Tanzania na nchi tajiri lakini inashindwa kuendelea kutokana kushamiri kwa ufisadi.


Alisema hata askari polisi ambao wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi, wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na kutotambua umhimu wa ustawi wa taifa lao.


“Ndugu zangu, nchi hii mali yetu, hatujaikodisha,hatuwezi kuvumilia maovu yanayoendelea,uchaguzi wa Arusha lazima urejewe upya,l azima wananchi tuwe tayari kupigania uhuru wetu, tunafahamu hata maauaji yaliyotokea kule Arusha haikuwa bahati mbaya,”alisema Singo.


Katika maandamano hayo ambayo yalianzia ofisi za chama hicho mkoa kupitia Soko Kuu la Majengo,Hospitali ya Mkoa, Barabara ya Morogoro na kuishia Viwanja vya Barafu yaliongozwa na askari polisi waliokuwa wakilinda usalama.
Tags:

0 comments

Post a Comment