UPO mpasuko wa wazi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kama ambavyo vikao na matamko mbalimbali yanayotoka kwenye chama hicho yanavyoonyesha, hasa kuhusu sakata la serikali kulipa mabilioni ya shilingi kwa kampuni ya Dowans.
HALI ya hewa ndani ya chama tawala CCM, inaonekana kuchafuka baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho (CC), kutoa uamuzi wa mambo mbalimbali ikitofautiana na tamko lililotolewa na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) juzi.Miongoni mwa uamuzi wa CC iliyokutana chini ya mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya KIkwete, ni kubariki malipo ya Sh94 bilioni kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC).
Tofauti hiyo ya CC iliyopinga tamko la UVCCM inaashiria kuchafuka kwa hali ya hewa ndani ya chama hicho kikongwe nchini.
Katika tamko lake, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa pamoja na mambo mengine lilipinga mpango wa Serikali kuilipa kampuni ya Dowans Sh94 bilioni kama hukumu ya ICC ilivyoagiza kwa kuwa pesa hizo ni nyingi kwa hali ya maisha ya Watanzania.
Katika taarifa hiyo, UVCCM imetaka hoja hiyo irudishwe bungeni ili Watanzania wajue nani aliyeifikisha mahali ilipo sasa.
Lakini jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio mbalimbali ya kikao hicho kilichoketi juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati alisema suala la Dowans limeamuliwa na mahakama ya kimataifa hivyo utekelezaji uliopo ni kuilipa kampuni hiyo.
“Kamati Kuu imetafakari na kubaini kuwa huu ni uamuzi wa ICC, mahakama hii imetusikiliza wote na sisi tumeonekana kuwa na makosa kwa kuwa tulivunja mkataba, hivyo imeona ni busara na wajibu kuheshimu uamuzi wa mahakama,” alisema Chiligati
Aliongeza: “Kwa vile wapo Watanzania waliofungua kesi kupinga malipo ya Dowans katika Mahakama Kuu, CC imeona ni vyema Serikali ikasubiri maamuzi ya Mahakama Kuu kuhusu pingamizi hili.”
Akizungumzia kauli za UVCCM kupishana na za Kamati Kuu, Chiligati alisema kuwa vijana nao wana haki ya kutoa mawazo yao.
“Vijana wana haki ya kutoa maoni yao, tunayachukulia kama maoni ya watu wengine waliyoyatoa kuhusu mambo mbalimbali likiwemo suala la Dowans,” alisema Chiligati.
Alisema kuwa suala la Dowans halina ubishi wala Serikali haiwezi kufanya ubabe, bali itafanya uamuzi ya busara na hekima kwa kuwa imeonekana kuwa na makosa.
“Kila tukio linalotokea katika maisha ni fundisho, kuhusu suala la Dowans kwa kweli tumejifunza, tumefanya kosa na tumepigwa penalti, kipindi kingine Serikali haitafanya makosa, wote tumejifunza ni somo tosha,” alisema Chiligati.
Aliongeza, kuwa sio kwamba wazee ndani ya CCM wameshindwa kazi na kusisitiza kwamba maoni ya vijana ni changamoto kwa kuwa vijana damu zao zinachemka na kwamba CCM lazima iwe na vijana na wazee ili mambo yaende sawa.
“Tutakaa na vijana na tutaelewana tu, suala hili kwanza lisubiri uamuzi ya Mahakama Kuu,” alisisitiza Chiligati.
Kauli ya Mahakama Kuu kuhusu Dowans
Wakati mgongano huo baina ya CCM na UVCCM ukitokea kuhusu suala la Dowans, kwa upande wake Mahakama Kuu imesema Tanesco inaweza kuilipa Dowans nje ya mahakama bila tuzo hiyo kusajiliwa.
Kauli hiyo ya mahakama imekuja wakati tayari Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na wanaharakati wa haki za kijinsia nchini wakiwasilisha Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara taarifa ya nia ya kupinga Serikali isiilipe kampuni ya Dowans Sh94 bilioni ilizoamriwa na ICC.
Katika hukumu hiyo ICC ililiamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia hiyo kutokana na kuvunja mkataba na kampuni hiyo kinyume cha taratibu.
Lakini, jana Mahakama Kuu ililitoa ufafanuzi na kueleza kuwa malipo dhidi ya kampuni hiyo yanaweza kufanyika hata kama tuzo hiyo haitasajiliwa mahakamani hapo.
Akizungumza na vyombo viwili vya habari ofisini kwake jana Mwananchi likiwemo, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu Tanzania, Salvatory Bongole, alisema kwa mujibu wa sheria zinazotumika katika usuhishi wa migogoro hiyo, malipo hayo yanaweza kufanyika hata nje ya mahakamani ikiwa pande husika zitakubalina hivyo.
“Pande zinazohusika (mshinda tuzo na mshindwa tuzo), wanaweza kukubalina na kumalizana kwa kulipana nje ya Mahakama, lakini kama watashindana ndio wanaweza kurudi mahakamani kusajili tuzo hiyo kwa mujibu wa taratibu,” alisema Bongole.
Bongole alisema ingawa mtu yeyote mwenye maslahi na tuzo hiyo anaweza kuweka pingamizi ili tuzo hiyo isiweze kusajiliwa mahakamani, iwapo sababu zake zitakubalika, lakini kama wahusika wataamua kumaliza nje ya mahakama basi mapingamizi yoyote hayatakuwa na nafasi tena.
Kutokana na maelezo hayo iwapo Dowans na Tanesco wataamua kutumia utaratibu huo kumalizana nje ya mahakama, ni dhahiri pingamizi lao halitakuwa na nguvu kisheria.
Uwezekano wa malipo hayo kufanyika kwa mfumo huo nafasi yake ipo wazi kutokana na Serikali kubainisha kuwa haina pingamizi dhidi ya hukumu hiyo hivyo kuridhia kulipa fidia.
Desemba 27 mwaka jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema ambaye ni mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya kisheria, aliliambia Mwananchi kuwa baada ya kuisoma hukumu hiyo ameridhika kuwa iko sawa na kwamba Serikali haina nia ya kukata rufaa.
Siku chache baadaye Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alitoa kile alichokiita tamo rasmi la Serikali kuhusu malipo hayo akisema kuwa Serikali imekubaliana na ushauri wa Mwanasheria Mkuu.
Alisema ingawa kiwango kinachotakiwa kulipwa na Serikali kwa kampuni hiyo ni kikubwa, lakini alisema hakuna jinsi na badala yake Serikali imemua kulipa ili kuepuka kujiingiza katika matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa riba ya malipo hayo.
Akitoa ufafanuzi wa mchakato wa usajili wa tuzo hiyo, Msajili Bongole alisema tayari tuzo hiyo imeshatumwa mahakamani hapo kutoka ICC na kwamba imetumwa na Katibu wa Sekretarieti ya ICC, Victory Oraowski, lakini akasema kuwa, bado haijapokewa rasmi kisheria.
Alisema licha ya tuzo hiyo kuwasilishwa mahakamani hapo, mchakato wa usajili wake haujaanza kwa kuwa utaratibu wa kisheria bado haujakamilika kulinganga na taratibu za usuluhishi na tuzo zinazotolewa pasipo amri ya mahakama.
“Sheria zinazotumika katika usajili wa tuzo hiyo ni sheria ya usuluhishi (Arbtration Act) Sura ya 15 ya Sheria za Tanzania pamoja na sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (Civil Procedure Code- CPC), sura ya 33 jedwali la 2 kifungu cha 20.
Alisema baada ya tuzo hiyo kuwasilishwa mahakamani, mshinda tuzo anapaswa kuwasilisha maombi ya maandishi akiambatanisha na hati ya kiapo ili tuzo yake iweze kusajiliwa.
Alisema baada ya mshindi wa tuzo kuwasilisha maombi hayo, Mahakama itatoa taarifa kwa mshindwa tuzo atoe sababu kwa muda maalumu atakaopewa na Mahakama aeleze kwa nini tuzo hiyo isisajiliwe.
“Kama mshindwa tuzo akisema hana pingamizi tunaisajili na akisema ana pingamizi basi tunasikiliza kwanza pingamizi hilo na kulitolea uamuzi. Baada ya taratibu hizo ndo tunaweza kuisajili sasa na kuwa nguvu ya kumlazimisha mdaiwa kulipa deni,” alisema Bongole.
Alisema mbali na mshindwa, mtu mwingine yeyote ambaye pia ataona maslahi katika tuzo hiyo ana haki ya kuwasilisha pingamizi lake ambalo pia litasikilizwa na kutolewa uamuzi kabla ya tuzo kusajiliwa.
“Kwa hiyo kwa sasa tumeletewa tu, hiyo tuzo ili tuihifadhi tukisubiri mwenye tuzo hadi atakapoleta maombi na wala si kwamba sisi ndio tunakwenda kumtafuta, mahakama haiwezi kwenda kutafuta kesi,” alisema Bongole.
Hata hivyo, Bongole alibainisha kuwa hakuna muda maalumu wa mshinda tuzo kuwasilisha maombi ya usajili wa tuzo yake na kwamba anaweza kukaa hata mwaka mmoja au anaweza kukubalina na mshindwa tuzo na kumalizana nje ya mahakama.
Mambo mengine ya Kamati Kuu
Mbali na suala la Dowans, Chiligati pia alizungumzia suala la baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri kutoa lugha tofauti kuhusu mambo mbalimbali na kusema kuwa kikao cha Kamati Kuu hakikujadili kwa kina suala hilo kwa kuwa tofauti zao watazimaliza ndani ya vikao vyao.
Chiligati alitolea ufafanuzi suala hilo baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari huku akifafanua: “Katika Kamati kuu hatukulizungumza suala hili kwa kuwa tunajua watalimaliza wenyewe kwa mujibu wa kanuni zao.
0 comments