Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ulinzi mkali kesi ya Dk Slaa, Mbowe Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAMIA ya wakazi Jiji la Arusha na idadi kubwa ya maafisa usalama wa taifa jana walihudhuria mahakamani kusikiliza kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali inayowakabili watu 29 wakiwamo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Viwanja vya Mahakama ya Mkoa wa Arusha jana viliendelea kuwa katika ulinzi mkali huku wafuasi wengi wa Chadema wakiwa wamezuiwa kuingia katika kumbi za mahakama kufuatilia kesi hiyo.

Kesi hiyo ilitajwa mapema asubuhi saa 3:00 na kusababisha watu wengi kuchelewa, lakini iliahirishwa hadi Februari 22 mwaka huu baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi haujakamilika.

Kama ambavyo ilitarajiwa, idadi ya watuhumiwa ilianza kupungua baada ya jana waendesha mashitaka wa Serikali wakiongozwa, Zakaria Elisaria kueleza kuwaondoa watuhumiwa wawili, ambao hawakusomewa mashitaka Januari 6.

Awali ilielezwa kuwa watuhumiwa hao walikuwa wamelazwa hospitalini, lakini hata hivyo, Mahakama ilipohamishiwa Hospitali ya Mkoa, hawakuwepo na kukuta watuhumiwa wanne pekee.

Hata hivyo, jana watuhumiwa sita, akiwamo Dk Slaa na mkewe hawakuhudhuria mahakamani baada ya kuelezwa na wakili wa utetezi, Method Kimomogoro kuwa ni wagonjwa.
 
Watuhumiwa wengine, akiwapo Mbowe, wabunge Philemon Ndesamburo, Godbless Lema na Joseph Selasini, walifika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo inayowakabili.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Elisaria aliiambia Mahakama mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha,  Charles Magesa kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kuvunja sheria kwa  kufanya kusanyiko bila ya kuwa na kibali Januari 5, mwaka huu.

Washtakiwa wengine ambao hata hivyo, hawakuwepo mahakamani ni pamoja Dadi Gadi, Juma Wambura, Elisante Noel pamoja na Richard Kimario.

"Mheshimiwa hakimu hawa wanne bado wapo Hospitali Mount Meru, wanaendelea na matibabu hali zao mbaya, hawawezi kuja mahakamani. Pia Dk Slaa na mchumba wake nao wapo Hospitali ya Muhimbili wanafanyiwa upasuaji. Dk Slaa amefanyiwa upasuaji kwenye mkono na Josephine amefanyiwa upasuaji kichwani wote wapo Muhimbili," alisema wakili wa washtakiwa hao, Methord Kimomogoro.

Baada ya hakimu Magesa kupata taarifa ya sababu ya washtakiwa hao kutokuwapo mahakamani hapo alimtaka wakili wa washtakiwa kuwasilisha hati za ugonjwa mahakamani kutoka kwa daktari anayewatibu ikiwa hali zao zitaendelea kuwa mbaya na kushindwa kuhudhuria kesi yao tena.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 22 mwaka huu ambapo itatajwa tena.

Hata hivyo, kufuatia wingi wa wafuasi wa Chadema uliokuwepo nje ya Ukumbi wa Mahakama, mbunge wa Jimbo la Arusha Godbless Lema alilazimika kuzungumza nao na kuwataka kuwa wavumilivu, akiwaahidi kuwa Februari 22 wote wataingia mahakamani kusikiliza kesi.

"Msichoke kuja hapa, kuja kwenu kuna maana kubwa sana ya kudai haki na mna haki ya kuingia vyumba vya mahakama. Febrauri 22, mimi ntawahi getini kusimamia muingie mahakamani,"alisema Lema.

Baada ya hutuba hiyo, viongozi hao wa Chadema waliondoka na wafuasi wao kuanza kuwashangilia na baadaye walitawanyika kwa amani.

Mbowe alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba wasingekwenda mahakamani kama moja ya sharti la kumaliza mgogoro wa kisiasa mkoani Arusha.

Chadema ilitoa kauli hiyo Januari 12, mwaka huu katika tamko lao walilotoa wakati wa kuaga miili ya watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano hayo.

"Kesi walizofunguliwa viongozi na wafuasi wa Chadema, zifutwe bila masharti na kuanzia sasa, viongozi hao, hawatahudhuria tena mahakamani kusikiliza kesi hizo za uongo," alisema Mbowe alipokuwa akisoma tamko la chama hicho

Kufutwa kwa kesi hizo au Chadema kutohudhuria tena mahakamani, ni moja kati ya masharti saba yaliyotolewa na chama hicho kwa Serikali katika kulimaliza tatizo hilo.

Masharti mengine ni kujiuzulu na kufunguliwa kesi za jinai kwa IGP Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha.

Mbowe alisema katika kuhakikisha masharti hayo yanafuatwa na madai kutekelezwa, chama hicho kimewaelekeza viongozi, wanachama na wafuasi wake nchini, kuandaa maandamano ya amani kwa ajili ya kulaani mauaji hayo
Tags:

0 comments

Post a Comment