Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wanamuziki 13 wafa ajalini

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WASANII 13 wa Kundi la Taarabu la Five Stars wamefariki dunia juzi usiku na wengine saba kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kupata ajali huko Mikumi, Morogoro.Rais wa bendi hiyo, Ally Juma, maarufu kama “Ally J” ambaye pia ni miongoni mwa walionusurika, alisema basi hilo lilikuwa na abiria 24, kati yao wasanii walikuwa 21, madereva wawili na abiria mwingine mmoja.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni kiongozi wa bendi hiyo, Nassoro Madenge na msanii wake maarufu ambaye katika siku za karibuni amekuwa akiwavutia mashabiki wengi wa muziki huo wa mwambao, Issa Ally maarufu kama Kijoti.
Wengine waliofariki dunia ni waimbaji, Husna Mapande na Hamisa Mussa; Shebe Juma (mpiga gitaa la solo), Omary Hashim (mpiga gitaa la besi), Omary Abdallah maarufu kama Tall (fundi mitambo), Hassan Ngereza (matangazo), Tizzo Mgunda na Rama Kinyoya (wapiga kinanda) na Maimuna Makuka, mcheza shoo wa kundi la Kitu Tigo la Ilala.

Mwingine ni mbeba vyombo wa bendi hiyo, Haji Mzaniwa (32) aliyefariki wakati akikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.

Miongoni mwa walionusurika katika ajali hiyo ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ni mwimbaji mkongwe wa taarabu nchini, Mwanahawa Ally, ambaye alikuwa ni mwimbaji mualikwa.

Wengine ni Suzana Benedict (32), Zena Mohamed (27), Samila Rajab (22), Rajab Kondo (25), Mwanahawa Hamis (38), Shaban Hamis (41) na Msafiri Mussa (22). Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema basi hilo aina ya Toyota Coaster lilipinduka baada ya kugonga lori lililokuwa limesimama barabarani baada ya dereva wa basi hilo lililokuwa katika mwendo mkali kukwepa kugongana uso kwa uso na lori jingine lililokuwa likija mbele.

Baada ya kugonga lori hilo lililokuwa limesheheni mbao, basi hilo lilipinduka na kuchanika vipande na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi. Dereva na baadhi ya abiria waliokuwa upande wake ndiyo walionusurika.

Mashuhuda hao walisema kwamba ajali hiyo ingeweza kusababisha vifo zaidi kama si jitihada za dereva wa lori aina ya Scania lililokuwa likija mbele, kukwepa. Katika jitihada hizo, lori hilo nalo lilipinduka.

Mkuu wa Usalama Barabarani, Mkoa wa Morogoro, Ibrahim Mwamakula alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa mbili usiku katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, kilometa takriban sita kutoka lango kuu la kuingia katika hifadhi hiyo.

Mwamakula alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi hilo, Juma Hassan ambaye anadaiwa kutoroka mara baada ya ajali hiyo. Bendi hiyo ilikuwa Mbeya ambako ilifanya onyesho lake la mwisho Jumapili iliyopita wilayani Kyela. Kabla ya kwenda huko, ziara ya kundi hilo la 5 Stars ilianzia Morogoro Jumatano na kufuatiwa na maonyesho mengine katika Miji ya Mikumi, Kilosa na Makambako

Tags:

0 comments

Post a Comment