Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wabunge 50 kuwekwa kitimoto

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WABUNGE 52 watafikishwa katika Baraza la Maadili, kujadiliwa na kuhukumiwa kutokana na kushindwa kujaza fomu za maadili ya uongozi wa umma tangu mwaka 2005, Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba imeelezwa.
Akizungumza na kamati hiyo iliyotembelea ofisini kwake jana, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Salome Kaganda, alisema wabunge hao watafikishwa kwenye baraza hilo Aprili 15, mwaka huu.

“Kila mbunge kati yao atatakiwa kueleza ni kwa nini hakujaza fomu hizo tangu zilipotolewa na baada ya hapo hukumu itatolewa,” alisema Kaganda.

Alisema wabunge hao ni wale ambao tangu fomu hizo zianze kutolewa hawajawahi kuzijaza kabisa.
Kamishna aliieleza kamati hiyo ya Bunge kuwa  hadi sasa Baraza la Maadili limepokea malalamiko 46 dhidi ya viongozi wanaokwepa kujaza fomu zao za tangu mwaka 2007, ambayo hayajawahi kutolewa hukumu. Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Angella Kaniki, alisema malalamiko hayo ni machache ikilinganishwa na hali halisi.

“Inawezekanaje malalamiko haya yawepo na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wahusika?," alihoji Kaniki.
Kamati pia imeishangaa sekretarieti hiyo kwa kuwa dhaifu katika kuwaadhibu viongozi wa umma wanaokiuka sheria na maadili ya utumishi wa umma.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Paul Lwanji, alisema baadhi ya viongozi wa umma wanatoleana maneno na kunyosheana vidole hadharani, lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi yao.  “Huu ni uvunjaji wa maadili kwa kiwango cha juu. Kuongea ovyo na kutupiana maneno ya kebehi hadharani ni kukosa uzalendo. Hili linafaa lingizwe kwenye Sheria ya Maadili ili iweze kuadabisha wahusika ipasavyo,” alisema Lwanji.

Kamati hiyo ya Bunge ilishauri kuwa Sekretarieti hiyo inapaswa kuwatambua viongozi waadilifu, kuenzi na kusimamia sheria ili kujenga uzalendo na utaifa.

Wajumbe wa kamati hiyo waliishauri Sekretarieti hiyo kuongezewa wajumbe, kwani idadi ya sasa ya watu watatu haitoshi. Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Idara ya Utumishi wa Umma, Tixon Nzunda, alifafanua juu ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.

Alisema sheria hiyo ina uwezo wa kumhoji kiongozi yeyote na kukagua akaunti yake ijapokuwa hatua hizo zina mlolongo mrefu wa kupitia mahakamani.

Alibainisha changamoto zilizopo katika utekelezaji wa sheria hiyo kuwa ni pamoja na upungufu  unaosababisha kudorora kwa utendaji kazi na upungufu wa fedha. Alisema Sekretarieti inahitaji Sh12 billioni ili kuweza kujenga ofisi na kufanya maendeleo mengine. "Bajeti yetu sasa ni Sh250 millioni kwa mwaka ambayo haitoshi hata kulipia kodi ya pango la ofisi," alisema.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo ya Bunge, jana ilishangazwa na hatua ya Mbunge wa Musoma, Nimrodi Mkono, kuwakaribisha katika ofisi hizo akisema kuwa eneo hilo ni lake. “Ndugu wajumbe karibuni sana hapa ni nyumbani kwangu mjisikie mko huru,”alisikika Mkono akiwaambia wajumbe wa kamati hiyo.

Hatua hiyo ya Mkono ilionekana kuchafua hali ya hewa na kusababisha wajumbe wa Kamati hiyo kuihoji sekretarieti hiyo kama jengo hilo linamilikiwa na mbunge huyo wa siku nyingi. Hata hivyo, Kaganda alisema kuwa mwenye hati miliki ya jengo hilo ni Rais.

Tags:

0 comments

Post a Comment