SIKU kadhaa baada ya kuibuka kwa mlolongo wa majibizano na kurushiana tuhuma miongoni mwa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sekretariati ya umoja huo safari hii imetakiwa kuomba radhi Watanzania kwa lugha chafu iliyoelekezwa kwa wazee na kukidhalilisha chama mbele ya wananchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM mkoani Kilimanjaro, Paul Makonda, alisema umoja huo umekuwa ukitoa matamko mbalimbali kupitia kwa katibu wake mkuu, ambayo yamekuwa yakishambulia viongozi wastaafu na kukiuka kanuni za umoja huo.
“Baraza Kuu la UVCCM limejinasibu kwa siku za karibuni na kutoa matamko kadhaa, katibu wake mkuu kuibuka na kumshambulia waziwazi Waziri Mkuu mstaafu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Frederick Sumaye, sio tu ni utovu wa nidhamu bali ni kuacha majukumu na kwenda nje ya wajibu wake,” alisema Makonda.
Makonda alisema kwa mujibu wa sehemu ya kanuni za UVCCM, hakuna hata moja inayoonyesha kwamba, UVCCM itakuwa na jukumu la kuelekeza cha kufanyika ama CCM au jumuiya nyingine za chama, serikali na taasisi zake bali kutekeleza katiba ya CCM.
Makonda alisema UVCCM ni jumuiya ya chama hivyo haina mamlaka ya kutoa maelekeezo kwa chama ama serikali.“Ukiona gari linapita reli sio jambo la ajabu, lakini gari moshi likipita barabarani basi ni tatizo kubwa, kwani lenyewe lina njia yake hiyo tu (specific way), ambapo haliwezi hata kwa dharura kuacha njia yake na kwenda barabarani,” alisema.
Aliendelea kuwa kwa kutoa matamshi dhidi ya Sumaye, Baraza Kuu limeidhalilisha Halmashauri Kuu ya CCM ambayo Sumaye ni mjumbe wake na Kamati Kuu ya CCM, ambayo Sumaye amekuwa mjumbe kwa miaka kumi mfululizo na kutumikia kwa uadilifu.
Alisema kwa kudhalilisha taasisi hizo mbili ndani ya chama, basi amekidhalilisha CCM na viongozi wake wote na amesababisha usumbufu na msuguano miongoni mwa viongozi wa chama na serikali, kwani Sumaye ni mtu anayeheshimiwa ndani na nje ya serikali ya Tanzania.Hivyo, Makonda alisema UVCCM ibaini kuwa imefanya makosa na inatakiwa kuomba radhi Watanzania na wazee ambao wamewakosea adabu.
Makonda alisema tatizo kubwa lililopo kwa sasa, ni ulegelege wa uongozi wa juu kiasi cha kufanya uamuzi ambao unaendana na makundi ya watu, aliowaita wenye fedha ambao wana nia ya kuchafua watu wanaoelekea kugombea urais kwenye chama hicho.
Alisema umoja huo umekuwa na tabia ya kuziba watu midomo, kiasi chakufanya vijana waogope kusema ukweli ingawa wanajua, kwa kuhofia kufukuzwa kazi au vyuoni.“Kwa woga huu ndio maana UVCCM imefikia hapa, lakini kuna wachache ambao tutajitokeza na kusema kweli hata kama kutahatarisha maisha,” alisema na kuongeza kuwa, hawezi kuishi kwenye nchi ambayo hata kama anajua ukweli ataogopa kuusema kwa kuogopa kufa.
Alishutumu vijana hao wa kitaifa kwa kujali zaidi maslahi yao, kwa madai kuwa walioko wameshakula na sasa ni ‘muda wao kula’.
“Vijana waliopikwa kichama tumewapoteza, sasa tumebakia na wahuni wanaovalia mashati ya kijani na kuleta mifarakano," alisema.Kijana huyo alipambanua kuwa UVCCM inajifanya kuwa inataka, lakini kwa maslahi ya wachache kujipambanua kama taasisi pekee ndani ya taasisi kubwa.Kukosa uadilifu, kukiuka kanuni halali za jumuiya na kukiuka katiba ya CCM ni udhihirisho wazi kuwa, viongozi wa UVCCM wameamua kuanzisha chama cha siasa ndani ya chama kingine.
Alisema baada ya kuamua kusema ukweli, uongozi wa umoja huo ulidai kuwa, yeye sio mwanachama wake kitu ambacho sio kweli, kwani yeye bado ni mwanachama hai wa chama hicho.“Wanadai walinivua uongozi mwaka 2009, lakini mwaka 2010 nilikuwapo kwenye Mkutano Mkuu wa CCM na nilisimamia kuhakiki kura za mgombea urais,” alisema Makonda na kuhoji:
“Sasa huku sio kutapatapa? Kama niliingia sehemu zote hizo wakati sio mwanachama, chama hiki kiko sawa?”Alisema tatizo lililopo sasa umoja huoni uongozi wa kitaifa na kwamba, ili kuboresha uachwe wilayani kwenye vijana na kitaifa uundwe upya.Kijana mwingine wa CCM, David Msuya, alisema anamshangaa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kukaa kimya na kuachia wanachama kulumbana badala ya kuwachukulia hatua.
Msuya alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa habari.
"Inashangaza Katibu Mkuu wa CCM kukaa kimya, badala ya kuwaita hawa wanaolumbana. Ukimya wake unanipa wasiwasi kwa kuwa haya yote anayaona na kuyasikia," alisema Msuya.
Alisema ni muhimu wanaCCM wakaacha kulumbana na kujenga chama kwa kuwa, hali hiyo haijengi bali inabomoa."Nimesikitishwa na UVCCM kuendelea kutoa matamshi ya kukidhoofu chama na wastaafu kutoa matamko yao," alisema.Msuya alisema ni vizuri UVCCM wakakaa na kufikiri sababu za kukosa majimbo uchaguzi uliopita, badala ya kulumbana.
Naye Moses Mashalla kutoka Arusha anaripoti kuwa, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, kupitia mkoa wa Mara, Anthony Mtaka, alisema malumbano hayo sio dalili nzuri kwa chama kinachoongoza serikali nchini.Mataka alisema malumbano hayo hayana tija kwa umma, huku akiwataka viongozi wanaolumbana kukumbuka dhamana ya utumishi na kura walizopewa kutumikia Watanzania.
"Malumbano kama haya sio mazuri kwa chama kinachoongoza serikali, kwani hayana tija kwa Watanzania, mimi ushauri wangu ni kwamba hawa viongozi wakumbuke ile dhamana na kura walizopewa kuongoza serikali," alisema Mtaka.
0 comments