Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - SERIKALI YATAMKA: Katiba mpya 2014

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SERIKALI IMESEMA MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA UTAANZA HIVI KARIBUNI NA ITAHAKIKISHA KUWA KATIBA MPYA INAPATIKANA MWAKA 2014.



SERIKALI imesema mchakato wa mabadiliko ya Katiba utaanza hivi karibuni na itahakikisha kuwa Katiba mpya inapatikana mwaka 2014.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Oliver Mhaiki, alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala inayoongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana, iliyotaka kufahamu jinsi serikali ilivyojipanga kwa mchakato huo.
Alisema maandalizi ya kuanza kwa mchakato huo yamekamilika na tayari muswada wake umeshapita katika vikao husika na kwamba kinachosubiriwa kwa sasa ni kufikishwa bungeni.
“Mchakato wa katiba itakayotokana na ridhaa ya wananchi utakamilika baada ya miaka miwili kutoka sasa. Wizara ilishaandaa waraka kuhusu suala hilo na ulishafikishwa katika kikao cha kamati ya ufundi ya serikali inayoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kwa hatua zaidi.
“Kamati ya Luhanjo ilishaujadili waraka na iliupeleka katika kikao cha baraza la mawaziri ambalo lilishaketi na kuupitisha waraka huo…hatua inayofuatia sasa ni waraka huo kupitiwa kama muswada kwa ajili ya kuwasilishwa kati ya mwezi Juni au lile Bunge la Novemba,” alisema Mhaiki.
Ufafanuzi huo ulitokana na maswali yaliyoulizwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Angellah Kairuki na Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), ambao kimsingi walitaka kujua Katiba mpya itapatikana lini na kutaka kujua nini kinaendelea tangu Rais Jakaya Kikwete atoe tamko lake kuhusu suala hilo.
Baada ya ufafanuzi huo, kamati hiyo iliipongeza serikali kwa maandalizi iliyoyafanya mpaka sasa na kuitaka iendelee kufanya maandalizi ya uhakika zaidi bila kubahatisha, kwani wanatekeleza agizo la rais.
Kwa upande wake Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, alisema wizara yake imejipanga vizuri ingawa imekuwa ikikabiliwa na changamoto hasa katika Idara ya Mahakama, kwa kuwa na upungufu wa mahakimu katika mahakama za mwanzo na wilaya nchini.
Kombani, alisema hivi sasa serikali imefanikiwa kuajiri mahakimu wa mahakama za mwanzo ambao ni 750 huku kukiwa na upungufu wa mahakimu 350, hali inayofanya mashauri ya kesi kuchelewa kusikilizwa kwa wakati.
“Naiomba kamati hii itambue wilaya zote 12 zilizoanzishwa katika Serikali ya Awamu ya Tatu hazina majengo ya mahakama ya wilaya, hali inayopelekea wananchi kutembea umbali mrefu kuzifuata mahakama zilipo na zaidi ya wilaya 30 hazina mahakimu,” alisema Waziri Kombani.
Alisema hali hiyo inasababishwa na ufinyu wa bajeti ya wizara hiyo pamoja na idara zake, ambapo kwa mwaka huu wa fedha unaoisha Juni mwaka huu walitengewa sh bilioni 499.4, ikiwa sambamba na idara zote.
Hata hivyo, Kombani alitoa wito kwa kamati hiyo kuhakikisha wanaunga mkono ombi lao la kutaka kuongezewa fedha katika bajeti ya mwaka huu ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Hoja na shinikizo la kutaka kuandikwa kwa Katiba mpya viliibuliwa kwa kasi mwishoni mwa mwaka jana na tamko la viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Tags:

0 comments

Post a Comment