Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - UVCCM: Dk. Slaa chaguo la vijana

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro (UVCCM) umeushutumu uongozi wa kitaifa wa umoja huo kwa kuwa dhaifu kiasi cha kusababisha vijana wengi nchini kumpa kura zao aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa.


Viongozi wa kitaifa wa umoja huo wametakiwa kujiuzulu kwenye nafasi zao kwa sababu ya kile kilichoelezwa kuwa wameshindwa kuongoza na badala yake wamekuwa wakitumiwa na mafisadi kutoa matamko ya kuwashambulia wanaopambana na ufisadi nchini.


Pia uamuzi wa kumteua kada wa siku nyingi wa CCM, Kingunge Ngombale- Mwiru, kuwa kamanda wa umoja huo umepingwa kwa madai kuwa hana sifa, kwani ameshapoteza umashuhuri na hawezi kwenda na kasi ya changamoto, kwa madai kuwa atapinga kila wazo jipya la manufaa ndani ya jumuiya hiyo.


Hayo yalisemwa juzi na mjumbe wa mkutano wa mkoa wa UVCCM mkoani Kilimanjaro, Paul Makonda, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Crane mjini Moshi.


Alisema viongozi wa UVCCM taifa ndio waliosababisha vijana wengi kujiunga, kukishabikia na kukipigia kura nyingi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita baada ya kushindwa kutoa mwelekeo na tumaini kwa vijana, jambo alilosema kuwa ndilo limechangia kuinyima CCM kura za vijana.


“UVCCM waseme gharama kubwa waliyoitumia katika kampeni za uchaguzi wa mwaka jana kulipia watoto wa vigogo kuzunguka nchi nzima kwa kisingizio cha kupiga kampeni zimeleta manufaa yapi? Iweje watu wanazunguka nchi nzima na mwishowe kundi kubwa la vijana wanakimbia kutoka CCM na kutua CHADEMA? Je, huu si usaliti wa wazi kufukuza vijana chamani na kuwapeleka CHADEMA?” alihoji Makonda huku akishauri viongozi waachie ngazi kwa ustawi wa UVCCM.


Alisema uongozi wa kitaifa wa UVCCM umejipambanua kama mawakala wa ufisadi kwa tabia yake ya kutoa matamko ya mara kwa mara yasiyo na tija kwa taifa zaidi ya kuwashambulia viongozi waandamizi na wastaafu wanaopinga ufisadi nchini.


Kwamba, hatua ya viongozi wa kitaifa wa UVCCM kuitaka sekretarieti ya CCM itoke madarakani inaashiria kuwa ni mambumbu wasiojua vema majukumu ya jumuiya za CCM.


“Wanasema viongozi wa serikali na wastaafu ambao CCM inawaheshimu na kuwapa nafasi Sitta (Samuel, Waziri wa Afrika Mashariki ) na Waziri Mkuu mstaafu Sumaye (Frederick) kuwa wanakosea kuongea nje ya vikao huku nao UVCCM wakitumia vyombo vya habari kuwakosoa nje ya vikao, jambo linaloonyesha uwezo wao kiutendaji ni mdogo,” alisisitiza Makonda.


Alisema kuwa aliamua kujitoa mhanga kulizungumzia hilo baada ya kuona vijana wenzake kutoka Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mbalimbali nchini hawakubaliani na namna mambo yanavyokwenda ndani ya umoja huo lakini wanashindwa kupinga kutokana na hofu ya kushughulikiwa.


Makonda alisema kuwa anguko la UVCCM kwa sasa linaonekana dhahiri kutokana na namna uongozi ulio chini ya Kaimu Mwenyekiti wake, Benno Malisa na Katibu Mkuu wake, John Shigela, ulivyokosa dira na mwelekeo, hali inayoifanya UVCCM ikose sifa ya kuwa jumuiya ndani ya CCM.


Alisema UVCCM imekuwa kama chama cha upinzani ndani ya CCM, akitolea mfano wa hatua ya umoja huo kupinga maaamuzi ya sekretarieti ya kumrudishia uanachama wa jumuiya hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Nape Nnauye, jambo alilowashauri kama wanashindwa kukubaliana na maamuzi sahihi ya CCM ni vema wakaachia ngazi na kuanzisha chama chao cha siasa.


“Hata kama kutumiwa huku kwa UVCCM ni kwa kwanza kuonekana duniani na kwa style hii misingi ya amani na utulivu inatikiswa kutokea ndani, ni nani atazuia …wanasema watafanya maandamano nchi nzima endapo mtu wanayemtaka kwa nafasi ya urais 2015 hapitishwi na chama, hivi hawa watu wana lengo zuri kweli? Kwa nini wasifanye maandamano kupinga malipo ya shilingi bilioni 94 ya Kampuni ya Dowans Tanzania Limited?” alihoji Makonda.


Aidha, alipinga uteuzi wa Hussein Bashe aliyedai mpaka sasa bado hajatoa majibu ya msingi juu ya utata wa uraia wake, halafu anapewa jukumu la kufanya utafiti wa mabadiliko ya kimuundo ya umoja huo, kwa madai kuwa hiyo ni mbinu na mkakati maalumu wa kusaka uongozi wa UVCCM 2012 na kwamba wanajiwekea mazingira ya kumpata rais wanayemtaka ateuliwe na CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2015.


“Mambo haya ndiyo yanasadifu uwezo mdogo wa kuamua mambo ya msingi ya vijana wa chama na taifa hili, badala yake unadhihirisha uwezo mkubwa wa kuamua mambo kwa maslahi ya mafisadi wachache ndani ya taifa hili.


“Na kwa vile viongozi wa UVCCM wanafanya kazi kwa maslahi ya mafisadi, basi hakuna dhambi nao wakijumuishwa kwenye kundi la mafisadi na waachie nafasi hizi ndani ya jumuiya na ndani ya CCM, waende wakaunde taasisi zao watakazofanya watakavyo,” alisema Makonda.


Mwanachama huyo wa UVCCM alishauri suala la kufanya utafiti wa kimuundo wa jumuiya hiyo lifanywe na wasomi au taasisi huru zenye wataalamu wasiofungwa na chama chochote, ambao watafanya utafiti kubaini walishindwa wapi na wafanye nini ili waweze kusonga mbele.
Tags:

0 comments

Post a Comment