IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BADALA ya kuendelea na mkakati wake wa kupambana na watu waliojenga klwenye maeneo ya wazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka atalazimika kutumia siku saba kutafakari barua ya mmiliki wa moja ya viwanja hivyo anayetaka aombwe radhi ndani ya muda huo kwa madai kuwa amechafuliwa.
Mmiliki huyo wa kiwanja hicho kilicho karibu na Hoteli ya Palm Beach jijini Dar es Salaam, Taher Muccadam pia ametishia kwenda mahakamani kudai fidia ya Sh2 bilioni iwapo Prof Tibaijuka, hatamuomba radhi.
Kiwanja hicho ni moja ya viwanja kadhaa ambavyo Prof Tibaijuka alisema ni vya serikali lakini wajanja wakavichukua kwa kutumia kisingizio cha viwanja vya wazi na hivyo kutaka virejeshwe serikalini.
Tibaijuka, ambaye aliambatana na katibu mkuu wa wizara wakati wa kukagua viwanja hivyo vilivyo ufukweni mwa Bahari ya Hindi, pia alitoa historia ya kila kiwanja hadi kilipovamiwa na kuwekwa majengo mapya.
Lakini Muccadam alifanya mkutano na waandishi wa habari jana na kuwaeleza kuwa maelezo ya Tibaijuka, ambaye alikuwa mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UNHABITAT), alimvunjia heshima mbele ya jamii na sasa anataka aombwe radhi ndani ya siku saba.
Notisi hiyo ya siku saba iliyotolewa jana na wakili wa kampuni ya Decoram attoneys imeeleza kuwa Waziri Tibaijuka alimvunjia heshima mmiliki huyo kwa kutamka kuwa alitoa rushwa ili kukipata kiwanja hicho.
“Amenivunjia heshima ndani na nje ya nchi na mimi nikiwa kama mwanasheria, nimeumia sana. Naamini sheria ni msumeno na inaweza kutoa haki kwa mtu yeyote,” alisema Muccadam katika notisi yake hiyo.
Muccadam alieleza kuwa alipata kiwanja hicho kihalali kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu baada ya pande zote mbili kufika mahakamani hapo na kuafikiana.
“Hii inaonyesha dhahiri kwamba wizara imekula matapishi yake kwani ndiyo iliyotoa vibali vyote halali, vikiwemo vya kubadilisha ramani na kupima tangu mwaka 1975,” alisema Muccadam.
Katika notisi hiyo Muccadam ameeleza kuwa kama waziri huyo hataomba msamaha katika muda huo aliompa, atamfikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Kiwanja hicho namba 1006 kilicho Upanga jirani na Hoteli ya Palm Beach ni kati ya viwanja ambavyo Profesa Tibaijuka alisema kuwa ni vya wazi na kwamba haviruhusiwi kuwa makazi.
Kwa mujibu wa Muccadam, kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa kwa hati namba 186164/25 iliyotolewa Januari Mosi mwaka 1975 kwa wamiliki wa kwanza ambao ni Shantaben Narottambahi Patel na Nilaben Girishumar Patel.
Alisema kiwanja hicho kilimilikishwa na Manispaa ya Ilala na miliki hiyo ilidumu kwa miaka 99 kabla yeye hajakinunua mwaka 2000.
Aliendelea kueleza kuwa mwaka 2000, kiwanja hicho kilifutwa kwa makosa na suala hilo likapelekwa Mahakama Kuu na kufunguliwa kesi namba 70/2004.
Baadaye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilipendekeza mgogoro huo umalizwe nje ya mahakama.
Aliendelea kueleza kuwa wizara na Manispaa ya Ilala vilishindwa kutekeleza makubaliano hayo hivyo ilimlazimu kufungua kesi nyingine Mahakama Kuu namba 107/2006.
"Niliendelea na malumbano hayo Mahakama Kuu kwa muda wote huo na hatimaye nilishinda kesi na kurudishiwa kiwanja hicho na kwamba, mahakama ilikubali nilipwe fidia ya dola 6 milioni za Kimarekani kama gharama za ujenzi huo," alisema Muccadam.
Muccadam alieleza kuwa alinunua kiwanja hicho ili ajenge jengo la ghorofa 22, lakini tangu wakati huo ameshindwa kuanza ujenzi kutokana na kuwepo kesi mbalimbali mahakamani.
You Are Here: Home - - Mmiliki Palm Beach ampa Tibaijuka siku saba
0 comments