Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mahakama yataka serikali kugharimia kesi za uchaguzi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeitaka serikali ibebe mzigo wa gharama zote za uendeshaji wa kesi za uchaguzi zilizofunguliwa katika vituo mbalimbali vya mahakama hiyo, kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.
Mahakama pia imetoa angalizo kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiwa mdau mkubwa katika kesi hizo kuwa lazima ijiandae na kuwezeshwa ili kuruhusu mashauri hayo, kuendelea na kumalizika kwa wakati bila kukwama.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Jaji Kiongozi Fakihi Jundu, alisema kufikia Desemba 10 mwaka huu jumla ya kesi 43 za kupinga matokeo ya ubunge, zilikuwa zimefunguliwa katika vituo 11 kati ya 13 vya Mahakama Kuu ya Tanzania

Uwingi wa kesi hizo za uchaguzi katika uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa mzigo mkubwa ambao serikali italazimika kuubeba kugharimia gharama za uendeshaji wake.
Jaji  Jundu alisema katika kuyashughulikia mashauri hayo kwa wakati na kwa haki, inakadiriwa kuwa kiasi cha Sh.2.263 bilioni kitahitajika.

"Izingatiwe kuwa ili haki itendeke na ionekane kutendeka, jaji hatasikiliza kesi katika kituo chake cha kawaida cha kazi. Tutalazimika kuwasafirisha kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine," alisema Jaji Jundu
Alibainisha kuwa lengo la kuwahamisha majaji hao kwenda kusikiliza kesi hizo nje ya vituo vyao, ni kuruhusu haki kutendeka kwa kuondoa dhana kwamba jaji anaweza kuwa na mawasiliano na uhusiano na upande mmoja katika kesi hiyo.

"Kwa kuzingatia yote hayo, itagharimu kiasi cha Sh.52,644,000 kwa kila kesi. Hivyo tunahitaji kiasi cha Sh.2,263,692,000 kuendesha mashauri haya. Fedha hizi sisi hatuna na mzigo ambao serikali lazima iubebe,"alisema.
Jaji Jundu alisema tayari wameishaiandikia Hazina kueleza mahitaji ya fedha hizo na kwamba baada ya majaji kutoka likizo Februa mwakani na kama serikali itakuwa imeshatoa fedha hizo, kazi ya kusikiliza kesi hizo itaanza mara moja.

Alisema uendeshaji wa kesi hizo ni gharama kubwa lakini kwa kuwa serikali ya Tanzania  inaamini katika demokrasia, haina budi kubeba mzigo huo kwa kuwa demokrasia ni gharama.
"Serikali lazima itoe hela kwa hili, haiwezi kuwepa isipotoa zitakwama, sisi tunatekeleza matakwa ya katiba," alisisitiza Jaji Jundu wajibu wa serikali kugharimia kesi hizo.
"Tunaiomba serikali kuiwezesha mahakama ili itemize jukumu hili muhimu katika kulinda heshima ya nchi yetu," alisisitiza.

Akizungumzia utaratibu wa uendeshaji wa kesi hizo, Jaji Jundu alisema kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi namba 1 ya mwaka 1985 kifungu cha 115 (2),mashauri hayo yanapaswa kuwa yamekamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu kufunguliwa.
Jaji Kiongozi alisema inakisiwa kuwa kila kesi itasikilizwa kwa muda wa siku zisizopungua 45 na kwamba kila kesi itakuwa na mashahidi 15.

Hata hivyo alisema kisheria iwapo muda huo utaisha kabla ya kesi hizo kumalizika, Waziri wa Katiba na Sheria kwa kujadiliana na Jaji Mkuu wataongeza muda wa miezi sita wa kusikiliza mashauri hayo.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa kesi hizo za uchaguzi, mahakama imezipa kipaumbele na kwamba tayari wameshajipanga katika kuzishughulikia kikamilifu.

Akielezea jinsi mahakama ilivyojipanga kushughulikia kesi hizo alisema Septemba 17 kilifanyika kikao cha Majaji Wafawidhi katika Hoteli ya Kunduchi jijini Dar es Salaam  ambapo walijadili sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya uchaguzi.
Tags:

0 comments

Post a Comment