IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SOKO la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limeanzishwa huku Tanzania ikishauriwa kuimarisha sekta ya usafirishaji hususan katika upande wa Bandari ya Dar es Salaam.
Endapo Tanzania itafanikiwa kuimarisha huduma zinazotolewa bandarini, inaweza kunufaika na soko hilo na kuongeza wawezekaji wa ndani na nje ya nchi.
Tanzania imetakiwa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo, kama zilivyo nchi nyingine duniani na hatimaye kukuza uchumi wao.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Balozi Juma Mwapachu, amezuru katika Bandari ya Dar es Salaam na kujionea jinsi kazi zinavyofanyika.
Katika ziara hiyo, aliyoongozana na baadhi ya wajumbe wa EAC, alieleza changamoto mbalimbali ambazo wanachama wanakabiliwa nazo.
Balozi Mwapachu anasema umefika wakati wa kuamka na kuendeleza bandari ili kuinua uchumi.
“Hii ni changamoto kwetu sote nchi wanachama, kuwekeza zaidi kwenye sekta hii, endapo tutaimarisha miundombinu yake basi bandari itachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuzaji uchumi wa nchi,” anasema Mwapachu.
Anasema nchi wanachama wa EAC ikiwemo Tanzania, zinatakiwa kuangalia miundombinu ya bandari ili kuleta ufanisi wa huduma za kupakua na kupakia bidhaa zinazosafirishwa ndani na nje ya nchi.
Balozi Mwapachu anasema ili nchi iweze kutumia na kunufaika ipasavyo na fursa hii ya ushirikiano, maboresho, katika sekta ya miundombinu, hasa ya bandari, si ya hiari kwa sasa, bali ni lazima.
Amefafanua kwamba Bandari ya Dar es Salaam bado inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za mrundikano wa bidhaa ambazo zinakaa kwa muda mrefu bandarini bila kusafirishwa, hali inayoweza kusababisha wadau na wafanyabiashara wakubwa kushindwa kuitumia huduma.
“Najua bado kuna changamoto kwenye Bandari ya Dar es Salaam, lakini kubwa kuliko zote ni ya kuziweka bidhaa muda mrefu bila kupakuliwa au kusafirishwa, hali hii inaweza kuwavunja moyo wawezekaji na wafanyabiashara wakubwa kutumia bandari hii,” anasema.
Balozi Mwapachu anasema kwa sasa Tanzania inapaswa kufikiria jinsi ya kuhudumia watu zaidi ya milioni 130 ndani ya EAC, jukumu ambalo linahitaji maboresho ya hali ya juu katika mfumo wa bandari, ikiwa ni pamoja na kupata teknolojia za kisasa, kuondoa vikwazo vinavyochelewesha upakuzi na kuongeza uwezo wa uhifadhi wa bandari zetu.
Anasema jumuiya ya kimataifa ina imani kubwa na ushirikiano huu wa nchi za Afrika Mashariki hasa baada ya kuonyesha mafanikio katika miaka mitano ya umoja wao.
Kutokana na mafanikio hayo, tayari jumuia hiyo imeonyesha nia ya kutaka kuusaidia umoja huo, kwa sharti kuwa misaada hiyo itasimamiwa na menejimenti ya jumuia.
“Ni wazi kuwa maboresho katika bandari yatahitaji fedha nyingi ambazo Mamlaka ya Bandari hazina kutoka katika vyanzo vyao, hivyo wanahitaji msaada. Bandari haiwezi kwenda kukopa katika jumuia za kimataifa pekee, ni lazima tuwasimamie kwa kuwa jumuia hizi zinafanya kazi katika ngazi ya jumuia, na hili ndilo lengo la ziara yetu,” anasema.
Kwa mujibu wa Mwapachu, jumuia za kimataifa zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya EAC kwa lengo la kuwekeza, hivyo ni jukumu la nchi wanachama kuboresha miundombinu itakayovutia uwekezaji wenye tija na manufaa kwa nchi zao.
“Napokea simu nyingi kutoka nchi mbalimbali, nimeshapokea kutoka Ufaransa na wanatupongeza kwa hatua tuliyofikia, tumekuwa mfano kwa nchi za Afrika.
“Baadhi ya nchi wamenialika nikatoe semina ya jinsi tulivyoweza kufanikisha mambo haya, haitakuwa vema tukashindwa kutumia nafasi hizi ndio maana tunataka kusimamia uboreshaji wa bandari zetu sisi wenyewe,” anasema.
Mwapachu anasema ziara hiyo itakuwa endelevu na wamepanga kuzifikia hata bandari za Mtwara, Tanga, Mombasa, Mwanza na katika ukanda wa Ziwa Victoria kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji, hali anayosema itakuwa chachu katika maendeleo ya sekta za utalii na biashara.
Anasema endapo sekta ya mawasiliano ikiwemo bandari itakuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma, kutavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje.
Katika ujumbe huo, anasema kuingia katika soko la pamoja na kuibuka mshindi kunahitaji kuwa na mbinu bora ili kuwashinda nchi wananchama kwa kuwekeza nguvu zake zaidi kwenye sekta husika.
“Kuingia katika soko la pamoja na kuibuka mshindi kunahitajika mbinu bora na tofauti zitakazosaidia kuwashinda nchi nyingine wanachama,” anasema Balozi Mwapachu na kuongeza kuwa kuna miundombinu ya mawasiliano mengine kama vile barabara na reli, lakini hii ya bandari ni zaidi ya hivyo.
Meneja wa Bandari, Idd Mkwata, anasema bado wanakabiliwa na matatizo ya uwezo mdogo wa bandari kulinganisha na matakwa ya wateja, miundombinu hafifu na teknolojia duni ambazo hazikidhi mabadiliko ya teknolojia, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa urasimu wa usimamizi wa shughuli za upakuaji na uhifadhi.
Anasema kizazi cha sasa kinahitaji vifaa vya kisasa na bora vya uhakika ili kufanya kazi kubwa kwa haraka na bora.
Katika kupunguza changamoto ya mrundikano wa bidhaa bandarini anasema wana mpango wa kupanua eneo, upanuzi huo utafanyika muda wowote kuanzia sasa pindi izitakapopatikana pesa za kutosha.
“Ni kweli kwamba kuna changamoto ya mrundikano wa bidhaa na makontena bandarini, tuna mpango wa kupanua eneo letu ili kuondokana na kero hii. Tutajenga eneo huko Bagamoyo na tunaamini kwa kiasi kikubwa itakuwa ni suluhisho la tatizo hili,” anasema na kuongeza kuwa Mamlaka ya Bandari iko tayari kushauriwa na wadau wengine kutoka nje na ndani ya nchi katika kuboresha huduma ili kukuza uchumi.
You Are Here: Home - - Soko la Pamoja Tanzania kunufaika?
0 comments