Obama aliapishwa kwa mara ya pili tena juzi kwa sababu ya kutotamka neno moja wakati akila kiapo katika sherehe zilizofanyika Jumanne wiki hii.
Jaji Mkuu, John Roberts, aliyemuapisha wakati wa sherehe za Jumanne, alilazimika kumuapisha tena Obama katika Ikulu ya Marekani baada ya kuruka neno moja wakati akimuapisha.
Taarifa iliyotolewa baadaye na Ikulu ilisema kwamba, maamuzi ya kurudia kiapo hicho juzi, yalichukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Akizungumza kwa utani kabla ya kula kiapo chake cha pili, Obama alinukuliwa akisema, "Tumeamua kufanya hivyo kwa kuwa lilikuwa ni jambo la kufurahisha…tutarudia tena kufanya vilevile taratibu."
Katika tukio la juzi, tofauti na alivyofanya Jumanne, Obama aliapa pasipo kulazimika kushika Biblia.
Mbali ya hilo katika uapaji wa mara ya pili mkewe Michelle ambaye katika kiapo cha kwanza alimshikia Biblia hakuwapo.
Kama hiyo haitoshi, tukio zima la marudio ya kiapo hicho, lilifanyika huku idadi ya watu walioshuhudia ikiwa ni ndogo, ikilinganishwa na mamilioni ya mashuhuda waliohudhuria sherehe za mwanzoni mwa wiki hii.
Habari zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu ambao pia hawakushuhudia kurudiwa upya kwa kiapo hicho ni waandishi wa habari.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kwamba, kwa mujibu wa Katiba, Rais anapaswa kuapa kwa kutamka; ‘‘Mimi.. ninaapa kwamba nitaitumikia Ofisi ya Rais wa Marekani kwa uaminifu na kwamba nitaitunza, kuilinda na kuitetea Katiba ya Marekani kwa kadri ya uwezo wangu.
Hata hivyo, kumbukumbu zinaonyesha kuwa, wakati wa kiapo cha kwanza, Jaji Mkuu, Roberts alianza kwa kusahau kutamka maneno "kwa uaminifu" jambo lililomlazimisha afanye masahihisho muda mfupi baadaye baada ya Obama kusita kwa muda kutokana na kile kilichoonekana kulitambua kosa hilo.
Alipofanya marejeo ya kiapo hicho baada ya mara ya kwanza kusita, safari hii aliyefanya kosa la kulisahau neno ‘uaminifu’ alikuwa Obama ; kwani aliyekosea mara ya kwanza alikuwa Jaji Roberts!
Obama anakuwa Rais wa tatu kurudia kula kiapo; marais wengine wawili, Calvin Coolidge na Chester Arthur, nao walilazimika kurudia viapo vyao, baada ya kufanyika kwa makosa kama hayo.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, mwaka 1929, Jaji Mkuu, William Taft aliongeza neno jipya ‘kuimarisha’ katika kiapo wakati akimuapisha Rais Herbert Hoover huku akililiondoa neno ‘kuilinda’.
0 comments