Dereva wa ajali ya gari Arusha ashitakiwa kwa makosa 45
DEREVA wa Kampuni ya Bonite Bottlers, aliyesababisha ajali iliyoua watu 16 na kujeruhi wengine 17, Daniel Lali, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa 45.
Mwendesha Mashitaka, Haruni Matagane, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, George Habeti, alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa anakabiliwa na makosa 16 ya kusababisha vifo na 17 ya kujeruhi abiria waliokuwa ndani ya basi lenye namba za usajili T 799 AWR.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo, dereva huyo ambaye alikuwa akilia muda wote aliokuwa kizimbani, anakabiliwa na makosa mengine ya kuharibu daraja na kusababisha hasara kwa serikali, hivyo kufanya idadi ya makosa yake kufikia 45.
Dereva huyo aliyekuwa akiendesha gari hilo lenye namba za usajili T 417 AMM, alifikishwa mahakamani hapo jana, akiwa amevunjika mguu na hadi sasa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mount Meru, akiwa rumande. Kesi hiyo itatajwa Februari 2 mwaka huu.
Wakati mshitakiwa huyo akisomewa mashitaka hayo, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James Kombe, alikuwapo kushuhudia kesi hiyo.
Kombe aliyesafiri jana kutoka Dar es Salaam kwa ajali hiyo, alisema kuanzia sasa madereva wazembe watakabiliwa na adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Katika hatua nyingine, baadhi ya majina ya watu waliofariki dunia juzi katika ajali hiyo iliyohusisha magari matano yaliyogongana katika daraja la Mto Nduruma, yamejulikana.
Kutambuliwa kwa miili hiyo kunafanya idadi yao kufikia 13 kati ya miili ya watu 16 waliofariki dunia katika ajali hiyo ya aina yake.
Waliotambuliwa ni pamoja na askari Polisi, PC Hamidu, mzaliwa wa Mwanga, mkoani Kilimanjaro na mwenzake PC Abinieli, kutoka mkoani Mbeya.
Miili ya askari hao, ilisafirishwa jana kwenda katika mikoa waliyozaliwa, huku mwili wa Abinieli, ukiwa katika hali mbaya kutokana na kuharibika.
Wengine waliotambuliwa ni David Ngunda (21), Maina Kireri, Nanganya mkazi wa Ngulelo, Anasitazia, mkazi wa Burka, Alice Kinjaa, Samweli Chuwa, mkazi wa Monduli na mtoto wa kike, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 10, ambaye hata hivyo jina lake halijajulikana. Majina ya maiti saba hadi sasa bado hayajatambuliwa.
Kwa upande wa majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo ni Exaudi Mbise (31), mkazi wa Akeri, Deogratius Gabriel (18), mkazi wa Mto wa Mbu, Leka Chuwa (73), mkazi wa Majengo na Sebastian Tarimo (26), mkazi wa Monduli.
Wengine ni Ailali Damian, mkazi wa Mbauda, Alyoce Joachim, mkazi wa Moshi, Eliya Abdallah (18), mkazi wa Moshi, Dismas Patrick, mkazi wa Ngarenaro, Isaac Angalili (15), mkazi wa Majengo, Scolastical Samson (65), mkazi wa Moshi Kibosho na Josephine Bonitas (17), mkazi wa Moshi, Rombo.
Wengine ni Emily Joseph, mkazi wa Moshi, Maria Apolinari, mkazi wa Rombo, Hamisi Majala na Elizabeth Patrick (21) na wengine saba walitibiwa na kuruhusiwa kurejea makwao.
Akizungumza katika ibada ya mazishi kwenye kambi ya askari wa Jeshi la Polisi, mjini Arusha, Kaimu Kamanda mkoani hapa, Robert Boaz, aliwapa pole ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huo.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori lenye namba za usajili T 424 AMM, mali ya Kampuni ya Coca Cola, lililokuwa likitoka Moshi kwenda mkoani Arusha, likiwa na kreti tupu za soda, kuligonga basi aina ya Coaster, lenye namba T 799 AWR.
Alisema baada ya kuligonga basi hilo lililokuwa na abiria kutoka Arusha, kwenda Moshi, nalo liligonga basi dogo aina ya Hiace, lenye namba za usajili T 607 ANW, ambalo nalo lililigonga gari jingine aina ya Land Cruiser, namba za usajili T 820 AMC.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, amesema ajali mfululizo zinazotokea nchini hazina budi kuwekewa mikakati madhubuti ya kudhibitiwa, kwani mamlaka husika zina uwezo huo, anaripoti, Mwandishi Esther Mbussi wa jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alisema hayo katika taarifa yake ya salamu za rambirambi aliyoitoa jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidore Shirima, kutokana na vifo vya watu 16 waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea eneo la daraja la Mto Nduruma, mkoani humo juzi.
“Kwa masikitiko na huzuni kubwa, napenda kwa dhati ya moyo wangu kukutumia salamu za rambirambi wewe Mkuu wa Mkoa wa Arusha kutokana na vifo vya wenzetu 16 waliofariki papo hapo katika ajali hiyo, kupitia kwako nawapa pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu na namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, Amin.
“Kwa watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo, natambua maumivu makali mnayoyapata hivi sasa, hivyo namuomba Mungu awape moyo wa uvumilivu na awawezeshe kupona haraka ili muungane tena na familia, ndugu na jamaa zenu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais alisema, serikali haitaendelea kuvumilia kutokea kwa ajali kama hizo, wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria ya usalama barabarani zipo.
0 comments