Mrema wa TLP atangaza kumvaa Kimaro wa CCM Vunjo | |||||||
Na Zaina Malongo BAADA ya kushindwa kufua dafu mara tatu katika mbio za urais, hatimaye mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema amerejea kwenye kinyang'anyiro cha ubunge baada ya kutangaza kuwa atapambana na Aloyce Kimaro kuwania jimbo la Vunjo. Mrema, ambaye amewahi kugombea urais akiwa na NCCR Mageuzi na baadaye TLP, alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20 kabla ya kutofautiana na serikali na baadaye kujiunga na upinzani katika miaka ya tisini. Wakati hali ikionekana kumuendea kombo Kimaro kwenye jimbo hilo, Mrema anaonekana kutaka kutumia mwanya huo kurudi Vunjo ambako TLP ina nguvu kubwa. Mwenyekiti huyo wa TLP aliliambia gazeti hili jana kuwa baada ya kumtikisa Kimaro katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu ambao chama chake kimeshinda katika vijiji 20 na vitongoji 48 dhidi ya vijiji 47 vya CCM, sasa anajipanga kwenda jimboni humo kugombea ubunge mwakani. "Baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, sasa namtangazia rasmi Kimaro kwamba mwakani naenda Vunjo kulichukua jimbo langu. Kimaro ameshindwa kuwasaidia wananchi ndio maana wamemzomea," alisema Mrema alipoongea na Mwananchi jana. Mrema, ambaye alikuwa waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya awamu ya pili, alitoa tamko hilo wakati akizungumzia tuhuma za Kimaro kwamba wanachama wa TLP ndio waliomzomea wakati akihutubia mkutano wa uliofanyika mji mdogo wa Himo ulio kwenye jimbo la Vunjo, Moshi Vijijini Jumatatu iliyopita. Kimaro alishikwa na maswahibu hayo baada ya kundi la takribani watu 100 wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa chama hicho kumpigia kelele likisema "hatukutaki", muda mfupi baada ya kuwatambulisha wenyeviti wa TLP waliohamia CCM. Kimaro alidai kuwa kundi hilo ni la watu wachache wa TLP waliotumwa na Mrema kwenye mkutano wake. “Kundi lilozomea liliandaliwa na Augustino Mrema lililetwa kwenye mkutano wangu na daladala kutoka eneo la Njia Panda, ilipo gesti house na baa yake inayoitwa Twiga. Wao waendelee kuzomea mimi sitishiki na siachi ngozi yangu ngumu nitapambana nao mpaka kieleweke,†alisema Kimaro.  Hata hivyo, Mrema alilieleza gazeti hili jana kuwa Kimaro hakuzomewa na wanachama wa TLP bali alizomewa na wananchi wa jimbo hilo baada ya kuwakera kwa hoja alipokuwa akizungumza jukwaani. Alisema Kimaro aliwakera wananchi hao kwa kutozungumzia kero ya maji ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu na badala yake akaanza kupiga siasa ambazo hazikuwasaidia. "Mbunge huyo kuzomewa Vunjo si mara ya kwanza," alidai Mrema. "Alishazomewa sana na wananchi sehemu nyingi... alishazomewa Kilema Kaskazini, Kilema Kusini, Marangu Magharibi, leo anashanga nini kuzomewa Vunjo?" Alisema kutokana na Kimaro kuonyesha kushindwa kuwahudumia wananchi, sasa anaamua kurudi jimboni humo kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwakani. "Kimaro haliwezi jimbo la Vunjo... ni bora angetafuta jimbo jingine mapema kwa kuwa mimi sasa narudi kumnyang'anya ubunge," alitamba Mrema ambaye baada ya kuondoka CCM alikwenda jimbo la Temeke na kushinda katika uchaguzi mdogo. Lakini Kimaro hakuonekana kutikishwa na uamuzi huo wa Mrema baada ya Mwananchi kuwasiliana naye kutaka maoni yake. "Kama anakuja aje, lakini akumbuke yeye ni mtu wa kushindwa tu... kushindwa hakuanza leo; alishindwa mwaka 1995, 2000, 2005 haoni kwamba ni mchovu na kachoka? "Mrema kafulia miaka yote hii kwenye urais, mwache aje atatukute tukimsubiri na atafulia tena. "Sio Mrema tu, amefulia yeye na TLP yote , TLP sio chama cha kitaifa, ina watu wawili tu; yeye na kiongozi mmoja hapa Vunjo, mbaya zaidi wote wamefulia, mwenyekiti kafulia na chama kimafulia." Kimaro alisema hatishwi na ujio wa Mrema jimboni humo kwa kuwa ushindi wake umeanza kujidhihirisha katika matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao KImaro alidai CCM ilishinda vijiji 48, TLP 19 Chadema 10 na NCCR Mageuzi kiti kimoja. |
You Are Here: Home - - Mrema wa TLP atangaza kumvaa Kimaro wa CCM Vunjo
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments