IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WATU 24 wamekufa na wengine 56 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Arusha kwenda Mwanza kupasuka tairi na kupinduka wilayani Nzega.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora Liberatus Barlow, ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kitangiri na Migua kiasi cha kilomita takribani 12 kutoka Nzega mjini.
Vifo hivyo pia vimethibitishwa na Daktari wa Wilaya ya Nzega, Dk. John Mombeki ambaye alisema wanne kati ya majeruhi hao wamekimbizwa Bugando kwa kuwa hali zao ni mbaya.
Alisema majeruhi wengine 52 wamelazwa Hospitali ya Nzega.
Ajali hii kubwa ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini tangu kuanza mwaka 2010 ilihusisha basi aina ya Scania T316 AZR mali ya Kampuni ya AM Coach na lililokuwa likitokea Arusha kwenda Mwanza.
Januari mwaka huu ajali nyingine mbaya ilitokea Mkoa wa Tanga ambapo watu 26 walifariki dunia, 25 papo hapo na mwingine hospitalini baada ya basi la abiria la Kampuni ya Tashrif walilokuwa wakisafiria, kuligonga lori la magogo katika Kijiji cha Hale-Kijijini wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Ajali hiyo ilitanguliwa na nyingine iliyotokea Januari 4, mwaka huu ambapo watu 11 wa familia moja wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro walikufa eneo la Uchira Moshi Vijijini, wakitokea katika shughuli ya kipaimara wilayani Hai.
Katika ajali ya Nzega ambayo ilitokea majira ya saa kumi jioni Kamanda Barlow alisema kwamba bado wanamtafuta dereva wa gari hilo aliyejulikana kwa jina moja la Robert ambaye hawajui kama ni miongoni mwa waliokufa au ametoroka.
Kamanda huyo alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, sababu ya ajali hiyo ni mwendo kasi ambapo dereva alishindwa kumudu gari lake baada ya tairi kupasuka. Alisema eneo hilo lina lami na lililonyooka hali ambayo inaweza kuleta ushawishi wa dereva kuendesha kasi.
Kamanda Barlow alisema kwamba tairi lililopasuka ni la mkono wa kushoto.
Hii ni mara ya pili kwa ajali kutokea katika eneo hili la Kitangiri na Migua katika kipindi cha miezi mitatu. Ajali nyingine ilihusisha basi dogo la abiria ambalo lilijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli Desemba mwaka jana. Katika ajali hiyo mtu mmoja alikufa.
Kamanda Barlow ambaye wakati anazungumza na gazeti hili alikuwa akielekea Nzega amesema kwamba atatoa taarifa kamili leo.
"Naelekea eneo la ajali, watu waliokufa ni wengi na majeruhi ni wengi na kwa Hospitali ndogo ya Nzega haiwezi kumudu, nakwenda huko kuona tutafanya nini" alisema Kamanda Barlow.
Katika ajali hiyo waliokufa ni wanaume watu wazima 14 na wanawake 6 wakati watoto ni wanne, wa kike wawili na wa kiume wawili wote wakiwa chini ya umri wa mwaka mmoja.
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.
You Are Here: Home - - Ajali mbaya yaua 24
0 comments